Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
Rais
wa Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB, Dkt. Akinumwi Adesina, amemaliza
ziara yake ya siku tatu nchini na kuahidi kuwa atahakikisha Tanzania
inaendelea kunufaika na misaada na mikopo yenye masharti nafuu kutoka
Benki hiyo kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kisasa katika Jiji la
Dodoma na mradi wa kuzalisha umeme wa Stieglers Gorge.
Akiwa
katika uwanja wa ndege Jijini Dodoma, Dkt. Adesina amemmwagia sifa Rais
Dkt. John Pombe Magufuli kwa namna anavyosimamia ukuaji wa uchumi
uliofikia wastani wa asilimia 7 kwa mwaka pamoja na kupambana na vitendo
vya ufisadi, rushwa, kuimarisha uwajibikaji wa viongozi kwa wananchi,
kupiga vita matumizi mabaya ya rasilimali za umma ili kuwaondoa wananchi
wake katika umasikini.
Dkt.
Adesina amesema kwa kutambua mchango huo pamoja na umahili wa Waziri wa
Fedfha na mipango Dkt. Philip Mpango, wa kusimamia uchumi na sera ya
bajeti na fedha, benki yake itaendelea kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha
ili nchi iweze kupiga hatua kubwa kupitia miundombinu mbalimbali
inayotekelezwa kupitia benki yake na washirika wengine wa maendeleo.
Miongoni
mwa miradi ambayo Benki hiyo imepanga kusaidia ni ujenzi wa Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa utakaojengwa katika eneo la Msalato, nje kidogo ya
Jiji la Dodoma ambapo kwa kuanzia benki hiyo itatoa zaidi ya shilingi
bilioni 200.
“Tumekuwa
na majadiliano ya kina na Mhe. Rais Dkt. John Magufuli kuhusu mradi wa
kuzalisha umeme wa Stieglers Gorge ambao utazalisha Kw 2100, Benki yetu
itaangalia namna ya kutoa fedha kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa mradi
huo mkubwa” alisema Dkt. Adesina.
Alisema
kuwa suala la mapinduzi ya viwanda haliwezi kufanikiwa bila kuwa na
nishati ya umeme ya uhakika na kwamba benki yake itawekeza dola za
Marekani bilioni 1.5 kwa ajili ya sekta ya nishati na itaongeza kiasi
kingine cha dola milioni 950 kwa ajili ya kazi hiyo.
“Mwaka
huu tutatoa fedha kwa ajili ya kuboresha nishati ya umeme katika ukanda
wa Kaskazini Magharibi mwa Tanzania na tuna mpango pia wa kuboresha
Shirika la Ugavi wa Umeme hapa nchini-TANESCO, ili liweze kuzalisha
umeme wa uhakika na wenye gharama nafuu kwa ajili ya kuendeleza mpango
wa Serikali wa kuwa na uchumi wa viwanda” aliongeza Dkt. Adesina
Kwa
upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ameelezea
kufurahishwa na ujio wa Rais huyo wa Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB,
Dkt. Akinumwi Adesina, na kwamba ujio huo umeleta neema kwa nchi baada
ya benki hiyo kuahidi kutoa shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kujenga
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato pamoja na kuahidi kutoa fedha
kwa ajili ya kujenga barabara za mchepuko (mzunguko) Jijini Dodoma.
Dkt.
Mpango amewataka watanzania kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali
za kuwaletea maendeleo na watembee kifua mbele kwa kuwa hivi sasa
Tanzania imeshika nafasi ya pili katika Bara la Afrika kwa ukuaji wa
uchumi kwa kasi ikitanguliwa na nchi ya Ethiopia, na Rais Adesina
amelisemea vizuri jambo hilo.
Ushirikiano
wa Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB na Tanzania ulianza tangu mwaka
1971, ambapo mpaka sasa benki hiyo imewekeza kiasi cha dola bilioni 3.6,
sawa na zaidi ya shilingi trilion 8, katika miradi mbalimbali ya
kiuchumi ikiwemo umeme, barabara, maji na usafi wa mazingira, uboreshaji
rasilimali watu pamoja na masuala ya utawala bora.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni