Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti (kushoto) akiteta jambo na
Mbunge wa Simanjiro James Ole Milya (katikati) na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Manyara
Mhandisi Tumain Magesa (kulia).
|
Waziri wa Madini Angellah Kairuki akiwa katika picha ya pamoja na
Wabunge wa Kamati ya Nishati na Madini na wabunge wengine wa Mkoa wa Manyara,
Kilimanjaro na Arusha.
Waziri wa Madini Angellah Kairuki akiwa katika picha ya pamoja na
wawakilishi wa Vyama vya Wachimbaji madini.
|
Na Ahmed Mahmoud
Waziri wa Madini Angellah Kairuki
amesema kuanzia sasa Serikali itaanza kutoa Leseni za madini biashara ya madini
kwa masharti magumu huku ikimtaka kila mwombaji kutoa taarifa za mauzo ya uzalishaji,
usafirishaji pamoja na mnyororo mzima wa biashara ya madini ikiwemo fedha
zinazoingia nchini kutokana na biashara hiyo.
Pia, ameiagiza Tume ya Madini
kuchukua hatua stahiki kwa kuhakikisha kila jambo katika mnyororo huo linasimamiwa
kikamilifu na kuongeza kuwa, yeye kama waziri mwenye dhamana atahakikisha
anafuatilia kila hatua itakayochukuliwa
na tume hiyo.
“Tume ichukue hatua. Nitakuwa na
ninyi. Msiache hata mmoja atakayekwenda kinyume na haya. Nilifanya hivyo katika
Sekta ya Utumishi wa Umma hata huku kwenye sekta ya madini, sitashindwa kufanya
hivyo,” alisisitiza Waziri Kairuki.
Waziri kairuki aliyasema hayo
jana tarehe 3 Agosti, Wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara wakati akipokea
taarifa ya Kamati Maalum iliyoundwa kuchunguza mnyororo wa madini ya vito
nchini.
Kamati hiyo ilifanya kazi yake
kwa muda wa siku 30 kuanzia tarehe 26
Aprili, 2018 kwa jukumu la
kuchunguza mnyororo wa madini ya
vito kuanzia kuzalisha hadi usafirishaji
nje ya nchi pamoja na kubaini sababu za utoroshaji wa madini na kupendekeza
hatua za kuchukuliwa ili kuzuia utoroshaji.
Pia, aliiagiza tume ya madini
kuanzia tarehe 4 Agosti, kuhakikisha inapata taarifa za uzalishaji za migodi
yote inayozalisha huku akitaka migodi husika ieleze mahali inakouzia madini
yao, anayeuziwa madini hayo na kuongeza kuwa, zoezi husika linawajumuisha pia dealers.
Waziri Kairuki alisema, wizara
yake imeamua kusimamia suala husika ikiwa ni jitihada za kuunga mkono juhudi
zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli za
kuhakikisha kuwa rasilimali madini zinawanufaisha watanzania wote.
“ Lazima watanzania tutambue kuwa
madini haya yanamilikiwa na watanzania wote. Tunatakiwa kuyalinda kwa ajii ya
maendeleo yetu na kwa manufaa ya vizazi vijavyo,” alisema Kairuki.
Akizungumzia biashara ya madini ya
tanzanite katika ukuta unaozunguka migodi ya tanzanite mirerani, alisema hakuna
serikali inayotaka watu wake wasifanye biashara, hivyo, lengo la ukuta huo ni
kuhakikisha kwamba inadhibiti utoroshaji wa madini na kuweka mfumo mzuri ambao
utawezesha madini hayo kuzinufaisha pande zote.
Alisema tayari wizara imeandaa
Kanuni za Mirerani (Mirerani Contolled Area) ambazo hivi sasa zinafanyiwa
maboresho baada ya kuwepo changamoto
kadhaa katika utekelezaji wake.
Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki
alisema serikali imebaini baadhi ya
wenye leseni za ‘broker’ kukaribisha wageni kutoka nje kufanya biashara hiyo
kinyume na taratibu na hatimaye
kusafirisha madini hayo, hivyo, aliwataka wote wanaofanya hivyo kuacha mara
moja na kuwataka watanzania wote wenye taarifa kuhusu suala hilo kutoa taarifa katika mamlaka zinazohusika.
“Kamati hii imefanya uzalendo na
imefanya kazi kubwa sana. Nimeipokea taarifa ya kamati lakini natamani
wangenitajia majina ya watoroshaji. Nilitamani sana kuona majina lakini naamini
itaniuma sikio,” alisisitiza Waziri Kairuki.
Pia, aliongeza kuwa serikali
itazifuta leseni za uchimbaji madini kwa
wale wote ambao wameshindwa kuyaendeleza maeneo yao na kupewa wengine wenye nia
ya dhati ya kuendeleza shughuli za uchimbaji madini nchini.
Akizungumzia mkakati wa serikali
katika kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani nchini, alisema kuwa serikali
inaendelea kukiimarisha kituo cha TGC kilichopo jijini Arusha, kwa kuongeza
wataalam katika masuala ya ukataji na unga’rishaji wa madini ya vito.
“Tayari tumepata walimu 7 kutoka nchini India, lakini bado
tunafuatilia wengine kutoka nchini Thailand,”alisema Kairuki.
Akiwasilisha taarifa ya Kamati kwa niaba ya Mwenyekiti wa
Kamati hiyo, Mratibu wa Kituo cha Jimolojia
Tanzania (TGC), Eric Mpesa alisema Kamati husika ilipata fursa ya kutembelea
mgodi wa Mundarara mpaka wa Namanga, Uwanja wa ndege wa KIA, Machimbo ya
Tanzanite Mirerani, TGC, Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Morogoro na Machimbo ya
Epanko, Morogoro
Akiwasilisha mapendekezo ya
kamati husika Mpesa alisema kuwa, kamati inapendekeza Serikali kutengeneza
mpango wa makazi katika eneo lililozungushiwa ukuta wa Mirerani ikizingatia
uwepo wa eneo la uchimbaji, biashara, uanzishwaji wa kituo cha One Stop Centre, huduma za kijamii,
maegesho ya vyombo vya usafiri, maeneo ya starehe na maeneo ya utalii.
Pia, alisema serikali ihakikishe
kuweka mfumo wa ulinzi katika eneo lililozungushiwa ukuta na pia ilishauri
serikali kuongeza wataalam wa Wizara katika maeneo ya migodi ili kurahisisha
ufanyaji biashara na kuwezesha kuzuia utoroshaji wa madini ya vito.
Pendekezo lingine ni serikali
kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata teknolojia za kisasa pamoja na tafiti za
kijiolojia kufanywa na watalaam kutoka
Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kwa malipo ya gharama
nafuu yatakayolipwa baada ya uzalishaji
kupatikana.
Pia, Kamati ilipendekeza
seriakali kuishawishi mifuko ya jamii isaidie wadau kuanzisha benki ya Madini itakayowapa
wachimbaji na wafanyabiashara mikopo yenye masharti nafuu.
Akizungumzia mcchango wa sekta ya
madini, alisema sekta hiyo inachangia fedha za kigeni cha kiasi cha wastani wa
dola za Marekani milioni 27.8 kwa mwaka isipokuwa almasi na kati ya hizo,
asilimia 27.8 ni madini yaliyosanifiwa na kunga’rishwa na asilimia 71.3 ni
madini ghafi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa
Manyara Alexander Mnyeti alisema kwa muda mrefu serikali imekuwa
ikichazewa kwa wadau katika migodi kutokulipa kodi stahiki za serikali.
Aliishauri wizara kufuta leseni
za wale wote walioohodhi maeneo yao bila kuyafanyia kazi ili kuwezesha leseni
husika kutumiwa na wengine wenye nia ya kuendeleza sekta ya madini.
Kuhusu suala la mikataba
ya ajira katika migodi hiyo aliishauri serikali na wadau kukaa pamoja na
kujadili suala husika na kulitafutia ufumbuzi.
Kamati iliyoandaa taarifa husika
ilikuwa na wajumbe 13 ikiongozwa na Mwenyekiti Sammy Mollel, Makamu Mwenyekiti
Hamis Kim, Katibu Adam Rashid pamoja na wajumbe 10 na Sekretarieti.
Wajumbe wa Kamati hiyo walitoka TAMIDA,
MAREMA, AREMA, RUVREMA, TAWOMA, BROKER pamoja na wajumbe kutoka Wizara ya
Madini na TGC.
Xxxxxx xxxxxxx xxxxxx xxxxxx xxxxxx
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni