Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu
Hassan akiangalia nguo zinazotengenezwa na Kiwanda cha A to Z. Kulia
kwake ni Mkurugenzi wa kiwanda hicho Bw. Kalpesh Shah, na kushoto kwake
ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo. Makamu wa Rais amefanya
ziara kwenye kiwanda hicho ikiwa sehemu ya kutambua mchango wa
wawekezaji wa ndani na changamoto wanazokutana nazo ili kupata majibu ya
kurahisisha kufanikisha Tanzania mpya ya Viwanda.
**************************************
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan
amesema serikali itaendelea kuviimarisha vyuo vya ufundi stadi nchini
–VETA- ili viweze kutoa wahitimu bora ambao watakidhi katika soko la
ajira hasa kwenye viwanda vilivyopo na vitajengwa nchini.
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo leo wakati
anazungumza na uongozi wa kiwanda cha A to Z kilichopo mkoani Arusha
katika ziara yake ambayo imeingia siku ya Pili ya kutembelea viwanda
mbalimbali mkoani humo ili kujua changamoto zinazokabili viwanda hivyo
na serikali kuzitafutia ufumbuzi.
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema serikali imetenga fedha za
kutosha zitakazotumika kuviimarisha vyuo vya Veta ili viweze kutoa
mafunzo bora yatakayosidia vijana kufanya kazi zao kwa ufanisi wa hali
ya juu pindi watakapoajiriwa au kujiajiri wenyewe.
Kuhusu maslahi kwa wafanyakazi wa Kiwanda cha A to Z,Makamu wa Rais
Samia Suluhu Hassan ameutaka uongozi wa kiwanda hicho kulinda na kutetea
haki za wafanyakazi kwa kutoa maslahi mazuri ambayo yatawezesha
wafanyakazi hao kufanya kazi kwa bidii.
Makamu wa Rais pia amesisitiza usawa katika ulipaji wa mishahara kwa
wafanyakazi wa ndani na wa nje ya nchi walioajiriwa kwenye kiwanda hicho
ili kuondoa tofauti za mishahara hali ambayo ijenga motisha kwa
wafanyakazi.Kiwanda cha A to Z kilichopo eneo la Kisongo mkoani Arusha
ambacho kinatengeneza vyandarua, nguo na mifuko mbalimbali ikiwemo ya
saruji kimeajiri zaidi ya wafanyakazi 7500 ambapo asilimia 80 ya
wafanyakazi wote ni wanawake.
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amewahimiza wawekezaji kote nchi
walipe kodi za serikali mapema kodi ambazo zitatumika kuimarisha utoaji
wa huduma bora kwa wananchi.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu
Hassan akitembezwa Mkurugenzi wa kiwanda hicho Bw. Kalpesh Shahkatika,
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu
Hassan akiwa na Mkurugenzi wa kiwanda hicho Bw. Kalpesh Shah akipata
maelezo ya namna kiwanda cha A to Z kinavyofanya utafiti wa kupambana na
wadudu wanaoharibu mahindi kutoka kwa Mkurugenzi wa kituo cha utafiti
cha Africa Technical Research Centre Dkt.Johson Ouma Odera. Kulia ni
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni