TAARIFA KUHUSU KUANZA KWA VIKAO VYA KAMATI ZA KUDUMU ZA BUNGE JIJINI DODOMA

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
BUNGE LA TANZANIA

 
Simu: +255 026 23222761-5
Fax No. +255 026 2322624
E-mail:  cna@bunge.go.tz


 
                     Ofisi ya Bunge,
                S.L.P. 941,
        DODOMA





TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Kamati za Bunge zitakutana Jumatatu tarehe 20 hadi 31 Agosti 2018, Jijini Dodoma kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Kumi na Mbili wa Bunge uliopangwa kuanza tarehe 4 Septemba 2018. Spika wa Bunge Mheshimiwa Job Ndugai (Mb), ameziita Kamati hizo kuanza shughuli zake tarehe hiyo kwa mujibu wa Kanuni ya 117 ya Kanuni za Kudumu za Bunge. 
Shughuli zilizopangwa kutekelezwa na Kamati ni kama ifuatavyo:-
  1. Uchambuzi wa Miswada ya Sheria

Miswada Mitano (5) ya Sheria inatarajiwa kujadiliwa na Kamati nne (4) zilizopelekewa Miswada hiyo kwa mujibu wa Kanuni ya 84(1).  Kamati na Miswada hiyo ni kama ifuatayo:-      
  1. Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa itachambua na kujadili ‘Muswada wa Sheria ya Kulitangaza Jiji la Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi wa Mwaka 2018’ [The Dodoma Capital City (Declaration) Bill, 2018];

  1. Kamati ya Katiba na Sheria itachambua na kujadili miswada miwili ambayo ni ‘Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 2) wa Mwaka 2018’ [The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (No. 2) Bill, 2018]; na ‘Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) wa Mwaka 2018’ [The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (No. 3) Bill, 2018];

  • Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii itachambua na kujadili ‘Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalam ya Walimu Tanzania wa Mwaka 2018’ [The Teachers’ Professional Board Bill, 2018]; na
  1. Kamati ya Bajeti itachambua na Kujadili ‘Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa Mwaka 2018’ [The Public Private Partnership (Amendment) Bill, 2018].
  1. Kupokea Taarifa mbalimbali za Wizara/Taasisi

Kamati tisa (9) za sekta, Kamati ya Bajeti na Kamati ya Masuala ya UKIMWI zitachambua Taarifa za Taasisi/ Wizara za Serikali kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali kwa mujibu wa Kifungu cha 7(1), kifungu cha 7(2) (i) (ii) (iii) na (iv) na Kifungu cha 9(a) vya Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Bunge.
  1. Uchambuzi wa Taarifa ya CAG

Kamati zinazosimamia matumizi ya fedha za umma ambazo ni
Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) zitachambua Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka unaoishia tarehe 30 Juni, 2017.
  1. Uchambuzi wa Sheria Ndogo

Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo itachambua Sheria Ndogo 121 zilizowasilishwa Bungeni tarehe 9 Aprili, 2018, wakati wa Mkutano wa Kumi na Moja wa Bunge. Madhumuni ni kutekeleza majukumu yake yalioainishwa katika Kifungu cha 11 cha Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Bunge.
  1. Uchambuzi wa Taarifa za Uwekezaji wa Mitaji ya umma
Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) itachambua Taarifa ya Uwekezaji wa taasisi/mashirika kumi na tatu (13) kwa mujibu wa Kifungu cha 12 cha Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Bunge.
Ratiba zote za Shughuli za Kamati za Bunge pamoja na Miswada itakayoshughulikiwa na Kamati katika kipindi hiki vinapatikana katika Tovuti ya Bunge ambayo ni www.parliament.go.tz
Imetolewa na:          Kitengo cha Habari, Elimu kwa Umma na Mawasiliano
Ofisi ya Bunge
DODOMA
17 Agosti, 2018.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni