DC CHONGO AMTUMBUA MHASIBU MKUU LONGIDO

daniel-Chongolo
MKUU wa Wilaya ya Longido, Daniel Chongo
……………..
NA MWANDISHI WETU
MKUU wa Wilaya ya Longido, Daniel Chongolo amemwagiza Mkuu wa Polisi kumkamata na kumfungulia mashtaka Mhasibu Mkuu (DT) wa Halmashauri ya wilaya hiyo mkoani Arusha Issa Mbilu, kwa tuhuma za kuhusika na upotevu wa sh. milioni 84.
Akizungumza juu ya agizo hilo la kukamatwa Mhasibu huyo, Chongolo alisema uamuzi huo unatokana na upotevu wa fedha hizo zilizorudishwa na benki zilizokuwa zilipwe kwa watumishi hewa na wale waliokuwa na matatizo kazini.
“Leo (jana) tulikaa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ili pamoja na mambo mengine kukamilisha mchakato wa kupitia na kung’amua maendeleo ya kushughulikia tatizo la watumishi hewa. DT tulimwita ili asaidie kutoa maelezo katika eneo hilo.
“Tulipomhoji kuhusu fedha hizo zilizorudishwa na benki na kupaswa kurudishwa Hazina hakuwa na jibu. Nimeagiza polisi na vyombo vingine kufanya uchunguzi ili hatua za kisheria zichukuliwe juu yake,”alisema.
Alisema tayari polisi wanamshikilia Mbilu kutokana na tuhuma hizo na kwamba huenda wiki ijayo akapandishwa kizimbani kujibu tuhuma hizo.
Mkuu wa Wilaya Chongolo aliwaasa watumishi wote wa halmashauri hiyo kuwa makini na fedha za umma kwa kuwa hakuna atakaeonewa haya endapo atabainika kusababisha upotevu au kula fedha za umma.
Alisema yeye ndiye mwenye dhamana ya kusimamia uwajibikaji na nidhamu kwa watumishi wote wa serikali wilayani humo hivyo anataka kila mmoja kuona akitekeleza majukumu yake kikamilifu.
“Hatutakuwa na simile. Kila mmoja awajibike kwa kuzingatia sheria, utaratibu na maadili ya kazi. Tutakayembaini anakwenda kinyume na hapo tutamuwajibisha,”alisema.
Alisema anataka kuona Longido ikiwa ni miongoni mwa wilaya zinazokimbiliwa na wawekezaji kwenye sekta mbalimbali ikiwemo ya ufugaji kwa kuwa kuna rasilimali nyingi zenye uwezo wa kuinua uchumi wa Arusha na taifa kwa ujumla.
“Endapo kila mtumishi atatekeleza majukumu yake ipasavyo ni wazi wawekezaji watahamasika kuja kuwekeza katika wilaya yetu lakini hawawezi kufanya hivyo kama kutakuwa na matukio ya ajabu ikiwemo utafunaji fedha na urasimu,”alisema.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni