MSAJILI
wa Vyama vya Siasa nchini Jaji Francis Mutungi kwa mamlaka aliyonayo
chini ya kifungu cha 19 cha Sheria ya vyama vya Siasa namba 5 ya mwaka
1992, amevifutia usajili wa kudumu vyama vitatu vya siasa kuanzia leo
hii.
Akizungumza
katika mkutano na waandishi wa habari ofisini kwake leo asubuhi Jaji
Mutungi alivitaja Vyama alivyovifuta kuwa ni Chama cha Haki na Ustawi
(Chausta), kilichopata usajili wake Novemba 15, 2001 kilichokuwa
kikiongozwa na James Mapalala kama Mwenyekiti wa Taifa na Mwaka Lameck
Mgimwa kama Katibu Mkuu.
Chama
kingine alichokifutia usajili wa kudumu ni Chama cha The African
Progressive Party of Tanzania (APPT Maendeleo) kilichopata usajili Machi
4, 2003 kilichokuwa kikiongozwa na Peter Kuga Mziray kama Rais Mtendaji
Taifa na Nziamwe Samwel kama Katibu Mkuu.
Jaji
Mutungi alikita chama kingine alichokifuta kuwa ni Chama cha Jahazi
Asilia kilichokuwa kikiongozwa Kasimu Bakari Ally kama Mwenyekiti wa
Taifa na Mtumweni Jabir Seif kama Katibu Mkuu ambacho kilipata usajili
wa kudumu Novemba 17, 2004.
Mutungi
alisema vyama hivyo vimepoteza sifa za usajili wa kudumu kwa kukiuka
masharti ya Sheria ya Vyama vya Siasa, ambapo kila chama klipewa taarifa
ya nia ya Msajili wa Vyama vya siasa kufuta usajili wake wa kudumu na
kutakiwa kueleza kwanini kisifutwe ambapo vilishindwa kutoa sababu za
kuridhisha kuwa havikukiuka sheria na bado vinavyo sifa za usajili wa
kudumu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni