WIZI WA FEDHA KWA KUTUMIA MTANDAO TISHIO DUNIANI

Jitihada za serikali katika kupambana na uhalifu wa mitandao imeungwa mkono kutokana na baadhi ya vyuo kuanzisha mitaala yenye somo la ulinzi wa  mitandao .
Moja ya jitihada za serikali katika kukabiliana na changamoto hiyo ni kupeleka muswada wa kutunga sheria ya uhalifu wa mtandao ya mwaka 2015  katika mkutano wa 19 wa bunge la jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambao ulipitishwa na bunge hilo .
Taarifa ya waziri wa Mawasiliano , Sayansi na Teknologia , Profesa Makame Mbarawa kuhusu sheria hiyo inasema kukua kwa kasi kwa matumizi ya Teknolojia ya Habarina Mawasiliano (TEHAMA) kumeleta mafanikio ya kwa kuongezeka kwa huduma za mawasiliano, huduma za kifedha na matumizi ya mitandao ya kijamii.
Aidha, mafanikio hayo yameleta changamoto nyingi
katika jamii ikiwemo  kuibuka kwa makosa mapya ya jinai na pia mbinu mpya za kutenda makosa ya zamani. 
Makosa hayo    yanajumuisha uhalifu wa mitandao ambapo
simu za mkononi, kompyuta au mifumo ya kompyuta hutumika kama nyenzo za kutenda uhalifu huo.
Mifano ya makosa hayo ni pamoja na  Wizi wa fedha kwa njia ya mtandao,  Ugaidi unaofanyika kupitia kwenye mitandao,   Maudhui potofu yanayosababisha mmomonyoko mkubwawa maadili,  uharibifu wamiundombinu muhimu ya Taifa ikiwemo mkongo wa Taifa wa Mawasiliano. 
 Akizungumza na gazeti hili , mtaalam wa ulinzi wa mitandao Ezekiel Mpanzo amesema tatizo la wizi wa mitandao limekuwa kubwa na benki pamoja na wananchi wamekuwa wakiingia hasara  kutokana na kutoligundua.
 Mpanzo ambaye pia ni mkuu wa chuo cha Teknologia na uongozi cha Kilimanjaro amesema  kwa upande wa vyuo vya ufundi vya NACTE  pamoja na vyuo vikuu wameliona tatizo hilo na wamejaribu kutengeneza mtaala ambao unasomo la kuzuiya wizi huo 
‘’ Tumetengeneza mtaala mzuri na kuingiza somo la ulinzi wa mtandao . Tumeuandaa sisi wenyewe na kuupeleka NACTE ambapo wameupitisha kwa hiyo tunaamini kwamba wanafunzi watakao maliza hapa watakuwa na ujuzi mkubwa na pia  utasaidia Taifa kwa ujumla kupunguza tatizo hilo ‘’ alisema Mpanzo . 
Amesema njia nyingine ya kuzuiya tatizo hilo ni wataalam wa hapa nchini ambao ni wachache kujiunga na vyama vya kuzuiya uhalifu wa mitandao duniani . 
‘’Wataalam wa hapa nchini wakijiunga na vyama hivyo vikiwamo Ethical hacking na  CISCO itasaidia kubadilishana uzoefu kuhusu mbinu wanazotumia wahalifu duniani kote kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknologia ‘’ aliongeza Mpanzo. 
Alisema uhalifu huu hawakubaliani nao,  cha kufanya ni kuwa na wataalam ambao siku zote wanataarifa zaidi kuliko wahalifu na wataalam wa hapa nchini wafanye mitihani ya ulinzi wa mitandao na wanapofaulu wapewe vyeti na kusajiliwa katika vyama vya ulinzi wa mitandao duniani .
 Changamoto ya uhalifu wa mitandao imekuwa ikileta mijada ambapo katika mkutano wa kuzuiya wizi kwa kutumia mitandao ilibainishwa kuwa kati ya mwaka 2010 na robo ya mwaka 2013 Tanzania ilipoteza shilingi bilioni 9.8 kutokana na wizi huo ambao ulifanywa katika mashine za benki za kitolea fedha za ATM. 
Ripoti hiyo ya septemba mwaka jana , ilitolewa katika mkutano wa kuzuiya wizi kwa kutumia mitandao ya nchi za Afrika ya mashariki mjini Arusha .
Akifungua mkutano huo , Naibu waziri wa mambo ya ndani Pereira Silima anabainisha kuwa kuna kesi zaidi ya 300 za uhalifu wa mitandao ambazo zinachunguzwa hapa nchini na baadhi ya hizo ziko karibu kufikishwa mahakamani
‘’ Pia kutokuwepo kwa raslimali za kutosha , kukosekana kwa uelewa wa kutosha wa kushughulikia masuala hayo kwa baadhi ya polisi wetu na wengine wanaofanya sheria zitekelezwe kunasababisha mapambano ya uhalifu wa mitandao kurudi nyuma ‘’ alisema
Katika ripoti yao washiriki wa mkutano walishauri  kwamba serikali kama mdau mkuu lazima ashirikiane na sekta binafsi na taasisi za kimataifa katika kuwaelimisha wanafunzi wa vyuo vya teknologia ya habari na mawasiliano .
Mengine ni kutafuta fedha kwa ajili ya kugharamikia program za utafiti ili kuongeza uelewa uliopo sasa na kutafuta nyingine za kuzuiya uhalifu huo .
Kwa upande wa vyuo , Mpanzo anasema wao wanafundisha kozi ya usalama wa mitandao lakini kinachokosekana ni wataalam wa kutosha waliobobea katika fani ya ICT kutokana na somo hilo kufundishwa kwa nadharia zaidi .
‘’ Kukosekana kwa wataalam waliobobea kunachangiwa na fani hiyo kutolewa kwa nadharia zaidi kuliko vitendo kutokana na uhaba wa vifaa vya kufundishia pamoja na maabara za kisasa za ambazo zitamwezesha mwanafunzi kujifunza kwa ufanisi ‘’ anasema na kuongeza .
Ameshauri serikali kutilia mkazo mfumo wa NACTE wa  ngazi ya cheti na diploma  kwani uzoefu umeonyesha kuwa wanafunzi wakipitia mfumo huo hadi vyuo vikuu wanakuwa watendaji wazuri kutokana na kupata mafunzo zaidi kwa vitendo .
Kwa wanafunzi ambao hawakufaulu kidato cha nne na cha sita wanaweza kusaidiwa kwa kupitia mfumo huu kwa kusoma kozi zinazofundishwa moja kwa moja kwa vitendo  kama zinazotolewa na chuo cheti ikiwemo CISCO networking ambayo ni ya kimataifa na inafahamika duniani kote pamoja na Microsoft server, oracle data base .
‘’ Naiomba serikali kuangalia namna ya kuwasidia kwa kuwalipia ili waweze kusoma kupitia mfumo wa diploma . Faida za kupitia mfumo huu ni kwamba mwanafunzi anapomaliza na kufika chuo kikuu anakuwa mzuri zaidi kwasababu anajifunza zaidi kwa vitendo na atakuwa katika nafasi nzuri ya kupata ajira ‘’ alisema Mpanzo . 
Tatizo la wizi kupitia mitandao  ni kubwa duniani kwani ripoti iliyotolewa na kampuni ya Kaspersky lab inasema genge la wahalifu wa mtandao limefanikiwa kuiba mamilioni ya dola za kimarekani kutoka kwenye akaunti za wateja wa benki 1000 katika mataifa 30 kati ya mwaka 2014 na 2015 
Wizi huo ulianza mwaka 2013 na bado unaendelea mpaka leo kwani benki zote zilizoathirika hazina uwezo wa kuwazuiya . Genge la Carbanak , linatumia mbinu ya kuambukiza virusi kwenye mashine za benki ikiwamo kamera za CCTV ili kunakili kila kitu kinachoandikwa kwenye komputa .
Ripoti hiyo inaelezea mbinu mpya za wahalifu mtandao wanazotumia kudukua nambari za akaunti za wateja za siri kabla ya kuingia na kuiba fedha.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, benki katika mataifa 30 yakiwamo , Russia , Marekani, Ujerumani , China , Ukraine na Kanada yameathirika kwa asilimia kubwa .
Hivi karibuni benki ya CRDB iliwaonya wateja wake kuwa makini na baadhi ya mitandao inayoibuka na kulaghai kwa kuwataka wananchi kutoa taarifa zao muhimu za kibenki jambo ambalo linahatarisha usalama wa fedha zao .

Mkurugenzi mtendaji wa benki hiyo , Dk. Charles Kimei anasisitiza wananchi wanatakiwa kuwa makini na kundi hilo , wasikubali kudanganyika kwa kutoa taarifa zinazohusiana na nyaraka nyeti za benki zao na kusisitiza kuwa ni  marufuku kutoa taarifa hizo kwa wafanyakazi wa benki .

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni