Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhani Ng’anzi akiwa akiwa katika kikao na Viongozi wa Makampuni ya Ulinzi Mkoa wa Arusha waliofika Ofisini kwake kwa ajili ya kujitambulisha
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha akiwa katika Picha ya pamoja na viongozi wa Makampuni ya ulinzi Mkoa wa Arusha pamoja na Baadhi ya Maofisa wa Polisi mkoani
………………………
Na Gasto Kwirini wa Polisi Arusha
Jeshi la Polisi Mkoani hapa limeyaonya baadhi ya Makampuni ya Ulinzi kuacha tabia ya kutumia magari yao ya dharura vibaya kinyume na utaratibu pindi wawapo barabarani.
Hayo yamesemwa leo na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhani Ng’anzi wakati akiwakaribisha ofisini kwake Viongozi wapya wa Makampuni ya Ulinzi Mkoa wa Arusha waliochaguliwa tarehe 11 Agosti mwaka huu katika Ukumbi wa Maofisa wa Polisi Arusha.
“Kuna baadhi ya Magari ya Makampuni ya Ulinzi yanatumiwa vibaya kwa kigezo cha kuwahi dharura japokuwa wakati mwingine huko waendako hakuna hiyo dharura inayowataka wafanye hivyo. Lakini pia pale kwenye ulazima msitumie magari hayo ya dharura kwa kubeba vitu haramu kama vile bhangi”. Alionya kamanda Ng’anzi.
Aidha aliwahakikishia kufuatilia na kuzifanyia kazi changamoto zao hasa za ucheleweshwaji wa utolewaji wa vibali vya umiliki wa silaha, ucheleweshwaji wa utolewaji wa matokeo ya alama za Vidole kwa Askari wapya wanaoajiriwa. Ameyataka Makampuni yenye changamoto hizo kuorodhesha majina yao kupitia viongozi hao, na kuyapeleka ofisini kwake ili aweze kuyafanyia kazi kwa kushirikiana na idara husika na matokeo ya Alama hizo na Vibali hivyo viweze kutolewa haraka na kwa wakati.
Pia amewahaidi kuwasiliana na Ofisi ya Mshauri wa Mgambo Mkoa wa Arusha ili Askari ambao hawakupata mafunzo wayapate kwa awamu huku wakiendelea na majukumu yao. Amewataka Viongozi hao kuorodhesha majina ya Askari hao na kuyapeleka Ofisini kwake.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Makampuni ya Ulinzi Mkoa wa Arusha Bwana Daudi Mungi kwa niaba ya Viongozi wenzake, alitoa shukrani kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha kwa ushirikiano wa mara kwa mara wanaondelea kuupata na kuhaidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi hilo wakati wote.
Awali akiwakaribisha Viongozi hao, Mkuu wa Operesheni wa Polisi Mkoa wa Arusha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Elias Tabana Mwita alisema kwamba ataendeleza ushirikiano uliopo kwa Makampuni ya ulinzi hasa ikizingatia kuwa mchango wa Makampuni hayo ni mkubwa katika kuimarisha ulinzi na usalama katika Mkoa huu. Pia aliwataka kufanya kazi kwa kufuata Sheria na taratibu zinazowaongoza.
Mwenyekiti wa Makampuni ya Ulinzi aliambatana na Viongozi wenzake ambao ni Makamu Mwenyekiti Bwana James Rugangila, Bi. Malima Macha ambaye ni Katibu, Naibu katibu Bwana James Babu na Mjumbe mmoja Bwana Rashid Mtungi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni