Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb)(kushoto) akiongoza Mkutano wa Wakurugenzi Watendaji wanaoziwakilisha nchi zao katika Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), katika kufanya tathmini ya maendeleo ya Miradi inayofadhiliwa na Benki hiyo, ambapo Wakurugenzi hao waliipongeza Tanzania kwa kutekeleza miradi kwa ufanisi. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji kutoka Afrika ya Kusini Bi. Mmakgoshi Lekhethe aliyeongoza ujumbe wa Wakurugenzi Watendaji wengine 12 (hawapo pichani), katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji kutoka Afrika ya Kusini Bi. Mmakgoshi Lekhethe (kulia) wakipeana mikono baada ya kumalizika kwa mkutano wa tathmini ya maendeleo ya Miradi inayofadhiliwa na Benki hiyo nchini Tanzania, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (wanne kulia) na Mkurugenzi Mtendaji kutoka Afrika ya Kusini Bi. Mmakgoshi Lekhethe (wa tano kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na Wakurugenzi Watendaji wanao ziwakilisha nchi zao katika Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), baada ya kumalizika kwa mkutano wa tathmini ya maendeleo ya Miradi inayofadhiliwa na Benki hiyo nchini Tanzania, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam.
Mmoja wa Wakalimani aliyeambatana na Wakurugenzi Watendaji wanao ziwakilisha nchi zao katika Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), akisalimiana kwa bashasha na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), (kulia) baada ya kumalizika kwa mkutano wa tathmini ya utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na Benki hiyo nchini Tanzania, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es salaam, ikiwa ni ishara njema kwa Taifa kwa kuwa walipongeza jitihada zinazofanywa na Serikali za kupambana na umaskini.
Na Benny Mwaipaja, WFM
Naibu Waziri Wizara ya Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) amesema Serikali inaendelea kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) katika kuhakikisha miradi yote ikiwemo ile inayofadhiliwa na Benki hiyo inatekelezeka kwa ufanisi Mkubwa.
Dkt. Kijaji ameyasema hayo alipokutana na Wakurugenzi Watendaji 12 wanaoziwakilisha nchi zao katika Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), katika Mkutano uliofanyika Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dar es salaam, baada ya ujumbe huo kutembelea miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Benki hiyo hapa nchini.
“Madhumuni makubwa ya ziara ya Wakurugenzi watendaji wa Benki ya AfDB waliokuja nchini tangu Februari 25, ni kukaa pamoja na Serikali ili kujadiliana kuhusu sera na mipango mikakati ya maendeleo, lakini pia kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa kupitia ufadhili wa Benki ya hiyo” Alifafanua Dkt. Kijaji.
Wakurugenzi hao ambao ndio watoa maamuzi katika Benki hiyo, wametembelea miradi ya maji Zanzibar na kwa upande wa Tanzania Bara wametembelea mradi wa kufua umeme wa Sokoine substation uliopo Manispaa ya Ilala.
Katika Mkutano huo, Serikali ya Tanzania imeendelea kuiomba Benki ya AfDB kuharakisha kazi za upembuzi yakinifu na hatimaye kutoa fedha ili utekelezaji wa miradi ya Maendeleo uanze mapema kwa kadri inavyowezekana.
Miradi hiyo ni pamoja na ule wa North – West grid wa kusafirisha Nishati ya Umeme kutoka Shinyanga hadi Mbeya kupitia Kigoma Katavi na Rukwa. Mradi utakaowezesha Mikoa ya Ukanda wa Magharibi kupata Nishati ya uhakika ya umeme na kufungua fursa za Maendeleo mbalimbali yakiwemo ya ujenzi wa Viwanda vidogo na vya kati.
Kwa kushirikiana na Benki hiyo ya AfDB mradi mwingine unaofanyiwa kazi ili kupata fedha za kuanza kuutekeleza ni ule wa kujenga barabara ya Nyakanazi, kupitia Kibondo, Kasulu hadi Manyovu, kwa kiwango cha lami na iwapo mradi huo ukipatiwa fedha na kukamilika kwa wakati kutasaidia kuchochea biashara ya wakazi wa maeneo hayo pamoja na Nchi ya Burundi.
Kwa upande wa Wakurugenzi Watendaji wa AfDB wanaoziwakilisha nchi zao, wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji kutoka Afrika ya Kusini Bi. Mmakgoshi Lekhethe, wameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Pombe Joseph Magufuli kwa ufanisi katika Nyanja zote ikiwemo ya kupambana na umaskini.
Wageni hao wamefurahishwa na namna Tanzania invyotekeleza miradi inayofadhiliwa na Benki hiyo, kwa kuwa kila walipopatembelea, wameona uthabiti na umadhubuti wa miradi, jambo ambalo limewaongezea hamasa ya kufanya kazi kwa karibu na nchi hiyo.
Wameitaka Serikali kuendelea kulishughurikia suala la deni la Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania-TANESCO, ili kuongeza ufanisi wa kiutendaji kwa lengo la kuchochea maendeleo ya nchi mijini na Vijijini.
Naibu Waziri Dkt. Kijaji amebainisha kuwa ipo mikakati iliyowekwa na Serikali ya kutatua suala la deni hilo kwa kuwa tatizo kubwa lilikuwa matumizi ya Mafuta ya dizeli katika kuendeshea mitambo TANESCO.
Aidha alisema kuwa kwa sasa upatikanaji wa Nishati ya Gesi katika maeneo mbalimbali ya Tanzania, utasaidia katika kuendesha mitambo hiyo badala ya Mafuta hivyo kutatua suala la deni hilo linalo likabili Shirika na hatimaye kutimiza ndoto ya watanzania ya kuimarika kwa uchumi utakao chochewa na Sekta hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni