Na Felix Mwagara/MOHA
NAIBU
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amelitaka
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuanzisha kituo cha zimamoto Wilaya ya
Ruangwa mkoani Lindi.
Masauni
alisema Aprili Mosi mwaka huu Jeshi hilo litakuwa na ofisi wilayani
humo ili askari wa Jeshi hilo waanze kutoa huduma sehemu mbalimbali ya
Wilaya hiyo ambayo ni muhimu kituo hicho kuwepo kutokana na uwepo na
machimbo ya madini ya dhahabu pamoja na mji kuendelea kukua kwa kasi.
“Tumekubaliana
vizuri baada ya Kamanda wa Zimamoto mkoa kuwa ifikapo tarehe moja
askari wa zimamoto watakuwepo hapa Ruangwa rasmi kwa ajili ya kuanza
kazi, na watapewa ofisi na halmashauri ya Wilaya, hivyo utaratibu wa
kupata vifaa vya awali uanze mara moja kama tulivyokubaliana,” alisema
Masauni.
Kwa
upande wake Kamanda wa Jeshi hilo Mkoa wa Lindi, Christina Sunga
alimuhakikishia Naibu Waziri pamoja na Watendaji wa Wilaya hiyo, agizo
hilo atalifanyia kazi haraka iwezekanavyo na mpaka ifikapo Aprili mosi
mwaka huu tayari askari wawili watakuwa wameripoti mjini Ruangwa.
“Uwepo
wa askari hawa kutarahisisha kwa kiasi kikubwa kutoa elimu kwa umma
jinsi ya kuzima moto pamoja na kupambana na uzimaji moto, licha ya kuwa
tunakuwa na vifaa vya awali vya uzimaji moto mpaka hapo tutakapopata
gari kwa ajili ya shughuli mbalimbali za uzimaji moto na utoaji elimu
zaidi,” alisema Sunga na kuongeza;
“Tunashukuru
Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa kwa kutupa ofisi kwa ajili ya askari
wa zimamoto lakini pia kutuwezesha kupata vifaa hivyo vya awali vya
uzimaji wa moto.”
Aidha,
Masauni alimuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, (RPC) Renatha
Mzinga kuandaa mchoro pamoja na gharama ya ujenzi wa kituo kikubwa cha
polisi cha Wilaya ya Ruangwa ili ujenzi huo uanze.
“Nimekagua
eneo la ujenzi wa kituo kipya cha polisi, eneo zuri na linafaa kwa
ujenzi wa kituo kikubwa cha polisi, maandalizi tayari yameanza na hivi
karibuni RPC atakamilisha mchoro pamoja na gharama ya ujenzi wa kituo
hicho hapa Ruangwa,” alisema Masauni.
Pia
Masauni amesema Wizara yake itahakikisha inawajengea ofisi Uhamiaji,
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) pamoja na Jeshi la Zimamoto na
Uokoaji wilayani humo ambapo kwasasa ofisi hizo zipo katika jengo la
Halmashauri ya Wilaya hiyo.
Naibu
WaziriMasauni amemaliza ziara yake ya siku mbili kwa kutembelea miradi
mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuzungumza na askari na maafisa wa
vyombo walio chini ya wizara yake mkoani Lindi na tayari amesafiri
mkoani Mtwara kuendelea na ziara yake.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni