WASHIRIKI TUZO ZA HABARI TANAPA ZAONGEZEKA

Tanapalogojohnson

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
WASHIRIKI WALIOWASILISHA KAZI ZAO TUZO ZA WAANDISHI WA
HABARI ZA TANAPA WAONGEZEKA

1. ZOEZI LAKAMILIKA

Zoezi la kuchambua na kuchuja kazi zitakazoshindanishwa mwaka huu katika Tuzo ya TANAPA MEDIA AWARDS limekamilika. Kati ya kazi 114 zilizotumwa kutoka vyombo mbalimbali vya habari, vikiwamo Magazeti, Radio na Runinga, ni kazi 82 tu zilizokidhi vigezo muhimu vya kiufundi vya kushiriki shindano. Jumla ya kazi zilizotumwa mwaka huu ni 114 na wakati mwaka jana kulikuwa na jumla ya kazi 34 tu.

Hili ni ongezeko la asilimia 235. Kati ya kazi 79 za magazeti zilizotumwa TANAPA, ni kazi 63 tu zilizokidhi vigezo muhimu vya kiufundi vya kushiriki shindano. Aidha, kati ya kazi 16 za Redio zilizotumwa ni kazi 7 tu zilizokidhi vigezo vya kiufundi vya kushiriki shindano. Na katika kazi za Runinga 19 zilizotumwa ni kazi 12 tu zilizokidhi vigezo vya kiufundi vya
kushiriki.

2. ONGEZEKO LA USHIRIKI
Mwaka jana jumla ya washiriki waliotuma kazi zao katika shindano walikuwa ni 24 tu. Mwaka huu jumla ya washiriki waliotuma kazi zao ni 67. Hii ina maana ushiriki umeongezeka kwa asilimia 179. Hii inatia moyo sana kwamba waandishi wengi wamehamasika kuandika na kushiriki katika shindano hili muhimu.


3. USHIRIKI KIJINSIA
Mwaka jana, washiriki 5 kati ya 24 waliotuma kazi zao walikuwa ni wanawake ambao ni sawa na asilimia takriban 21 ya washiriki wote. Mwaka huu washiriki wanawake walikuwa 12 sawa na asilimia takriban 18 ya washiriki wote. Napenda kutoa wito kwa waandishi wanawake kuongeza ushiriki wao katika shindano hili kwani wapo wengi wanaoandika kuhusu masuala ya Uhifadhi na Utalii lakini hawashiriki.

4. UHIFADHI NA UTALII WA NDANI
Kwa ujumla kati ya kazi 114 zilizotumwa, kazi zilizohusu Uhifadhi ni 64 (sawa na 56%), wakati kazi zilizohusu Utalii wa Ndani ni 50 (sawa na 44%). 5. 

KUKIDHI VIGEZO VYA USHINDANI
Asilimia takriban 24 ya kazi zote zilizotumwa mwaka jana hazikukidhi viwango muhimu vya ushiriki. Katika shindano la mwaka huu asilimia ya kazi ambazo hazikukidhi viwango vya ushiriki ni 28. Kwa asilimia hizi ni dhahiri tatizo la kutozingatia vigezo linaongezeka. Hivyo basi, ipo haja ya washiriki kuhakikisha wanakuwa makini katika kuzingatia masharti na kanuni za ushiriki.

6. SABABU ZA KUTOKIDHI VIWANGO
Kazi zote zilizotupwa kapuni ni zile ambazo hazikukidhi viwango vya kiufundi vya ushiriki ambavyo viliainishwa wazi katika tangazo hilo.

Mifano ya kazi zilizoenguliwa:
• Mshiriki anatuma kazi ya Redio au Runinga lakini katika fomu ya kushiriki hakuna mhuri rasmi wa chombo husika wala sahihi ya Mhariri, Msimamizi wa Kipindi au Mkuu wa Uzalishaji. Na kuna washiriki hawakujaza hata fomu.
• Mshiriki anatuma kazi ambayo mada yake inahusu masuala ya uhifadhi au utalii wa ndani katika maeneo yaliyo nje ya Hifadhi za TANAPA.
• Mshiriki anatuma kazi katika mfumo ambao haukutajwa katika tangazo (kwa mfano;
wapo waliotuma Kanda (kaseti) badala ya kutumia mifumo iliyoainishwa katika fomu ya ushiriki au katika tangazo.
• Mshiriki anatuma kazi iliyochapishwa katika Jarida ama katika tovuti peke yake na si katika Gazeti, Redio au Runinga. Kazi zinazoshindanishwa katika Tuzo hii ni zile zinazotolewa kwanza katika Magazeti, Radio na Runinga, vyombo vinavyowafikia watu wengi zaidi. 

7. HATUA INAYOFUATA
Hatua inayofuata ni ya majaji kupitia kazi zilizokidhi vigezo vya kiufundi kwa ajili ya kupata washindi katika makundi husika na kutoka vyombo vyote vya habari yaani Magazeti, Redio na Runinga. Baada ya kupatikana washindi, TANAPA itatangaza tarehe na mahali zitakapofanyika hafla ya utoaji tuzo.

8. TUZO KWA WASHINDI
Tuzo mbalimbali hutolewa kwa washindi wa Tuzo za Habari za TANAPA ambapo washindi hupewa tuzo kama ifuatavyo:

i. Washindi wa Kwanza: 2,000,000/-, Ngao, Cheti na Safari ya Mafunzo katika
mojawapo ya nchi za SADC

ii. Washindi wa Pili: 1,500,000/-, Cheti na Ziara ya Mafunzo katika Hifadhi za Taifa
iii. Washindi wa Tatu: 1,000,000/- na Cheti. 

Imetolewa na Idara ya Mawasiliano
HIFADHI ZA TAIFA TANZANIA

02.03.2014

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni