MHE. JENISTA MHAGAMA: “SERIKALI IMETIBU WAATHIRIKA WA TETEMEKO LA ARDHI MKOANI KAGER BURE”.

kae1
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama (kulia) akiangalia athari ya tetemeko katika eneo la Shule ya Msingi Bieju Kata ya Mtukula wakati alipowasili Wilayani Misenyi kwa ajili ya ziara ya kushuhudia baadhi ya maeneo yaliyoathirika na tetemeko la ardhi Mkoani Kagera leo 21 Septemba, 2016.
kae2
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama (kulia) akipokea maelezo juu ya idadi na thamani ya uharibifu katika shule ya Sekondari Mtukula toka kwa Mkuu wa Wilaya ya Misenyi, Luteni Kanali Denice Filangali Mwila wakati alipowasili Wilayani hapo kwa ajili ya ziara ya kushuhudia baadhi ya maeneo yaliyoathirika na tetemeko la ardhi Mkoani Kagera leo 21 Septemba, 2016.
kae3
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama (kushoto) akiongea na wakazi wa Kata ya Bugandika, Wilayani Misenyi wakati alipofanya ziara Wilayani hapo kushuhudia baadhi ya maeneo yaliyoathirika na tetemeko la ardhi Mkoani Kagera leo 21 Septemba, 2016. PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-WHUSM. 

                                      Na Benedict Liwenga-WHUSM, Kagera.

SERIKALI imetibu wananchi bure ikiwa ni sehemu ya msaada wake kwa waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera.

Kauli hiyo imetolewa leo Mkoani Kagera na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama wakati alipofanya ziara Wilayani Misenyi kushuhudia baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa na tetemeko la ardhi.

Mhe. Mhagama ameeleza kuwa, Serikali hadi hivi sasa imewatibu watu zaidi ya 400 kupitia hospitali zake za Wilaya na Mkoa kwa kuagiza madaktari kutoka nchini China ambapo zoezi la kusambaza damu pamoja na dawa za kutosha kwa waathirika lilifanyika na hakuna mwananchi aliyetozwa fedha kama malipo ya huduma hiyo.

“Tuishukuru Serikali yetu kwa kutusadia kupata dawa na damu ya kutosha na tulihakikisha kuwa kila mtu aliyepatwa na tetemeko na kujeruhiwa anatibiwa kwa gharama za Serikali ndiyo maana tuliagiza madaktari kutoka China pamoja na Mwanza ili kusaidia kuwatibu wananchi waliopatwa na majeraha makubwa”, alisema Mhe. Mhagama.

Aliongeza kuwa jumla ya wagonjwa ambao kwa sasa wanaendelea kutubiwa hospitalini ni 23 na ndiyo ambao wamefanyiwa upasuaji mkubwa na hali zao zinaendelea vizuri tofauti ilivyokuwa hapo awali.


Alifafanua kuwa, Serikali haiwezi kumsaidia kila mtu kwani haina uwezo huo lakini inajitahidi kurejesha miundombinu yake na taasisi zake zikiwemo zahanati, shule barabara kwa kushirikiana na wadau wanaojitokeza kuunga mkono juhudi za kuwasaidia waathirika wa tetemeko hilo, hivyo ametaka wananchi kujitokeza na kushirikiana kwa pamoja katika kuwasaidia waliopatwa na tukio hilo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Misenyi Luteni Kanali Denice Filangali Mwila amesema kuwa katiika Wilaya yake sehemu iliyoathirika zaidi ni Kata ya Minziro ambapo jumla ya nyumba 512 haziwezi watu kuishi,pia nyumba 1,524 zenye nyufa mbalimbali zinazohitaji ukarabati, Taasisi za serikali 91 na taaisis 71 za watu binafsi ikiwemo makanisa na misikiti imeathirika na tetemeko hilo.

Ameongeza kuwa tayari amepata msaada wa Serikali katika tukio hilo kupitia Kamati ya Maafa ni ambapo jumla ya maturubai 520 amepewa kwa ajili ya maeneo mbalimbali, chakula, blanketi 240 ambazo pia zimegaiwa kwa waathirika pia.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Bugandika Bw. Amudi Migeyo amewataka wananchi wake kutobeza juhudi za Serikali zinazofanywa sasa ambapo amewataka kuridhika na chochote wakipatacho katika kipindi hiki kigumu.

Hivi karibuni siku ya tarehe 10 Septemba, 2016 mkoa wa Kagera ulikumbwa na ukubwa wa nguvu za mtetemo wa ardhi wa tetemeko la 5.7 kwa kutumia skeli ya ‘Ritcher’ ambapo jumla ya watu 17 walipoteza maisha na majeruhi kadhaa ambapo wengi wao wameshapatiwa matibabu na wanaendelea vizuri.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni