TATIZO LA UMEME DAR KUTATULIWA.


Na Beatrice Lyimo-MAELEZO.

SERIKALI imedhamiria kuimarisha mtandao wa usafirishaji na usambazaji umeme nchini ili kufikia malengo ya taifa ya asilimia 75 ya watanzania wanaonufaika na huduma ya umeme ifikapo 2025.

Katika kutimiza azma hiyo, hivi karibuni Serikali kupitia Shirika la ugavi la umeme Tanzania (TANESCO) imezindua mradi wa uboreshaji wa huduma za umeme jijini Dar es salaamu uliobuniwa kwa lengo la kuboresha Miundombunu ya Usafirishaji na usambazaji umeme katika jiji la Dar es salaam.

Mradi huo umetokana na ongezeko la wahitaji wa huduma ya umeme katika Jiji la Dar es Salaam ambapo mradi huo utasaidia katika kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na hivyo ku0vutia wawekezaji wapya katyika sekta za viwanda.

Akizindua Mradi huo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema kuwa Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imekuwa katika jitihada mbalimbali za kuboresha miundombinu yake ili iweze kuwafikia wananchi wengi na katika ubora unaohitajika.

“Mradi huu wa kuboresha miundombinu ya umeme unalenga kuimarisha upatikanaji wa huduma ya umeme wa uhakika katika jiji la Dar es Salaam” anasema Majaliwa.Anasema mradi huo utafungua fursa nyingi za uzalishaji na kupelekea upatikanaji wa fursa za ajira za uhakika kwa wananchi.

Aidha, Waziri Mkuu anasema kuwa upatikanaji wa Umeme wa uhakika utaiwezesha nchi kufikia uchumi wa kati kupitia viwanda ikiwa ni lengo la Serikali ya Awamu ya Tano.Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Mhandisi. Felchesmi Mramba alisema kuwa Mradi huo umetumia jumla ya Shilingi bilioni 74.6, ikiwa ni fedha kutoka Serikali ya Finland kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania.

“mradi huu unafadhiliwa na Serikali ya Finland ambapo wametoka kiasi cha Tsh. Bilioni 63.56 sawa na asilimia 94.3 pamoja na Serikali imetoa kiasi cha Tsh. Bilioni 11.03 ikiwa ni asilimia 5.7.Mhandisi Mramba anaongeza kuwa mradi huo utasaidia kuvutia wawekezaji wapya katika sekta za viwanda na biashara nchini ili kuchochea ukuaji wa Sekta ya Viwanda vilivyopo kutokana na uwepo wa nishati hiyo inayokidhi mahitaji ya jamii.

Katika hatua hiyo, Mhandisi Mramba alibainisha baadhi ya miradi iliyohusisha Mradi huo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kituo kipya cha kupoza umeme cha kV 132/33/2x50MVA cha City Center, ujenzi wa kituo cha udhibiti mifumo ya usambazaji umeme katika msongo wa kV 33 na kV 11.

Akifafanua zaidi anasema miradi mingine ni pamoja na ujenzi wa njia ya umeme chini ya ardhi kwa ajili ya kuunganisha vituo vya Kariakoo, Railway na Sokoine mpaka kituo cha zamani cha city center.

Sambamba na hilo anasema kuwa, miradi mingine ya uboreshaji umeme inayoendelea jijini Dar es salaam ni mradi wa TEDAP unauhusisha uboreshaji wa miundombinu ya usafirishaji na usambazaji umeme katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo na Mikoani, ikiwemo maeneo ya Gongolamboto, Kipawa, Kurasini, Chang’ombe, Mbagala, Ubungo, Mburahati, eneo la uwanja wa ndege KIA, pamoja na Mikoa ya Kilimanjaro na Arusha.

Aidha alisema kuwa mradi wa ukarabati na uboreshaji miundombinu ya umeme jijini Dar es salaam katika maeneo ya Ilala, Jangwani Beach, Kunduchi, Mwananyamala, Muhimbili na Msasani unatekelezwa na Serikali ya Tanzania kupitia TANESCO kwa kushirikiana na Serikali ya Japan kupitia JICA unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Februali mwaka 2017.

Mhandisi Mramba alisema kuwa Miradi hiyo ya usafirishaji umeme na usambazi umeme inatekelezwa sambamba na miradi mikubwa ya ufuaji wa umeme wa Megawat 425 ya Kinyerezi II na upanuzi wa Kinyerezi I ambayo kwa sasa iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Mbali na hayo Mhandisi Mramba alisema kuwa tatizo la kukatika kwa umeme kumepungua ikilinganishwa na awali pia upotevu wa umeme umepungua kutoka asilimia 18 hadi asilimia 17 kwa mwaka 2016.

Kwa upande wake Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo ameutaka uongozi wa TANESCO kushughulikia na kumaliza changamoto ya kukatika kwa umeme nchini kwani kufikia uchumi wa kati kupitia viwanda itahitaji umeme wa uhakika.
Pia Waziri wa Biashara na Maendeleo wa Finland Bw. Kai Mykkanen, alisema kuwa Serikali ya Finland itaendelea kushirikiana na Tanzania katika masuala ya maendeleo hususani katika sekta ya Nishati.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni