Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa RAHCO, Ndg Masanja Kadogosa leo amekutana na wafanyabiashara waliovamia maeneo mbali mbali ya reli mkoani Dodoma na kufanya mazungumzo nao. Wafanyabiashara hao wapatao 200 kutoka maeneo ya stendi ya mkoa, na stend ya daladala ya Jamatini, walikusanyika katika club ya reli (Dodoma railway club) kwa mazungumzo yaliyohusisha changamoto mbali mbali wanazokutana nazo wakiwa katika maeneo hayo ya reli.
Mkurugenzi aliwahakikishia kuwa nia ya serikali sio kuwanyanyasa wafayabiashara hao au kuwapa usumbufu bali RAHCO kama kampuni inataka kuwabahini na kuwafahamu watu walipo katika maeneo ya reli na sio kwa mkoa wa Dodoma tu bali zoezi hili ni la nchi nzima maeneo ambayo reli inapita.
Sheria ya reli ya mwaka 2002 inaweka wazi juu ya maeneo ya reli (hifadhi ya reli),kuwa kwa maeneo ya mjini kutoka katika njia ya reli upande wa kushoto na kulia ni mita 15 na kwa maeneo ya vijijini ni mita 30,sheria hiyo inaendelea kusema kuwa mtu yeyote atakae fanya shughuli zake katika maeneo hayo ya reli bila kibali au makubaliano na RAHCO anakuwa amevunja sheria hiyo, hivyo kampuni hodhi ya
rasilimali za reli inaweza kumchukulia hatua mbali mbali ikiwemo kuvunja majengo au miundombinu iliyopo katika hifadhi hiyo. Mkurugenzi amewataka wafanyabiashara hao kupitia kwa viongozi wao waliopo kuanza kujiandaa kwa kuingia mkataba na RAHCO wa kufanya biaashara katika maeneo ya reli tofauti na hivi sasa ambapo wengine wanakaa bila kulipa kodi sehemu yoyote na wapo wanaolipa kodi kwa manispaa ya Dodoma wakati maeneo hayo ni ya RAHCO.
Wengi wa wafanyabiashara hao wamekuwa wakilipa kodi kimakosa kwa manispaa ya Dodoma licha ya wafanyabiashara wengine kukosa leseni za biashara kutoka kwa manispaa hiyo kwa kuambiwa kuwa manispaa siyo wahusika wa eneo hilo.
“Karibu kila mtu hapa anafahamu kuwa maeneo mnayofanyia biashara ni ya reli lakini bado mnaendelea kulipa kodi Manispaa, siwaambii kuwa msilipe kodi ila zile zilizopo kisheria za manispaa lipeni manispaa na zile za eneo mnayofanyia biashara lipeni sehemu husika. Ujio wangu huu sio wa kuwafukuza au kuwavunjia kwa sababu nilishatuma timu yangu kuweka alama ya X kwa wale wote ambao wapo maeneo ya reli kivamizi, na kisheria natakiwa kuwavunjia maana mpo hapo bila makubaliano yoyote na sisi (RAHCO).
Hivyo basi kama sheria inavyosema nataka muendelee kuwepo hapo lakini kwa makubaliano na RAHCO, mtulipe kodi ya kukaa kwenye maeneo yetu lakini Kikubwa Zaidi muelewe kuwa kunamradi mkubwa wa Standard Gauge unakuja karibuni tukiwataka muondoke kupisha mradi huo muwe tayari kuondoka kwa ridhaa yenu wenyewe.” Alisema Kadogosa
Kadogosa aliendelea kwa kusema “Makao makuu kuhamia Dodoma inatufanya na sisi kuwaza kujenga reli kwa ajili yakuwa na treni za abiria za mjini (Commuter train) kama zile mbili zilizopo Dar es salaam, hivyo nilazima tuhakiki maeneo yetu na kujua nani anafanya nini katika maeneo hayo kwa sasa”.
Mkurugenzi aliwataka viongozi wa wafanyabiashara hao kutoka maeneo mbali mbali kuunda kamati itakayoongozwa na wafanyakazi kutoka RAHCO na TRL kwa ajili ya kufanya tathmini mbalimbali na kuwatambua wafanyabiashara wote ili waweze kuingia mkataba wa muda mfupi mfupi na RAHCO kipindi hiki ambapo hatua mbalimbali za maandalizi ya ujenzi wa standard gauge zinapoendelea.
Imetolewa na Ofisi ya Uhusiano, RAHCO.
21/12/2016
Kaimu Mkurugenzi wa RAHCO katikati, Bw.Masanja kadogosa akiongozana na baadhi ya viongozi wa wafanyabiashara katika maeneo ya reli wakielekea kukagua maeneo hayo ambapo wafanyabiahara hao wanafanya shuguli zao.
Mkurugenzi Kadogosa akiwasalimia wauza viatu waliopo katika eneo la reli nyuma ya stand ya daladala ya Jamatini wakati wa ukaguzi wa maeneo ambayo wafanyabiashara wengi wanalitumia.
Wafanyabiashara katika stendi ya Jamatini mkoani Dodoma, wakiendelea na shughuli zao wakati Mkurugenzi wa RAHCO Bwana Kadogosa akifanya ukaguzi katika maeneo ya reli yaliyopo hapa stand ya daladala ya Jamatini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni