POLISI mkoani Morogoro wanashikilia watu 11, wakazi wa Kijiji cha Mpofu wilayani Kilombero kwa tuhuma za kuvamia na kuchoma moto kituo kidogo cha polisi na ofisi ya serikali ya kijiji hicho.
Watuhumiwa
hao ni sehemu ya zaidi ya watu 100 wanaodaiwa kufanya uhalifu huo
katika kituo hicho cha polisi Mbingu, katika taarifa ya Mgeta.
Watuhumiwa
hao wanadaiwa kufanya tukio hilo wakishinikiza polisi wamwachie
mtuhumiwa aliyewekwa mahabusu katika kituo hicho, Bashiri Kadugula (25),
kwa tuhuma za kumshambulia mkewe, Veronica Chabula (21) ili wamwadhibu.
Kamanda
wa Polisi wa mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo, alisema jana kuwa,
Kadugula aliwekwa ndani kwa kumkata mkewe kwa panga sehemu mbalimbali za
mwili kutokana na wivu wa mapenzi.
Alisema
katika tukio hilo ni la Agosti 20, mwaka huu saa 4:00 usiku, mtuhumiwa
huyo baada ya kufanya kitendo hicho kwa mkewe akitoroka na ndugu wa
Veronica walifanikiwa kumkamata na kumfikisha kituo kidogo cha Polisi
Mbingu, ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Alisema
baada ya ndugu kuondoka kituo cha polisi, kitambo kidogo kulitokea
kundi la watu wakirusha mawe kituoni hapo, wakitaka wamuue mtuhumiwa
huyo kwa kukerwa na kitendo chake cha kinyama. Kamanda Paulo alisema,
askari waliokuwepo kituoni hapo walijitahidi kuwazuia watu hao lakini
walizidiwa nguvu.
Alisema polisi walifanikiwa kumtoa mtuhumiwa mahabusu na kumwokoa sambamba na kuokoa silaha za kituo hicho.
Alisema,
watu hao waliokadiriwa kuwa zaidi ya 100, walivamia kituo hicho kidogo
cha Polisi na kukichoma moto ambapo nyaraka mbalimbali zilizokuwa ndani
ya kituo hicho ziliungua na kuteketea kabisa.
Kamanda
wa Polisi wa mkoa alivitaja vitu vilivyoteketea kwa moto kuwa ni pamoja
na pikipiki tano zenye usajili T 979 BGA aina ya Sky Mark, T901 BUJ
aina ya Sanlug, T801 BQA aina ya Sanlug, mali ya Askari Wilson, T194 BVR
aina ya T-Better, mali ya Askari Isaya na T904 BUJ aina ya Tianda.
Alisema,
kundi la watu hao baada ya kukichoma moto kituo kidogo cha polisi,
lilivamia pia Ofisi ya Serikali ya Kijiji cha Mpofu na kisha kuchoma
moto nyaraka mbalimbali, ambapo katika matukio hayo watuhumiwa 11
walikamatwa.
Amewataja
waliokamatwa kutokana na tukio hilo kuwa ni Imani Mwampombe (40),
Geofrey Mwaikambo (46), Eugen Kikoti (41), Janken Mwaikambo (55),
Meshack Kikoti (42), Eliud Chumbula (52) na Shukrani Lukimo (35) ambao
ni wakulima na wakazi wa kijiji hicho cha Mpofu.
Wengine
waliokamatwa ni madereva wawili wa bodaboda ambao ni Ramadhani Hussein
(29), mkazi wa Kitongoji cha Ngajengwana, Salum Ngala (36), John Mtikila
(55) na Rodrick Mwaikambo (36) wote wakulima na wakazi wa Kijiji cha
Tandale- Igima.
Kamanda
huyo wa Polisi wa mkoa alisema kwamba watuhumiwa hao wanaendelea
kuhojiwa na watafikishwa mahakamani mara upelelezi utakapokamilika na
kwamba polisi wanaendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine waliotoroka na
kusisitiza kuwa wananchi wanapaswa kutii sheria na kuacha kujichukulia
sheria mkononi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni