BARABARA YA NYIGO-IGAWA CHACHU YA MAENDELEO NYANDA ZA JUU KUSINI


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, (wa pili kushoto) akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Njombe Mhandisi Yusuph Mazana (wa tatu kushoto), wakati akikagua nguzo ya daraja la mto Halali katika barabara ya Nyigo-Igawa yenye urefu wa KM 64.6 wilaya ya Wanging'ombe, mkoani humo. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole- Sendeka, akisikiliza.

Serikali imesema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya Nyigo-Igawa yenye urefu wa KM 64.6 kwa kiwango cha lami kumepunguza ajali zilizokuwa zikitokea na kutarahisisha shughuli za kibiashara na usafirishaji wa mazao katika kanda ya nyanda za juu kusini. Amezungumza hayo mkoani Njombe, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe, wakati alipokuwa akikagua ujenzi wa barabara hiyo inayojengwa na mkandarasi wa Kampuni ya China Railway Seventh Group.

Waziri Kamwelwe amesema kuwa ameridhishwa na ujenzi wa barabara hiyo pamoja na madaraja yake ambao kwa sasa umefikia asilimia 97. "Nimeridhika na ujenzi wa barabara hii kwa kuwa hapo awali ilikuwa inaelezwa kuwa na ajali nyingi lakini sasa zimepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na upana wa barabara hii kufikia mita tatu na nusu kila upande na mabega ya mita moja na nusu" amesema Waziri Mhandisi Kamwelwe.
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Njombe Mhandisi Yusuph Mazana, akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe (wa pili kulia), na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole- Sendeka (kulia), kuhusu hatua mbalimbali zilizofikiwa katika kitengo cha mizani iliyopo eneo la Makambako mkoani humo.

Ameongeza kuwa Serikali inaendelea na miradi ya ujenzi na ukarabati wa barabara nyingi hapa nchini kwa ubora na viwango vya juu ikiwa na lengo la kurahisisha usafirishaji, kuleta maendeleo kwa wananchi na kupunguza ajali.

"Hakuna Serikali inayopenda kupoteza wananchi wake katika ajali za barabarani hivyo ujenzi wa barabara utaenda sambamba na usalama wa wananchi wetu kwa kuwekewa alama, taa na michoro barabarani", amesisitiza Mhandisi Kamwelwe.

Kuhusu mzani wa makambako, Mhandisi Kamwelwe amesema kuwa mwarobaini wa foleni katika eneo hilo umepatiwa tiba kwa kuwa sasa magari yanapimwa pande zote mbili ili kuondoa msongamano. Aidha, amewataka wananchi kutoharibu miundombinu ya barabara ikiwemo alama za barabarani, taa pamoja na vyuma vinavyowekwa chini ya madaraja kwani vitu hivyo vina umuhimu wake na huongeza umakini kwa madereva wawapo barabarani.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, (wa kwanza) na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole-Sendeka, wakitoka kukagua kingo za daraja la mto Halali lililopo katika barabara ya Nyigo-Igawa yenye urefu wa KM 64.6 wilaya ya Wanging'ombe, mkoani humo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole-Sendeka, pamoja na kuishukuru Serikali kwa ujenzi wa miradi ya barabara za wilayani amemuomba Waziri Kamwelwe kujenga kipande cha barabara kwa kiwango cha lami kinachoelekea katika eneo la mgodi wa madini ya chuma tarafa ya Mndindi wilayani Ludewa. Amemuelezea pia umuhimu wa kujenga barabara ya Kibena-Lupembe ambayo bado haijaanza kujengwa na inatengewa fedha kila mwaka kwani ndio eneo lenye uzalishaji mkubwa wa mazao na barabara hiyo inaunganisha mkoa wa Njombe na mkoa wa Morogoro.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Njombe, Mhandisi Yusuph Mazana, amesema kuwa mpaka sasa kazi zilizobaki katika barabara hiyo ni uwekaji wa alama za barabarani, michoro ya barabarani, kingo na taa za barabarani na kazi ya mifereji ya maji.

Mhandisi Mazana amemueleza Waziri Kamwelwe kuwa katika eneo la Makambako barabara mpya imehamia upande wa kulia mita 2.5 na kuathiri baadhi ya maeneo ya wananchi wapatao kaya 22 na hivyo tathimini ya mali zilizoathirika zinaendelea kuandaliwa kwa ajili ya malipo ya fidia. Ujenzi wa barabara ya Nyigo-Igawa yenye urefu wa KM 64.6 ni sehemu ya mradi wa barabara ya Mafinga-Igawa KM 138.7 ambao umefadhiliwa na Serikali ya Tanzania kupitia mkopo wa Benki ya Dunia chini ya mradi wa Southern Africa Trade and Transport Facilitation Project (SATTFP) na utagharimu kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 103.
Kaimu Mhandisi Mkazi kutoka kampuni ya LEA JV South Asia, Manish Kumar (kushoto), akimuonesha ramani Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe (katikati), wakati akikagua ujenzi wa barabara ya Nyigo-Igawa yenye urefu wa KM 64.6 kwa kiwango cha lami, mkoani Njombe. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole-Sendeka akifuatilia.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, akisalimiana na mkazi wa kijiji cha Ilembula wilaya ya Wanging'ombe Bi. Hadija Samuli, wakati alipokuwa akikagua barabara ya Nyigo-Igawa yenye urefu wa KM 64.6 inayojengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Njombe.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya Nyigo-Igawa KM 64.6 inayojengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Njombe. Mradi wa ujenzi huo utakamilika mwezi Disemba mwaka huu na utagharimu kiasi cha zaidi ya Shilingi bilioni 103.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni