Arusha kulindwa kwa CCTV- Camera


Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo (katikati) akizungumza na
Balozi wa Sweden Nchini Tanzania Bi. Katarina Rangnite akizungumza
aliyeambatana na Wabunge toka Sweden walipotembelea Ofisini kwake hivi karibuni.



ARUSHA

MKOA wa Arusha umeanza kujipanga katika utaratibu wa kulinda
mji kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya CCTV – Camera ili kuimarisha usalama
wa mji “Safe City”, Mfumo huu utawezeshya Mji kulindwa masaa 24 dhidi ya
uhalifu kwa raia, wawekezaji na watalii.

Kauli hiyo ilitolewa leo mjini hapa na Mkuu wa Mkoa huo Mrisho Gambo ofisini
kwake mara baada ya kutembelewa na Balozi wa Sweden nchini, Bi. Katarina
Rangnite aliyeambatana na Ujumbe wake wa Wabunge kutoka Nchini Sweden.
Akizungumza na ujumbe huo RC Gambo alisema, mkoa huo tayari umekwisha
kuonyesha nia ya kuwekeza katika mfumo huo ili kuwaongezea wananchi na
mali zao usalama zaidi.

“Nia yetu ni kuona hali ya usalama katika mkoa wa Arusha ikiwa ya juu sana ili
kuendelea kuwavutia watalii zaidi kutoka nchi mbalimbali Duniani. Malengo yetu
ni kuwa na mifumo itakayoulinda mkoa wetu kwa Saa 24 na mwaka mzima,”
alisema RC Gambo na kuongeza:
“Hatua hii itaongeza ulinzi kwa raia na mali zao, pia kwa wawekezaji waliopo
mkoani kwetu na watalii wanaokuja kutembelea hifadhi na vivutio mbalimbali
kwani Arusha ndio kitovu cha utalii hapa nchini,” alisema.

Kwa upande wake Balozi Rangnite ambaye kiongozi wa msafara huo
uliojumuisha pia wabunge kutoka Bunge la Sweden wanaowakilisha Kamati ya
Kilimo na Mazingira, alikubaliana na nia ya kuwekeza kwenye mfumo wa
usalama wa mkoa wa Arusha.

Balozi Rangnite alimueleza Mkuu wa Mkoa Gambo kwamba, nchi ya Sweden
inayo wataalamu waliobobea katika mifumo hiyo ya usalama wa miji hivyo
alimuomba Gambo kuwasilisha kwake maandiko ya vitu vinavyohitajika ili
kuwezesha mradi huo kutekelezwa.

“Tukipata maandiko mbalimbali ya mradi tunaweza kuangalia ni wapi Serikali
ya Sweden inaweza kuwekeza ikiwamo kusaidia kwa manufaa ya wananchi wa
nchi zote mbili,” alisema Balozi Rangnite.

Aidha Gambo alitoa ombi kwa Balozi wa Sweeden kushirikiana na Mkoa wa
Arusha kwenye Kampeni ya Kulinda vyanzo vya Maji ili kuwezesha mradi
mkubwa wa maji unaosimamiwa na mamlaka ya maji safi na maji taka
(AUWSA) kutekelezwa kwa mafaniko makubwa. Itakumbukwa kwamba
imepatiwa Bil 476 ili kumaliza tatizo la maji Jiji hapa.

Katika ziara ya ujumbe huo pamoja na mambo mengine ulikuwa na lengo la
kuangalia fursa mbalimbali za uwekezaji katika Kilimo, Mazingira na maeneo
muhimu kutoka mkoani Arusha.

Ujumbe huo kutoka Sweden ukiongozwa na Balozi Rangnite uliridhishwa na
kuvutiwa na maeneo ya utalii yaliyopo katika mkoa huo yakiwamo pia mazingira
rafiki yanayoruhusu uwekezaji kwa jamii yao.
Kiongozi wa ujumbe toka Sweden Bi. Matilda Irnkarns (kushoto) akikabidhi
zawadi yao kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo


Kutoka kushoto ni Balozi wa Sweden Nchini Tanzania Bi. Katarina Rangnite
akifuatiwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mashaka Gambo pamoja na
Kiongozi wa msafara wa wabunge toka Sweden Bi. Matilda Irnkarns kwenye
picha ya pamoja baada ya Kikao
Katika picha ya pamoja ni kutoka kushoto ni Katibu Tawala wa Mkoa Ndg.
Kwitega, Balozi wa Sweden nchini Tanzania Katarina Rangnite , Mkuu wa Mkoa
wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo, kiongozi wa msafara wa wabunge toka Sweden
Bi. Matilda Irnkarns, ujumbe toka Sweden pamoja na viongozi wa Ofisi ya Mkuu
wa Mkoa wa Arusha.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni