Moshi. Upande wa mashtaka, umewasilisha mahakamani maelezo ya namna mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Scolastica iliyopo mji wa Himo, Humpherey Makundi alivyouawa.
Katika maelezo hayo, mshtakiwa wa pili, Edward Shayo anadaiwa kukataa wazo la kumpeleka mwanafunzi huyo hospitali baada ya kuzimia kwa kipigo badala yake, aliagiza atupwe Mto Ghona.
Maelezo hayo yalisomwa jana mbele ya Jaji Haruna Songoro wa Mahakama Kuu na wakili wa Serikali mkuu, Joseph Pande wakati wa usikilizwaji wa awali baada ya washtakiwa kukana mashtaka.
Katika kesi hiyo, Pande anasaidiana na wakili mwandamizi wa Serikali, Abdallah Chavulla huku upande wa utetezi ukiwakilishwa na mawakili Elikunda Kipoko na Gwakisa Sambo.
Kesi hiyo inayovuta hisia za wakazi wengi wa ndani na nje ya mkoa wa Kilimanjaro, inamkabili Shayo ambaye ni mmiliki wa shule hiyo, mwalimu wa nidhamu, Labani Nabiswa na mlinzi, Hamis Chacha.
Mwanafunzi huyo alitoweka shuleni Novemba 6, 2017 na kubainika ameuawa baada ya mwili wa mtu aliyedaiwa na polisi wa kituo cha Himo kuwa ni mtu mzima mwenye ndevu, kufukuliwa kwa amri ya Mahakama.
Mwili wa mtoto huyo uliokotwa Novemba 10 katika Mto Ghona mita 300 kutoka shuleni hapo na polisi waliuchukua mwili huo na kuupeleka Hospitali ya Mawenzi na kuzikwa kwa madai haukutambuliwa.
Akisoma maelezo ya namna kosa hilo lilivyotendeka, Pande alidai Novemba 6, 2017 usiku, mshtakiwa wa kwanza (Chacha) alisikia kishindo cha mtu akiruka ukuta wa shule kwa nje.
Alimkimbiza wakati huo yeye (Chacha) akiwa na panga mkononi na alipomfikia alimpiga kwa ubapa na alianguka chini, baada ya kuanguka aliendelea kumshambulia hadi akapoteza fahamu.
Baada ya kuona marehemu kapoteza fahamu, alimpigia simu Shayo na Nabiswa ambao walifika eneo la tukio na lilitolewa wazo la kumpeleka hospitali lakini Shayo anadaiwa kukataa.
Badala yake, inadaiwa mmiliki huyo wa shule aliwaagiza Chacha na Nabiswa waubebe mwili huo na kuutupa Mto Ghona ambako washtakiwa hao wawili walitekeleza agizo hilo na kumtupa mtoni.
Pande alidai katika maelezo hayo kuwa wakati Nabiswa akijua kilichokuwa kimetendeka, alirudi shuleni na kuitisha mkusanyiko wa wanafunzi wote (roll call) na kuita mmoja mmoja.
Hata hivyo, katika mkusanyiko huo wa wanafunzi lilipoitwa jina la Humphrey Makundi ilisikika sauti iliyoitikia lakini mwanafunzi huyo hakuonekana hata kwenye mabweni ya wanafunzi usiku huo.
Kwa mujibu wa maelezo hayo, Novemba 8, baba mzazi wa mtoto huyo, Jackson Makundi alijulishwa juu ya kutoweka kwa mwanaye na Novemba 10, 2017 taarifa ikatolewa Kituo cha Polisi Himo.
Pande alidai siku hiyo hiyo, kulipatikana taarifa ya kuonekana kwa mwili ukielea katika Mto Ghona ambako polisi waliuopoa na kuupeleka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kilimanjaro, Mawenzi.
Kutokana na kwamba mwili huo ulishaanza kuoza na ulikuwa haujatambuliwa, ulizikwa siku iliyofuata ya Novemba 11 na Manispaa ya Moshi katika makaburi ya Karanga yaliyopo manispaa hiyo.
Polisi waliendelea na uchunguzi na Novemba 17, 2017 ofisi ya mwanasheria mkuu wa Serikali (AG), iliwasilisha ombi mahakamani la kufukuliwa mwili huo ili ufanyiwe uchunguzi. Mahakama ilitoa kibali cha kufukuliwa kwa mwili huo na ulipofukuliwa, baba mzazi aliweza kuutambua kuwa ni wa mwanaye na Novemba 19, 2017 ukafanyiwa uchunguzi na madaktari.
Pande aliieleza Mahakama kuwa, katika uchunguzi wa madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC waligundua kuwa kifo cha mwanafunzi huyo kilitokana na majeraha aliyoyapata kichwani.
Pia, katika uchunguzi huo zilichukuliwa sampuli za damu na ute kutoka kwa marehemu kwa ajili ya vipimo vya Vinasaba (DNA), ambavyo vilioana na sampuli zilizochukuliwa kwa wazazi wa marehemu.
Nini kilifuata?
Baada ya uchunguzi huo, washtakiwa hao walikamatwa na mshtakiwa wa kwanza (Chacha), anadaiwa kukiri kosa hilo katika maelezo yake aliyoandika polisi na kwa mlinzi wa amani.
Pande alieleza kuwa mbali na kukiri kosa hilo, lakini alidai mshtakiwa huyo alienda mbali zaidi na kuwapeleka polisi hadi eneo alipokuwa amehifadhi panga alilotumia katika mauaji hayo.
Baada ya kukamilika kwa usomwaji wa maelezo hayo ya kosa, Jaji Songoro aliwataka washtakiwa kupitia kwa mawakili wao kueleza mambo ambayo hayabishaniwi na yanayobishaniwa.
Akizungumza kwa niaba ya washtakiwa, wakili Kipoko aliiambia Mahakama kuwa wateja wao hawapingi majina yao na kwamba ni kweli wameshtakiwa kwa kosa la mauaji ya kukusudia.
Hata hivyo, alieleza kuwa washtakiwa hao wanakana ukweli (facts) uliomo katika maelezo hayo pamoja na mtiririko wake wote na kwamba wanatambua ni jukumu la Jamhuri kuthibitisha hayo.
Baada ya kukamilika kwa hatua hiyo, Jaji Songoro aliutaka upande wa mashtaka kueleza idadi ya mashahidi watakaowaita kuthibitisha shtaka hilo ambalo ilielezwa kuwa watakuwa 34.
Mashahidi hao ni pamoja na baba wa marehemu, Jackson Makundi, maofisa wa polisi waliopeleleza shauri hilo, mtaalamu wa DNA na madaktari waliofanyia uchunguzi mwili huo. Pia, Pande aliijulisha Mahakama kuwa wanatarajia kuwasilisha vielelezo vya nyaraka 15 yakiwamo maelezo ya kukiri kosa ya mshtakiwa Chacha akiwa polisi na kwa mlinzi wa amani.
Mbali na nyaraka hizo, lakini watawasilisha pia taarifa ya mawasiliano ya simu kutoka kampuni ya Vodacom, inayodaiwa kuonyesha washtakiwa waliwasiliana muda, saa na siku ya mauaji.
Mbali na vielelezo hivyo, upande huo wa mashtaka uliieleza Mahakama kuwa utawasilisha vielelezo halisi (physical or real) ambavyo ni simu saba, panga moja na nguo za marehemu.
Kwa upande wa mawakili wa utetezi, wao waliiambia mahakama kuwa orodha ya mashahidi wao pamoja na vielelezo watakavyovitumia, wataviwasilisha kabla ya washtakiwa kuanza kujitetea.
Kabla ya kuahirishwa kesi hiyo hadi kikao kijacho kitakachopangwa na Mahakama, Kipoko alimuomba Jaji Songoro kama itampendeza, aipangie kesi hiyo tarehe ya karibu ya kuanza kuisikiliza.
Wakati akiahirisha kesi hiyo, Jaji Songoro alisema kesi hiyo itaenda hatua ya tatu ya usikilizwaji kamili katika kikao kijacho kitakachopangwa na Mahakama na washtakiwa wataendelea kubaki mahabusu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni