Wasichana yenye umri mdogo wametakiwa kuacha tabia ya kujihusisha
na vitendo vya ngono katika umri mdogo kwani wanajiweka kwenye hatari
kubwa ya kupata maambukizi ya magonjwa hatari ikiwemo Saratani ya mlango
wa kizazi pampja na gonjwa hatari la UKIMWI.
Rai hiyo imetolewa na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, na mkuu wa
wilaya ya Monduli Mhe. Idd Kimanta wakati wa uzinduzi wa chanjo mpya ya
Saratani ya Mlango wa Kizazi katika halmashauri ya Arusha, uliofanyika
kwenye hospitali ya wilaya ya Olturumet.
Mkuu wa wilaya huyo amewaasa wasichana kuacha tabia ya kujihusisha na
vitendo vya ngono, licha ya kupata kinga ya Saratani ya Mlango wa
Kizazi na kuongeza kuwa chanjo hiyo haizuii kupata maambukizi ya
magonjwa mengine yanayoombukizwa kwa njia ya kujamiiana.
Amefafanua kuwa, vitendo vya ngono katika umri mdogo vinachangia sana
kukatisha ndoto za wasichana wengi na wakati mwingine husababisha
wasichana wengine kupoteza maisha.
Hata hivyo Kimanta amewataka wazazi, walezi na jamii nzima
kuhakikisha wasichana wenye umri wa miaka 14, wanakwenda kupata chanjo
hiyo huku akiwataka viongozi wa kata zote kusimamia zoezi hili kwa
ufasaha na kuhakikisha hakuna mtoto atakayekosa chanjo hiyo pamoja na
kuwaonya watu watakaokwamisha zoezi hilo kuchukuliwa hatua kali za
kisheria.
Naya mratibu wa chanjo halmashauri ya Arusha Dkt. Yassin Winga ,
amesema kuwa halmashauri inategemea kuwapatia chanjo jumla ya wasichana
4,239 itakayotolewa kwenye vituo 50 vilivyopo kwenye vituo vya kutolea
huduma za afya ndani ya halmashauri na zoezi litafanyika ndani ya wiki
nzima.
Dkt. Winga amefafanua kuwa, zoezi la chanjo litatolewa pia kwa
kutumia 'Mobile Clinic' kwa wakazi wa maeneo ya pembezoni na kusema kuwa
chanjo hii itatolewa mara mbili na mara tatu kwa wasichana wenye
maambukizi ya VVU ndani ya miezi sita.
Aidha baadhi ya wanafunzi waliofika kituoni hapo na kupatiwa chanjo
hiyo, wamekiri kuridhishwa na chanjo hiyo na kusema kuwa wanaamini
chanjo hiyo itawakinga na ugonjwa wa Saratani ya Mlango wa Kizazi na
kukiri kutokujihusisha na vitendo vya ngono katika umri mdogo.
Asnath Melau msichana aliyepatiwa chanjo amesema kuwa, chanjo
waliyoipata ni muhimu kwa maisha ya msichana hasa ukizingatia wanawake
wengi hupoteza maisha kutokana na ugonjwa wa kansa ya mlango wa kizazi.
"Hii chanjo ni nzuri na ni muhimu kwetu wasichana, kwa kuwa wakina
mama wengi wanakufa na kansa ya mlango wa kizazi, tunashukuru serikali
kwa kutupatia kinga na inatupa amani ya kutokupata maambukizi" amesema
Asnath.
Hafla hiyo imeambatana na igizo lililohamasisha jamii kuhakikisha
wasichana wa miaka 14 wanapata chanjo ya Saratani ya Mlango wa Kizazi
pamoja na upimaji wa afya, lililotolewa na kikundi cha sanaa cha vijana
cha ACE AFRICA.
Hata hivyo Mkuu wa Wilaya Kimanta amelishukuru shirika lisilo la
kiserikali la ACE AFRICA kwa kujitoa kwa halina mali kushiriki shughuli
mbalimbali za kijamii ndani ya halmashauri ya Arusha