BAADA YA KAMPUNI YA AGRO TEK KUSHINDWA, SMZ SASA KUINGILIA KATI MATUMIZI YA MASHAMBA YA MIPIRA YALIYOPO UNGUJA NA PEMBA


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa sasa imejipa kazi kuendelea
kutafakari hatma muwafaka ya matumizi sahihi ya Mashamba ya Mipira
yaliyopo katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba.


Alisema uwamuzi utakaotolewa hapo baadaye utazingatia zaidi kutoa
fursa kwa wafanyakazi waliokuwa wakihudumia Mashamba hayo baada ya
Kampuni iliyopewa jukumu na Serikali la kuyasimamia ya Agro Tek
kushindwa kuendeleza mradi huo na hatimae kuingia mitini.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo baada ya kulitembelea shamba la
Mipira la Maziwani Wete wakati akizungumza na Wafanyakazi wa Mashamba
ya Mipira ya Kisiwani Pemba walioamua kuanzisha Umoja uliopewa jina la
Tuwezeshe kwa lengo la kuyaendeleza Mashamba ya Mipira Kisiwani
Pemba.

Alisema mradi wa uoteshaji wa miti ya Mipira Zanzibar ulioanzishwa na
Serikali kwa nia safi ya kutoa ajira kwa Vijana Wazalendo sambamba na
kuongeza mapato ya Taifa umepata majaribu makubwa na kukosa kutimiza
ndoto iliyokusudiwa.

Balozi Seif ameelezea faraja yake kutokana na kazi kubwa inayoendelea
kufanywa na Umoja huo wa Tuwezeshe Maziwani Wete Pemba ya kuyahudumia kiuzalishaji Mashamba hayo mpango ambao utayawezesha Mashamba ya Mipira Kisiwani humo kuendelea kuwa katika mazingira salama.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba kuutumia ujuzi
walioupata wafanyakazi hao wa Tuwezeshe chini ya Makampuni yaliyopita
ni jambo jema na la msingi linaloleta matumaini ya upatikanaji wa
ajira na kipato.

Aliwataka wafanyakazi hao kuendelea kulipa kodi Serikalini kutokana na
uzalishaji wa mradi wao kitendo ambacho kitaamsha ari na muelekeo
mwema kwa Serikali katika maamuzi yake kutokana na mradi huo.

Katika kuunga mkono jitihada za Wananchi hao wa maeneo ya Maziwani
Wete Pemba Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliahidi kusaidia nguvu
za uwezekaji wa Jengo lao la Kituo cha Afya walilojenga kwa njia ya
kujitegemea.

Akisoma Risala Katibu wa Umoja huo wa Tuwezesha Maziwani unaojihusisha
na uzalishaji wa zao la Mipira Ndugu Mohammed Jadi Suleiman alisema
wana Umoja huo hivi sasa wanafuraha na matarajio makubwa ya maisha yao
tokea kupewa ruhusa ya kuendelesha mradi huo wa Mipira.

Nd. Suleiman alisema upatikanaji wa mishahara kwa wakati umekuja
kutokana na kasi nzuri ya uzalishaji wa utomvu iliyopo hivi sasa jambo
ambalo pia limeleta imani kubwa kwa wafanyabiashara waliokuwa wakiidai
Kampuni iliyokuwa ikiendesha mradi huo.

Alisema Umoja huo ukiendelea kulipa kodi zake kama kawaida kwa Bodi ya
Mapato Zanzibar { ZRB } na Mamlaka ya Mapato Tanzania { TRA }
wafanyakazi hao wamedhamiria kuanzisha vitalu vipya vya miti ya Mipita
wakilenga kuliendeleza zao hilo.

Katibu huyo wa Umoja wa Tuwezeshe aliitahadharisha Serikali Kuu haja
ya kuondokana na Makampuni yenye kuonyesha dalili za kukosa uaminifu
jambo ambalo baadaye huiletea hasara kubwa Serikali kwa kuacha madeni
na sifa mbaya.

Nd. Suleiman alisema ipo mifano hai iliyoonyeshwa na baadhi ya
Makampuni hayo mababaifu yaliyoacha deni la zaidi ya shilingi Milioni
184,254,750/- walizokuwa wakidai wafanyakazi 412 wa mashamba ya
Mipira Pemba pamoja na asilimia 5% waliyokatwa ya ZSSF lakini haikufikishwa kwa Taasisi husika.

Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alipata fursa ya
kukagua usindikaji wa Mpira katika hatua ya awali ya utomvu katika
kituo cha Mashamba ya Mipira kilichopo Mwani Mperani na baadae kukagua
shamba la Mipira liliopo katika Kijiji cha Maziwani Wete.

Afisa Ugani wa Shamba la Mipira Maziwani Bwana Suleiman Hamad
alimueleza Balozi Seif kwamba Wafanyakazi wa Umoja huo hivi sasa
wameamua pia kuanzisha kilimo cha Viungo kwa lengo la kujiongezea
kipato zaidi.
Bwana Suleiman alisema hatua ya awali wameanza na uoteshaji wa zao la
Vanila kwa Ekari Tano litakaloendelea hadi ekari 20 ndani ya mashamba
ya Mipira ili kulinda uchafuzi wa mazingira ndani ya eneo hilo ikiwani
ni pamoja na kudhibiti ukatwaji ovyo wa miti ya Mipira.

Kazi hiyo itakwenda sambamba na uoteshaji wa mazao mengine ya viungo
kama Pili Pili manga pamoja na hiliki mazao yenye uhakika wa soko
Kimataifa akitolea mfano zao la Vanila kwa sasa lililofikia thamani ya
shilingi Milioni 200,000,000/- kwa Tani Moja.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa ili wa Rais wa Zanzibar
27/11/2016..
You might also lik

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni