MPINA APIGA MARUFUKU UKAMATAJI HOLELA WA MIFUGO


NA JOHN MAPEPELE, MOROGORO
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amepiga marufuku tabia ya
ukamataji mifugo kiholela inayofanywa na baadhi ya watumishi wa umma na
kusababisha mifugo mingi kufia mikononi mwa Serikali kwa kukosa huduma
muhimu ikiwemo maji, malisho na matibabu na hivyo kusababisha hasara
kubwa kwa wafugaji na Taifa kwa ujumla.
Mpina amesema katika
siku za hivi karibuni kumeibuka tabia ya baadhi ya watendaji wa Serikali
kuendesha operesheni za kukamata mifugo na kuifungia bila kuipatia
huduma muhimu ikiwemo maji, malisho na matibabu na matokeo yake mifugo
mingi hufa na kusisitiza kuwa operesheni hizo zinapofanyika ni lazima
zihusishe pia maofisa wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kuwa na uelewa wa
pamoja wa jambo hilo.
Aidha Mpina alisema utaratibu
unaofanyika hivi sasa wa kukamata hovyo mifugo ni ukiukwaji wa sheria
namba 17 ya Magonjwa ya Wanyama ya mwaka 2003 na, Sheria ya Ustawi wa
Wanyama Namba 19 ya Mwaka 2008 ambazo zinataka mifugo inapokamatwa
kuzingatia masuala ya magonjwa na ustawi wa mifugo katika kipindi chote
inapokuwa imeshikiliwa.
Akifunga maonesho ya 25 ya Nane nane
Kanda ya Mashariki inayojumuisha mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani na
Morogoro katika viwanja vya Mwalimu JK Nyerere mjini Morogoro kwa niaba
ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Waziri Mpina pia alielezea
kutoridhishwa na utoaji wa mikopo wa Benki ya Kilimo (TADB) ambapo kwa
taarifa iliyotolewa sekta ya uvuvi hakuna mkopo wowote uliotolewa
katika mwaka wa fedha uliopita huku upande wa sekta ya mifugo
wakiambulia wajasiamali wanne tu .
Aidha kiasi cha jumla ya
mikopo iliyotolewa ya Sh. Bilioni 39 kwa mwaka mzima ni kidogo sana
ikilinganishwa na mahitaji wa mikopo katika sekta za kilimo,mifugo na
uvuvi, huku akipongeza kazi nzuri inayofanywa na Taasisi ya PASS na
SAGGOT-CTF katika kuwadhamini wakulima , wafugaji na wavuvi katika
kupata mikopo.
Kutokana na changamoto hizo, Waziri Mpina
ameitaka benki hiyo kurekebisha kasoro zilizopo na kujipanga vizuri
kuhudumia sekta hizo, vile vile amewaagiza makatibu wakuu wa Kilimo,
Mifugo na Uvuvi kuitambua na kupitia miradi yote ya wajasiriamali katika
sekta zao ili kuwezesha upatikanaji wa mikopo kwa wakati.
Sambamba
na hilo amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kupitia idara
ya maendeleo ya jamii na idara ya ushirika kuwaandaa na kuwaunganisha
wananchi katika kukidhi vigezo vya kupata mikopo katika taasisi za
fedha.
Pia aliagiza Halmashauri zote nchini kuwatambua vijana
wanaohitimu mafunzo katika vyuo vya ugani vya SUA, FETA, LITA na ATI na
kuwatumia katika safari ya kuleta mageuzi ya uvuvi,mifugo na kilimo
katika maeneo yao na kwamba hata mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa
wanawake,vijana na walemavu kundi hili la wagani liangaliwe kwa jicho la
pekee.
Mbali na hilo Waziri Mpina alisema pamoja na Serikali
kuwekeza fedha nyingi katika ujenzi wa mialo na masoko ya samaki baadhi
ya halmashauri zimetelekeza miundombinu hiyo na kuendelea kutoa huduma
katika maeneo yasiyo rasmi, pia baadhi ya mialo na masoko haifanyiwi
matengenezo wala ukarabati kiasi cha kukosa huduma muhimu kama maji,
vyoo, umeme na majokofu ya kuhifadhia samaki hali inayosababisha
usumbufu na hasara kwa wananchi licha ya kutozwa ushuru kila uchao.
Kufuatia
hali hiyo Waziri Mpina ametoa miezi mitano kwa Halmashauri zote nchini
kuhakikisha zinakarabati na kuweka huduma muhimu na kwamba wataoshindwa
kufanya hivyo mialo na masoko hayo yatarejeshwa chini ya usimamizi wa
Wizara na halmashauri hizo hazitaruhusiwa tena kukusanya mapato
yatokanayo na sekta hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mkoa
wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo alimhakikishia Waziri Mpina kuwa
maagizo yote aliyotoa watayafuatilia na kuyasimamia ili kuona
utekelezaji wake kwani Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuleta
mageuzi ya kweli katika sekta za Kilimo,Mifugo na Uvuvi.
Pia
Ndikilo alisema ni jambo la kusikitisha kuona licha ya fursa kubwa za
mifugo na uvuvi zilizoko katika mikoa ya Kanda ya Pwani lakini hadi sasa
hakuna kiwanda hata kimoja cha kuchakata samaki wala nyama na kumuomba
Waziri Mpina kuandaa kongamano ya mikoa hiyo ili kujadili kwa pamoja
namna ya kuwekeza katika viwanda vya kuchakata bidhaa hizo.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Kebwe Stephen Kebwe alisema maonesho hayo
ya mwaka huu yamekuwa na mafanikio makubwa kwani wakulima,wafugaji na
wavuvi na makundi mengine yamejitokeza kwa wingi na wamepata fursa ya
kujifunza teknolojia mpya zitakazoboresha uzalishaji.
Maonesho hayo yalihudhuriwa na wakuu wa mikoa, wilaya, mameya,
wakurugenzi wa halmashauri,madiwani pamoja na sekta binafsi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni