Upo
mjadala unaoendelea na kufukuta kuhusu uamuzi wa Serikali kupeleka
Muswada wa Sheria Bungeni kufanya marekebisho katika Sheria ya Mifuko ya
Hifadhi ya Jamii. Muswada huo sijauona na haujawekwa hadharani. Hata
hivyo, lililopenyezeka katika vyombo vya habari ni taarifa ya azma hiyo
ya Serikali iliyotamkwa katika kikao cha Serikali na wadau kuwa Muswada
huo utafuta FAO LA KUJITOA.
Nimefuatilia
mjadala huo na kuisoma barua ya wazi ya vyama vya wafanyakazi kwa umma
ikilaani vikali nia hiyo ya Serikali na muswada. Nikasikia na kusoma
tena kauli mbalimbali za Serikali na Mamlaka ya Hifadhi ya Jamii (SSRA)
kuhusu azma hiyo na mambo mengine mengi yanayoambatana na muswada
unaondaliwa. Kwa maelezo hayo, muswada huo una mambo mengi zaidi ya
kinachoitwa fao la kujitoa. Aidha, maelezo yao ni kuwa muswada wenyewe
haujakamilika isipokuwa ni hatua ya maoni tu.
Ninachokiona
kwa haraka haraka ni kuwepo kwa ombwe la taarifa katika suala hili
jambo linalofanya mjadala wenyewe kwenda harijojo. Ombwe hili litafanya
hata muswada wenyewe ukitolewa tushindwe kuujadili vizuri na kwa
nafasi. Kwa sababu hiyo, nimejitolea kuchokoza mjadala kwa kuyaweka
bayana mambo 10 ya msingi ya kuyaelewa kuhusu hifadhi ya jamii kama
ninavyoyainisha hapa chini.
1.
Ipo tofauti kati ya dhana mbili 'AKIBA YA WAFANYAKAZI' na 'HIFADHI YA
JAMII' yaani Provident Scheme na Social Security. Provident Scheme
inakupa tu jumla ya fedha wewe na mwajiri mliyochangia siku ya kustaafu
na mnaachana kimoja. Social Security inahusisha mnyumbuliko wa mafao
ikiwemo malipo ya kila mwezi baada ya kustaafu, matibabu kwa mtu na
mwenza, gharama za maziko na malipo kwa mjane na kusomeshewa watoto.
Kutokana na uchanga wa mifuko hii, mafao bado yanatofautiana kati ya
mfuko na mfuko hatimaye mbeleni mafao yanapaswa kufanana katika mifuko
yote.
2.
Hifadhi ya Jamii ni Haki ya Kikatiba na si suala la hiyari. Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema kuwa kila mtu anahaki ya kupata
hifadhi. Aidha Hifadhi ni Haki ya Binadamu katika Tamko la Haki za
Binadamu na Mikataba ya Shirika la Kazi Duniani. Haki hiyo inaambatana
na wajibu kwa Serikali, Mwajiri na Mfanyakazi. Serikali kusimamia na
kuhakikisha Haki hiyo inatolewa na kupatikana, Mwajiri kumchangia
Mfanyakazi na Mfanyakazi kuchangia kwa mujibu wa Sheria.
3.
Hakuna kitu kinachoitwa FAO LA KUJITOA kulikuwepo na KUJITOA KWENYE
MAFAO. Kwa kuwa mifuko iliyopo iliundwa kwa sheria tofauti kwa nyakati
tofauti, baadhi ya mifuko ilikuwa bubu kuhusu kipengele cha kukataza
kujitoa hali iliyofanya watu kujitoa bila kukataliwa. Hivyo hakuna FAO
LA KUJITOA lililofutwa na hakuna Mfuko wowote wenye fao hilo.
Kilichofanyika ni kuoanisha Sheria mbali mbali za Mfuko na kuwa na
Sheria moja kurahisisha udhibiti na usimamizi ambapo katika Sheria hiyo
ya 2012 imetamka bayana kutokuwepo na kujitoa kuziba ombwe lililoachwa
na sheria mbalimbali.
4..
Hifadhi ya Jamii ni KINGA si AKIBA. Hifadhi ya Jamii ni sawa na bima ya
kumkinga mfanyakazi na mwanachama dhidi ya majanga yanayoweza kumpata
na kumpotezea uwezo wake wa kuzalisha na kujikimu. Majanga hayo ni kama
kustaafu,kupata vilema na kamwe si mfuko wa akiba na mikopo, chama cha
kuweka na kukopa au upatu. Hivyo michango yako katika hifadhi ya jamii
haiwezi kuwa mbadala wa wewe kujiwekea akiba na kuwekeza sehemu ya
kipato chako inayobaki kwako baada ya kukatwa mchango wako usiovuka
asilimia 10 ya mshahara wako(kwa wale wafanyakazi). Kushindwa kwako
kuweka akiba hakuhalalishi kugeuza Mfuko wako wa Hifadhi ya Jamii kuwa
ni Benki. Hoja ni kuongeza tija na hatimaye mishahara/kipato na kujenga
utamaduni wa kuweka akiba (culture of saving).
5.
Michango yetu kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ni MBEGU ambayo mavuno
yake yanatokana namna tunavyoendelea kuyapalilia na kunyunyuzia dawa kwa
kuendelea kuchangia. Huwezi kupanda leo na kuvuna kabla ya mazao
kukomaa au msimu wa mavuno kufika. KUJITOA KWENYE MAFAO NI SAWA NA
MKULIMA KULA MBEGU.
6.
Unapostaafu au kwa sababu yoyote unapolazimika kuhifadhiwa na jamii kwa
kupewa kinga una uwezo wa kutumia zaidi ya ulichochangia. Hifadhi ya
jamii hutoa kinga kwa kadiri ya uhitaji na si kwa kadiri ya mchango
pekee. Hii inatokana na uwekezaji unaofanywa na mifuko ya hifadhi ya
jamii kwa upande mmoja na muendelezo wa mitiririko ya michango kwa wale
ambao bado wako katika umri wa kuchangia. Mafao yako wewe baada ya
kuchukua kiinua mgongo yataendelea kulipwa na wale ambao bado
wanachangia. Hivyo, kuruhusu watu kujitoa ni kumomonyoa nguzo ya Hifadhi
ya Jamii ya vijana na wanaojiweza kuwafaa wazee na wasiojiweza. Ndivyo
ilivyo duniani kote.
7.Skimu
za Hifadhi ya Jamii tofauti na iliyokuwa skimu ya mifuko ya Akiba ya
Wafanyakazi inapaswa kugusa wananchi wote kwa kuwa ni haki ya kikatiba
na si wafanyakazi pekee. Inapaswa kugusa wasiojiweza,wasio na ajira,
waliojiajiri,wakulima, wanamichezo na wengine walioko kwenye sekta isiyo
rasmi. Tuendako kila mtanzania anapaswa kuwa mwanachama wa hifadhi ya
jamii kama ilivyo kwa nchi zilizoendelea ambako namba yako ya uanachama
wa hifadhi ya jamii ndio kitambulisho chako kikuu. Hivyo hoja ya kujitoa
katika mfuko ulipwe ukajiajiri haijitoshelezi. Huko tuendako hata
ukijiajiri hatimaye itakuwa ni lazima uchangie hifadhi ya jamii kama
ilivyo lazima sasa kulipa kodi alimradi una kipato kiwe cha kuajiriwa au
kujiajiri. Kujiunga katika hifadhi ya jamii kwa wasio waajiriwa katika
sekta rasmi ni hiyari tu kwa sasa katika kipindi cha mpito.
8.
Tanzania imeingia katika skimu hii mwanzoni mwa miaka ya 2000
tulipobadilisha mifuko iliyokuwapo. Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi (NPF)
ukawa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na uliokuwa Mfuko wa Pensheni kwa
Mashirika ya Umma (PPF) ukabadilika kutoka kuwa mfuko wa Mashirika ya
Umma tu na kuwa mfuko wa kila mtu, na Serikali kuunda PSPF, LAPF nk.
Sisi Tanzania ndio tumeianza safari ya kuelekea kwenye hifadhi ya jamii
na bado hatujafikia huko. Katika muda mfupi manufaa yameanza kuonekana
kadri uwezo wa mifuko unavyoongezeka na kupata faida. Leo tuna bima ya
afya, fao la ulemavu kazini, fao la kujifungua, fao la elimu, fao la
afya vijijini nk. Huko tuendako, mafao haya yatafanana katika mifuko
yote na upo uwezekano wa mifuko yote ya sasa kuunganishwa na kuwa
mmoja. Hatuwezi kufika huko ikiwa wanachama wataruhusiwa kujitoa kila
wanapojisikia kufanya hivyo maana itaathiri uimara wa mifuko.
9.
Kama ilivyo kanuni ya msingi kwa sheria yoyote, katika kila sheria
lazima kuwepo na mazingatio (exceptions). Zipo aina ya sekta au kazi
ambazo kwa mazingira yake ya asili ya shuruba zake hakuna mfanyakazi
anayeweza kuhimili kuwa na uwezo wa kufanya kazi hizo hadi miaka 55.
Aina hizi za kazi humfanya mfanyakazi apoteze uwezo wake wa kufanya kazi
na kuchangia kutokana na sababu za kiafya (na)au ulemavu. Lazima sheria
itambue watu wa aina hii na kazi za aina hii ili kuwawezesha hawa
kuanza kunufaika na hifadhi ya jamii kabla ya umri wa kisheria uliowekwa
wa kuchangia kwa miaka 15 au kupata mafao ya kiinua mgongo kabla ya
miaka 55 kwa hiyari na 60 kwa lazima. Hawa wanahitajika kuwekewa FAO
lao (si kujitoa) mahsusi la kuwahifadhi, kuwasitiri na kuwakinga dhidi
ya kudhalilika na kufadhaika katika jamii. Hawa wanahitaji hifadhi.
Mjadala wetu wafaa kuelekezwa hapo tunapojadili kuhusu marekebisho ya
Sheria. Pia tujadili pendekezo la fao la kukosa ajira na ikiwezekana
kama tunaweza kutumia michango yetu kama dhamana kukopea nyumba,
kujisomesha nk na si kujitoa. Tusipoteze lengo kwa kile alichokisema
Mwl. Nyerere, 'Tukipoteza muda mwingi kugawana KIBABA tutapoteza wasaa
wa kugawana PISHI'.
10.
Mimi na wewe hatuiujui kesho yetu wala hatuna uhakika wa msaada wa
ndugu zetu na rafiki zetu pale tutakapofikwa na uzee au janga. Hifadhi
ya Jamii ndio mbeleko yetu ya kujishikizia. Mimi na wewe na wengi wetu
ambao ndio wafanyakazi wengi wa Tanzania ambao hatujachangia mifuko kwa
zaidi ya miaka 15 kuweza kustahili mafao ya pensheni tuna maslahi gani
na kujitoa kwenye mafao? Hao viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi
wanaotutia hamasa mbona wote umri wao umeshakwenda na wamekaa mkao wa
kufaidika na pensheni? Tukumbuke Ujana Ukuta na Fainali Uzeeni.
Inawezekana kabisa sijatoa majawabu na ieleweke haikuwa lengo langu. Lengo langu ni kuchokoza tu mjadala. Tujadili.
*Ndugu Kibaja Kariongo ni
mdau wa harakati za wafanyakazi
mdau wa harakati za wafanyakazi
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni