Na Munir Shemweta, Morogoro
Waziri
wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi amesisitiza umuhimu wa
kuwashirikisha watumishi katika mipango ya uendeshaji Taasisi kwa kuwa
suala hilo lipo kisheria.
Aidha,
alisema kwa miaka yote Serikali imekuwa ikisisitiza Taasisi kujenga na
kutekeleza utaratibu wa kushirikisha watumishi na hali hiyo inatokana na
ukweli kuwa palipo na watumishi wengi pana mawazo mengi.Profesa Kabudi
alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati akifungua mkutano wa kumi na tatu
wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania
uliofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA)
mkoani Morogoro.
‘’Ushirikishwaji
watumishi kwenye mipango ya uendeshaji ofisi unasaidia kupata mawazo
mengi na mapya yanayoweza kurahisisha uendeshaji wa ofisi na kutoa fursa
ya kusikiliza kero na changamoto kwenye uendeshaji wa Taasisi na
kushirikiana katika kutafuta ufumbuzi’’ alisema profesa Kabudi.
Aliongeza
kuwa, kwa kushirikiana na watumishi ni dhahiri wanapata morari wa
kushiriki kikamilifu kwenye utekelezaji wa mipango ya taasisi ambayo wao
wenyewe walishiriki kuiandaa.Waziri huyo wa Katiba na Sheria alisema,
ushirikishwaji unafanywa kupitia baraza la wafanyakazi kwa kuwa baraza
ni chombo kinachowashirikisha wafanyakazi katika kupanga , kusimamia na
kutekeleza mipango mbalimbali inayohusu shughuli za kazi za Taasisi kama
zilivyoainishwa katika sheria za nchi.
Kwa
mujibu wa Profesa Kabudi, Mabaraza hutoa fursa kwa wafanyakazi kushiriki
katika maamuzi mbalimbali na kuboresha uhusiano baina ya wafanyakazi na
uongozi pamoja na mazingira ya utendaji hasa mahala pa kazi hivyo
baraza ni chombo cha kuimarisha na kuboresha demokrasia mahala pa kazi.
Amewataka
wajumbe wa baraza wa Tume ya Kurekebisha Sheria kuzingatia suala la
nidhamu kazini, misingi ya kazi na kutekeleza majukumu kwa kuzingatia
sheria, kanuni, taratibu. Aidha, alitaka uzembe kazini upigwe vita na
suala la kufanya kazi kwa mazoea kukomeshwe na kubainisha
kuwa,vipaumbele viwekwe katika kulinda rasilimali za Tume na kuwa na
nidhamu katika matumizi ya fedha na mali zake.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Kurekebisha
Sheria ambaye ni Katibu Mtendaji Tume Casmir Kyuki alisema katika
kipindi cha Julai 2017 hadi Machi 2018 Tume yake imeweza kutekeleza
majukumu yake kama yalivyoainishwa katika bajeti.
Ameyataja
majukumu hayo kuwa ni kufanya mapitio ya Mfumo wa Sheria Unaosimamia
Haki Jinai, Sheria ya Ushahidi, Uchambuzi wa Kesi za Mahakama ya Rufaa,
Mfumo wa Sheria Unaosimamia Huduma ya Ustawi wa Jamii, Mfumo wa Sheria
za Ufilisi pamoja na kutoa elimu ya sheria kwa umma.
Ameishukuru
serikali kwa mabadiliko makubwa iliyoyafanya katika sekta ya sheria
kupitia tangazo la serikali namba 48,49 na 50 ambapo yameleta muundo
mpya kwa kuanzishwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai na ile ya
Wakili Mkuu wa Serikali ili kuongeza tija na ufanisi katika utendaji
kazi.
Waziri
wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi akifungua mkutano wa
Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Kurekebisha Sheria uliofanyika katika
Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine, kushoto ni Katibu Mtendaji wa Tume Casmir
Kyuki na kulia ni Katibu wa Baraza Ambokile Mwakasungula (Picha na
Munir Shemweta-TUMESHERIA)
Katibu
Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Casmir Kyuki (Kushoto)
akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Waziri wa Katiba na Sheria
Profesa Palamagamba Kabudi kufungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa
Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania uliofanyika katika Chuo Kikuu cha
Kilimo Sokoine mkoani Morogoro, kulia ni Katibu wa Baraza Ambokile
Mwakasungula (Picha na Munir Shemweta-TUMESHERIA)
Waziri
wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi akimsikiliza Katibu
Msaidizi wa Tume ya Kurekebisha Sheria Khalist Luanda mara baada ya
kufunguka mkutano wa Baraza la Wafanyakazi Tume ya Kurekebisha Sheria
uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine mkoani Morogoro,
katikati ni Katibu Msaidizi wa Tume (Idara ya Mapitio) Angelah Bahati
(Picha na Munir Shemweta-TUMESHERIA)
Sehemu
ya Wajumbe Baraza la Wafanyakazi la Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania
wakimsikiliza Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi
(hayupo pichani) wakati akifungua mkutano huo uliofanyika Chuo Kikuu cha
Kilimo Sokoine mkoani Morogoro.
Waziri
wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi akiwa katika picha ya
pamoja na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi Tume ya Kurekebisha Sheria
katika Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine mkoani Morogoro.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni