BADO BARA LA AFRIKA LAKUMBWA NA KIGUGUMIZI CHA KUTEKELEZA ITIFAKI YA KUANZISHWA KWA MAHAKAMA YA AFRIKA YA HAKI ZA BINADAMU


 Image result for MAHAKAMA YA AFRIKA YA HAKI ZA BINADAMU NA WATU                                       

                    Na Mahmoud  Ahmad Arusha
Nchi 30 zimeridhia itifaki ya kuanzishwa kwa mahakama ya Afrika ya haki za binadamu na watu ambapo nchi 7 ndizo zimetoa tamko rasmi la kutambua na kukubali mamlaka ya mahakama ya Afrika ya haki za binadamu na watu kuweza kupokea kesi za watu binafsi na mashirika yasio ya kiserikali.

Ambapo imeonekana bado nchi za Bara la Afrika zimekumbwa na kigugumizi katika kufikia suala zima la kuridhia na kutambua na kukubali mamlaka ya mashirika ya binafsi na wananchi wake kuweza kupeleka mashauri mahakamani hapo hali inayowawia vigumu kuweza kufikia malengo ya mahakama hiyo.

Kauli hiyo imetolewa na waziri wa Katiba na sharia dkta Harrison Mwakyembe kwenye kongamano lililoandaliwa na mahakama ya Afrika ya haki za binadamu kusherehekea miaka 10 ya mahakama hiyo na kutathmini kazi za mahakama hiyo kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita katika kongamano lililofanyika jijini Arusha.

Dkta Mwakyembe alisema kuwa anasikitishwa sana kati ya nchi 30 zilizoridhia itifaki ya mahakama hiyo ni nchi saba ndizo zimekubali wananchi na mashirika yasio ya kiserikali kupeleka mashauri yake mahakama ya Afrika ya haki za binadamu na kuzitaka nchi nyingine kutekeleza kwa karibu itifaki hiyo.

Alisema kuwa wajibu wa nchi za bara la afrika ni kuunga mkono kwa vitendo itifaki hiyo itakayosaidia uwepo wa utawala bora unaoheshimu haki za binadamu pamoja na changamoto mbali mbali zinazoikabili nchi za bara hili ambapo nchi kama Tanzania inawajibu mkubwa katika kuhamashisha nchi nyingine kujiunga na mahakama hiyo.

Awali akiongea na waandishi wa habari Rais mahakama hiyo Jaji Sylvain Ore, alisema kuwa Lengo la kongamano hilo la siku mbili ni pamoja na kutathmini kazi za Mahakama hiyo katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Jaji Sylvain Ore,alisema kuwa kongamano hilo limehudhuriwa na wajumbe 150 ambapo mwishoni mwa kongamano watatoka na mapendekezo yatakayosaiodia kukuza utendaji wa shughuli za mahakama katika siku zijazo.

Wajumbe wa kongamano hilo ni pamoja na wasomi ,taasisi za mashirika yasiyo ya kiserikali,tasisi za Umoja na Afrika (AU) na wawakilishi wa masuala ya sheria na wale wa taasisi za haki za binadamu kutoka ukanda wa Afrika .

Aidha kongamano hilo litafuatiwa na kikao cha ngazi ya juu cha Umoja wa Afrika kuhusu haki za Binadamu kitakacho fanyika November 23-26, pia  jijini Arusha.

Kikao hicho, ambacho kinatarajiwa kufunguliwa na Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kitapitisha mpango kazi wa miaka 10 kuhusu ukuzaji na ulinzi  wa haki za Binadamu barani Afrika.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni