MAKAMU WA RAIS AZINDUA SIKU YA MWANAMKE WA MFANO TANZANIA

Makamu wa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM akizindua Siku ya Wanawake wa Mfano Tanzania iliyoandaliwa na Umoja wa wanawake wa Tanzania (UWT) katika ukumbi wa PTA, jijini Dar es Salaam 
Mama Fatma Karume akionyesha juu tuzo ya Mwanamke wa Mfano Tanzania ikiwa sehemu ya kutambua mchango wake katika harakati za Mapinduzi ambapo yeye alikuwa mke wa Rais wa kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Abeid Aman Karume 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi tuzo ya Mwanamke wa Mfano mke wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mama Salma Kikwete. 
Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Mhe. Anna Makinda akionyesha juu Tuzo yake ya Mwanamke wa Mfano mara baada ya kukabidhiwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan. 
Mama Fatma Karume mke wa Rais wa kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar akitoa nasaha zake mara baada ya kupokea tuzo ya Mwanamke wa Mfano iliyoandaliwa na Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT). 

Picha na Ofisi ya Makamu 

……………….. 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Wanawake walikuwa na mchango mkubwa katika harakati za Uhuru wan chi hii. 

Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Siku ya Mwanamke wa Mfano Tanzania iliyoandaliwa na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) 

Makamu wa Rais alisema Ni dhahiri kuwa wanawake walikuwa na mchango mkubwa sana. Walifanya kazi kubwa katika uhamasishaji, malezi ya watoto na vijana na kusimama bega kwa bega na kuunga mkono wanaume waliokuwa mstari wa mbele katika mapambano. Walifanya mengi nyuma ya pazia ambayo yalikuwa na mchango mkubwa katika Taifa letu. Mapenzi yao, subira yao na mchango wao wa hali na mali ndio uliowapa nafasi wanaume kufanikisha harakati za uhuru kwa kuwa wanawake waliwapa wepesi kwa kuwapunguzia mzigo mzito uliokuwa mabegani mwao. Haiyumkini, katika ngao yetu ya Taifa, ikatambua nafasi ya mwanamke kwa kuwekwa sambamba na mwanaume. 
Makamu wa Rais aliendelea kusema kutokana na kazi kubwa ya wanawake jasiri na mashujaa waliotutangulia, wanawake wa nchi yetu wameendelea kutoa mchango mkubwa katika Uongozi katika nchi yetu na nje ya mipaka yake. 

Makamu wa Rais alitoa wito kwa Wanawake na kusema Tuzo za “Mwanamke wa Mfano Tanzania” ziwe chachu yetu Wanawake katika kuchapa kazi, kuungana, kushikamana katika kuleta maendeleo miongoni mwetu na jamii nzima ya Watanzania. Sisi wanawake ni nusu ya watu wote nchini. Sisi tukijiongeza tukaendelea, kaya zetu zinaendelea na hatimaye nchi inaendelea. 

Makamu wa Rais aliwataka Umoja wa wanawake Tanzania (UWT) kuchukua jukumu lenu la kuwasemea, kuwatetea na kuwaunganisha wanawake wote wa Tanzania wana CCM, wasio wana CCM na wasio na vyama. Ndio wajibu wa UWT mliopewa na Katiba ya CCM. Katika nchi yetu, hamna chombo chochote kikubwa cha kuwaunganisha wanawake isipokuwa ninyi. Nawakumbusha kuwa nanyi mnatazamwa na wanawake wa nchi yetu. 

Jumla ya Tuzo 26 za Mwanamke wa Mfano zilitolewa .

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni