HALMASHAURI KIGAMBONI KUFUNGUA KIDATO CHA TANO,SITA JULAI MWAKA HUU

 Muonekano wa ubavuni wa jengo la bweni la wanafunzi  
  moja ya chumba cha wanafunzi ndani ya bweni 
 korido la moja ya bweni litakalotumiwa na wanafunzi wa kidato cha tano
 ujenzi wa jengo la utawala ukiendelea
moja ya jengo la maabara ya kisayansi
 baadhi ya vifaa vya majaribio ka vitendo vilivyopo ndani  ya maabara ya sayansi
 baadhi ya vifaa kwaajili ya mafunzo kwa vitendo
Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni inatarajia kufungua kidato cha tano na sita Julai mwaka huu katika Shule ya Sekondari Nguva kwa kuwa na wanafunzi 160 wa kiume pekee ikiwa na michepuo ya PCM,PCB,HGE na EGM. 
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni Bw.Stephen Katemba amesema kuwa katika kutatua changamoto ya ukosefu wa Shule ya Sekondari yenye kidato cha tano na sita kwenye Halmashauri, na kutimiza maelekezo ya Serikali kwa kila Halmashauri kuwa na shule ya kidato cha tano na sita, Manispaa iliamua kuboresha miundombinu ya Shule ya Nguva ili iweze kukidhi mahitaji hayo. 
Aidha amesema kuwa mradi huu unatekelezwa kwa thamani ya shilingi 492,864,576 kwa kushirikiana na Serikali kuu, ambapo Serikali kuu imeweza kuchangia kiasi cha shilingi 259,000,000 na vyanzo vya ndani vya Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni ilichangia shilingi 233,864.576. 
Mkurugenzi amesema kwamba ili kuhakikisha Shule ina hadhi ya kidato cha tano na sita kwa mujibu wa vigezo vya wizara, ujenzi wa mabweni mawili kwaajili ya wanafunzi, vyoo, ujenzi wa daharia ambao bado unaendelea, ujenzi wa madarasa manne na ununuzi wa madawati, ununuzi wa vitanda kwaajili ya mabweni ya wanafunzi, ukarabati wa maabara ya sayansi na ujenzi wa jengo la utawala linalojengwa kwa juhudi za Mkuu wa Mkoa Mh. Paul Makonda vimefanyika . 
Mkurugenzi amesema kuwa lengo kuu ni kuhakikisha masomo ya kidato cha tano na sita yanatolewa kwa watoto wanaomaliza kidato cha nne kwa shule za sekondari za Kigamboni. 
Kukamilika kwa mradi kutawezesha kuongeza idadi ya wanafunzi watakaojiunga na kidato cha tano na sita,kuchochea maendeleo ya elimu katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni kwa kutoa fursa pana kwa wanafunzi kujiunga na elimu ya juu. 
Ameongeza kuwa ujenzi wa bwalo la chakula litakalowawezesha wanafunzi kutumia kwaajili ya chakula linaendelea kujengwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. 
Imeandaliwa na: 
Kitengo cha Teknolojia, Habari na Mawasiliano 
Halmshauri ya Manispaa ya Kigamboni 
13/04/2018

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni