Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dkt. Albina Chuwa akizungumza alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu takwimu za afya katika Mkutano Mkuu wa Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya Jijini Dodoma. Kutoka kulia ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), anayeshughulikia Sekta ya Afya, Dkt. Zainabu Chaula, na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Mpoki Ulisubisya. Kauli mbiu ya mkutano huo ni; “Uboreshaji wa Mazingira ya Kutolea Huduma za Afya ni Msingi wa Wananchi Kuelelekea Tanzania ya Viwanda na Uchumi wa Kati”
Baadhi ya Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya waliohudhuria katika Mkutano Mkuu wa Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya uliofanyika Jijini Dodoma. Kauli mbiu ya mkutano huo ni; “Uboreshaji wa Mazingira ya Kutolea Huduma za Afya ni Msingi wa Wananchi Kuelelekea Tanzania ya Viwanda na Uchumi wa Kati”.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema njia bora ya kukabiliana na changamoto ya ukusanyaji wa Takwimu za kiutendaji wa kila siku katika wizara, Idara na taasisi za umma ni kuwa na mfumo wa uratibu wa takwimu hizo chini ya kituo kimoja cha uratibu.
Mkurugenzi Mkuu wa NBS Dk. Albina Chuwa ameuambia mkutano wa Waganga wa Mikoa na Waganga Wafawidhi uliofanyika Dodoma hivi karibuni kuwa katika kufanya hivyo ushirikiano kati ya wadau ni suala la msingi ili kuboresha takwimu za afya.
“Lengo letu ni kuwa na kituo kimoja cha takwimu za afya ambacho takwimu zote za afya zinapatikana hapo kuanzia vifo na uzazi, idadi ya madaktari na watumishi wa afya, elimu yao, uzoefu wao na hata madawa yalipo hospitalini na iwe ni rahisi mtu kuzipata”Dk. Chuwa alifafanua.
Alifafanua kuwa kufanya hivyo kutawezesha kufanya uchambuzi wa kina wa viashiria mbalimbali kwa kulinganisha viashiria husika na upatikanaji, utayari, ubora matumizi ya huduma zitolewazo.
Mkurugenzi Mkuu huyo alibainisha kuwa kati ya vyanzo vingi vya takwimu za afya kimojwapo ni takwimu za kiutawala ambazo kama ilivyo katika sekta nyingine ukusanyaji wake unahitaji maboresho makubwa.
“Uboreshaji wa takwimu za kiutendaji (kiutawala) wa kila siku ikiwemo za sekta ya afya ni suala la kipaumbele kwa kuwa maamuzi mengi yanayohusu maendeleo yetu yanatumia takwimu hizi” Dk. Chuwa alisisitiza.
Katika mnasaba huo, Dk. Chuwa alibainisha kuwa NBS jukumu lake kubwa ni kuratibu na kutoa miongozo wakati watakwimu wa wizara na taasisi ambao ndio wenye jukumu la kukusanya takwimu za wizara na taasisi zao.
Alivitaja vyanzo vya Takwimu za afya kuwa ni pamoja na Sensa ya Watu na Makazi, Tafiti za Kitaifa katika Jamii, Tafiti za Tathmini ya Utoaji Huduma katika Vituo vya Afya na Usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu.
Vyanzo vingine ni Mifumo ya Ugawaji na Usambazaji Dawa, Vitendanishi na Vifaa Tiba, Mifumo ya Bima ya Afya, Ukusanyaji Takwimu za Ufuatiliaji Hali za Afya na Ugonjwa, Tathmini za Utekelezaji wa Afua za Afya, Ufuatiliaji Shirikishi wa Utekelezaji wa Afua za Afya,Mfumo wa Ukusanyaji wa Takwimu katika Jamii kupitia Serikali za Vijiji na Tafiti za Vyuo na Taasisi Mbalimbali.
“Kwa kawaida wizara zina vitengo vya ufuatuliaji na ukusanyaji Takwimu (monitoring and evalution) ndio vinavyopaswa kutekeleza majukumu hayo sisi NBS ni kuongoza na kufuatilia kama ukusanyaji unafuata miongozo iliyowekwa”alisisitiza.
Wakati huo huo Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Mpoki Ulisubisya alisifu ushirikiano uliopo kati ya Wizara yake na Ofisi ya Taifa ya Takwimu ambao umewezesha kufanya kazi kwa pamoja na kwa ufanisi mkubwa.
“Nimefurahi kwa ushirikiano wetu na NBS ambapo katika ushirikiano huo tunatumia njia sahihi za kuthibitisha (verify) takwimu zetu na hiyo ndio njia sahihi ya kujenga jamii inayomiliki takwimu zake” Alisema Katibu Mkuu huyo.
Alimpongeza Dk. Chuwa kwa kukubali kushiriki katika mkutano huo ambapo alizungumzia kwa kina masuala ya Takwimu za afya, namna NBS inavyoshiriki katika kusimamia takwimu za sekta ya afya na mchango wa NBS katika kuimarisha ukusanyaji wa takwimu za afya nchini. Alieleza pia sehemu ya maudhui ya Sheria ya Takwimu Na. 9 ya Mwaka 2015.
Kwa upande wao washiriki walipendekeza NBS ichapishe taarifa ya matokeo ya tafiti mbalimbali za afya inazozifanya hadi katika ngazi ya wilaya badala ya kuishia ngazi ya taifa na mkoa tu.
“Tunazihitaji sana taarifa za matokeo ya tafiti zenu. Kule kuna viongozi na wataalamu ambao wanapaswa kuelewa yaliyojiri katika tafiti hizo na kuyafanyia kazi matokeo yake kwa ajili ya kupanga mipango mbali mbali ya maendeleo”alisema mmoja wa washiriki.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni