WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza
Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Bw. Rashid Taka na Mkurugenzi wa
Halmashauri hiyo Bw. Raphael Siumbo kufanya uchunguzi na kuwachukulia
hatua watendaji wote watakaobainika kuhusika katika uuzwaji wa
kiwanja cha shule ya msingi Waso.
Ametoa agizo hilo jana jioni (Alhamisi,
Desemba 15, 2016) wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa
hadhara uliofanyika kwenye kata ya Waso Wilaya ya Ngorongoro akiwa
katika ziara ya kikazi mkoani Arusha.
Waziri Mkuu alisema Serikali haiwezi
kuvumilia kuona watendaji wachache wasiokuwa waadilifu wanamega
kiwanja cha shule na kukiuza kwa maslahi yao, hivyo aliwataka
viongozi hao kufuatilia na kumpa taarifa ya hatua za kisheria
walizochukua kwa wahusika.
“Mkuu wa wilaya na Mkurugenzi hapa
kuna malalamiko ya viwanja fuatilieni viwanja hivyo vinavyolalamikiwa
na wananchi ni viwanja gani je hiyo ya kwamba mmeuza viwanja vya
shule ameuziwa nani,” alisema.
Aidha, Waziri Mkuu amemtaka Bw. Taka
ahakikishe Mkuu wa Idara ya Ardhi, Maliasili na Mzingira, Bw.
Switbeth Byorushengo anatekeleza majukumu yake ipasavyo. Ametoa agizo
hilo baada ya wananchi kudai Ofisa huyo ameshindwa kufanya kazi na
kumuomba Waziri Mkuu aondoke naye.
Alisema Bw. Byorushengo anatakiwa
kuhakikisha halmashauri hiyo inapima viwanja vya kutosha na kutoa
hati kwa wananchi ili waweze kupata maeneo ya kujenga makazi na
shughuli zingine za kijamii.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
alimuagiza Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Bw. Byorushengo kuhakikisha
halmashauri hiyo inaanza ujenzi wa hospitali ya wilaya na ifikapo
Aprili, 2017 awe amepewa taarifa za ulipofikia ujenzi huo.
Kwa upande wake Mkurugenzi huyo alisema
tayari wapo katika mchakato wa ujenzi wa hospitali ya wilaya ambapo
wametenga sh. milioni 800 za kuanzia.
Akizungumzia kuhusu mgogoro wa ardhi
kati ya vijiji vya Tarafa ya Loliondo na Hifadhi ya Taifa ya
Serengeti, Waziri Mkuu alitoa muda wa siku 30 kwa uongozi wa Shirika
la Hifadhi za Taifa Nchini (TANAPA) wawe wamekamilisha uhakiki wa
mpaka huo.
Naye Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na
Uvuvi ambaye ni Mbunge wa Ngorongoro Mheshimiwa William Ole Nasha
alimuomba Waziri Mkuu kuwasaidia kutatua mgogoro huo wa ardhi kwa
kuwa ni wa muda mrefu na unakwamisha shughuli za maendeleo.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw.
Mrisho Gambo alisema Wilaya ya Ngorongoro inachangamoto nyingi
ikiwemo ya ardhi na sasa kuna mgogoro kati ya Kampuni ya Thomson
Safari na wananchi ambao wanadai kuwa ardhi hiyo ilichukuliwa
kinyemela na mwekezaji huyo bila ya wao kushirikishwa.
Alisema baada ya ziara ya Waziri Mkuu
kumalizika mkoani hapa atarudi wilayani Ngorongoro kwa ajili ya
kutatua kero mbalimbali ikiwemo ya ardhi na matumizi mabaya ya fedha
zinazotolewa na wawekezaji ambazo matumizi yake hayajulikani.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, DESEMBA 16, 2016.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni