Na Ahmed Mahmoud
Serikali imeahidi kuendelea kuziwezesha kifedha taasisi
mbalimbali zinazojihusisha na utafiti vikiwemo vyuo vikuu ili kuleta
tija kwa taifa kufikia uchumi wa kati
Akifungua Mkutano wa nne wa jumuia ya watafiti kutoka nchi
za Afrika Mashariki (EARIMA), unaofanyika jijini Arusha,Mkuu wa wilaya
ya Arumeru ,Jerry Muro akimwakilisha mkuu wa mkoa wa Arusha,amesema kuwa
serikali itaendelea kugharamia tafiti hizo ili kuwawezesha kuwafikia
wakulima na wafugaji waweze kukua kiuchumi.
Amewaomba watafiti hao kuelekeza nguvu zao katika tafiti
zinazofikika kwa jamii katika ukanda wa Afrika Mashariki kuhakikisha
tafiti zao zinalinufaisha taifa na wananchi wake katika kushiriki
shughuli za maendeleo
"Wataalamu na wabobezi wa tafiti mbalimbali mtusaidie
kuzifanya tafiti hizi kuleta tija ili kulifikisha taifa katika uchumi wa
kati"Amesema Muro
Amewataka watafiti hao kutoka nchi za Afrika Mashariki
kuunganisha nguvu ya kutafuta njia zitakazosaidia tafiti zinazofanyika
katika nchi hizo ziweze kwenda kwenye utekelezaji, hususani zile
zinazolenga kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa Mataifa hayo.
Naye Mwenyekiti wa jumuiya ya watafiti wa Nchi za Afrika Mashariki (EARIMA), upande wa Tanzania Dk. Alfred Sebahene, amesema mkutano huo umekuja baada ya kuwa tafiti nyingi zinazofanywa bado hazijaleta tija ya kuchangia uchumi wa nchi hizo hususani katika kutatua matatizo yaliyopo kwenye sekta za kilimo na Mifugo.
Amesema mkutano huo utajadili na kutoka
na mapendekezo yatakayosaidia tafiti zinazofanywa ziweze kwenda kutatua
changamoto zinazoikabili jamii ya mataifa hayo.
Amesema tafiti nyingi katika nchi
mbalimbali za Afrika Mashariki zinafanana ila changamoto kubwa ni
kutokana na mazingira yaliopo na hivyo mkutano huo utasaidia
kubadilishana uzoefu .
Kwa upande wake mkuu wa sekretarieti ya
EARIMA ambaye ni mhadhiri mwandamizi wa chuo kikuu cha Dar es salaam Dk.
Edwinus Lyaya amesema watafiti wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya
bajeti ya kufikisha tafiti zao kwa jamii.
Amesema mkutano huo unalenga kusimamia
utafiti na ugunduzi na kuhimiza tafiti za wataalamu ziweze kutoka kwenye
makablasha na kuwafikia wananchi.
"Tunajadiliana ili kuzitoa tafiti kwenye
maandishi na kufikia kwenye vitendo ili tafiti hizo ziweze kuzaa matunda
kwa jamii" Amesema
Mmoja wa Watafiti kutoka Chuo kikuu cha
Nelson Mandela Prof.Charlea Lugomela alisema chuo chao kimeshaanza
kutoa tafiti mbalimbali zenye matumaini kwa Wakulima na Wafugaji.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni