SIKU chache baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuahidi serikali 
kuangalia uwezekano wa kuishtaki Benki ya Standard ICBC ya Uingereza 
kuhusiana na ufisadi uliofanyika katika mkopo wa Dola za Marekani 
milioni 600 (Sh trilioni 1.2) ambazo serikali ilikopa kwa kutumia Hati 
Fungani, imebainika kuwa uchunguzi kuhusiana na suala hilo upo katika 
hatua za mwisho.
 Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru Kamishna, Valentino Mlowola 
Benki hiyo inadaiwa kutoa hongo ya dola za Marekani milioni 6 (Sh 
bilioni 12) kama rushwa kwa maofisa wa serikali ili iweze kupata 
biashara hiyo nchini.
Waziri Mkuu Majaliwa akizungumza na gazeti hili hivi karibuni alisema
 serikali itafanyia kazi maoni ya wadau mbalimbali wakiwemo wabunge 
wanaoshauri kushtakiwa kwa benki hiyo kutokana na kashfa hiyo.
“Sisi kama Serikali tutaifanyia kazi na pale tutakapoona tumefikia 
katika hatua ya kutoa taarifa kwa umma kuhusiana na utekelezaji wa 
ushauri huo, tutafanya hivyo,” alisema Waziri Mkuu.
Akizungumza na gazeti hili juzi, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia
 na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Kamishna Valentino Mlowola alisema 
taasisi hiyo inaendelea na uchunguzi huo ulio katika hatua za mwisho 
ikishirikiana na vyombo mbalimbali vya uchunguzi vya ndani na nje ya 
nchi.
Mkurugenzi huyo alisema uchunguzi huo utakapokamilika hivi karibuni, 
serikali itakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kuamua kuhusu benki hiyo 
kushtakiwa au kutoshtakiwa kuhusiana na suala hilo.
“Wakati wowote uchunguzi huu utakamilika na hivyo suala hilo 
litapatiwa ufumbuzi na taarifa rasmi itatolewa kwa wananchi ili wajue 
hatma ya fedha zao zilizochukuliwa isivyo halali katika suala hili,” 
alisema Mlowola.
Inadaiwa kuwa Machi 8, 2013 Serikali ya Tanzania ilikopa fedha dola 
za Marekani milioni 600 sawa na Sh trilioni 1.2 kutoka nje kwa msaada wa
 Benki ya Standard ya Uingereza ambayo sasa inaitwa Standard Bank ICIC 
Plc kwa kuweka Hati Fungani.
Mkopo huo wenye riba yenye kuweza kupanda ulianza kulipwa mwezi Machi
 mwaka huu na utalipwa mpaka mwaka 2020 kwa mikupuo 9 inayolingana.
Ifikapo mwaka 2020, Tanzania italipa deni hilo pamoja na riba jumla 
ya Dola za Marekani milioni 897 (karibu Sh trilioni 2), lakini hata 
hivyo wadau mbalimbali wakiwemo wabunge wanadai kuwa mkopo huo 
umegubikwa na ufisadi huku benki hiyo ikidaiwa kutoa hongo ya dola za 
Marekani milioni 6 (Sh bilioni 12) kama rushwa kwa maofisa wa serikali 
ili iweze kupata biashara hiyo.
Baada ya kuibuka kwa sakata hilo, Takukuru walitumia taarifa ya 
Taasisi ya Uchunguzi wa Makosa Makubwa ya Uingereza (SFO) katika 
kuchukua hatua zinazostahili dhidi ya Watanzania wanaotajwa katika 
sakata hilo. Hata hivyo inalalamikiwa kuwa SFO haikufanya uchunguzi 
dhidi ya Benki ya Uingereza ya Standard.
Akizungumzia suala hilo, Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto (ACT- 
Wazalendo) alisema maslahi ya Tanzania katika sakata hilo yatakuwa 
makubwa endapo serikali itaweza kufanikiwa kuonesha kuwa Benki ya 
Standard ilihonga kupata biashara hiyo nchini.
Akitaja faida hizo Zitto alisema, “ moja, itakuwa ni fundisho kubwa 
kwa kampuni za kimataifa kwamba Afrika si mahala pa kuhonga na kupata 
kazi na kutoadhibiwa. Mbili, Tanzania haitalipa mkopo huu na riba zake. 
Tutakuwa tumeokoa zaidi ya Sh trilioni 2 katika Deni la Taifa na 
kuelekeza fedha tulizokuwa tulipe riba kwenda kwenye kuhudumia wananchi 
wetu kwenye afya na elimu,” alisema Zitto.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni