Dar es Salaam. Kutokana na moto ulioteketeza magari katika kituo cha forodha Rusumo, kampuni ya usafirishaji ya Bakhresa (S.S. B Transport) imepata hasara ya zaidi ya Sh1.5 bilioni.
Msemaji wa kampuni za Azam, Hussein Sufian akizungumza na Mwananchi jana, alisema malori manne ya kampuni hiyo yameteketea kabisa na moja limeungua kiasi.
Alisema malori hayo yalikuwa yamebeba pumba za ngano zilizokuwa zikisafirishwa kutoka Rwanda kwenda Bandari ya Dar es Salaam kabla ya kupelekwa nje ya nchi. “Moto uliozuka Rusumo umetusababishia hasara ya Dola 700,000 za Marekani (zaidi ya Sh1.5 bilioni) zinazojumuisha malori na mzigo uliokuwamo. Jambo jema ni kwamba kila lori lilikuwa limekatiwa comprehensive insurance (bima kubwa ya gari),” alisema Sufian. Malori hayo yenye thamani ya Dola 150,000 za Marekani kila moja, alisema yalikuwa mpakani yakisubiri kupata vibali vya kuendelea na safari.
Juzi, magari saba yaliteketea kwa moto katika kituo hicho kilichopo wilayani Ngara mkoani Kagera ulipo mpaka kati ya Tanzania na Rwanda baada ya lori lililobeba dizeli kuligonga jingine kutokana na hitilafu ya mfumo wa breki.
Katika tukio hilo, dereva mmoja alifariki dunia na utingo alijeruhiwa baada ya kuruka kutoka ndani ya gari ili kujiokoa. Moto huo ulizimwa na helikopta kutoka Rwanda kwa kushirikiana na gari la zimamoto kutoka wilayani Karagwe.
Mkuu wa Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Ngara, Edward Bishanga alisema kituo cha zimamoto kinajengwa wilayani humo na sasa wanasubiri gari la zimamoto na vifaa kutoka serikalini.
Alishauri ili kudhibiti ajali ni vyema vituo vya maegesho vikajengwa maeneo tofauti na yenye miteremko mikali ya Milima K9, Kumuyange, Machinjioni ya Rusumo na Kobero kuingia Burundi.
Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Michael Mtenjele alisema yamekuwapo matukio ya ajali kutokana na magari kupita yakiwa na mizigo mizito na madereva kukumbana na changamoto ya kutozijua barabara zenye miteremko na milima mikali.
Barabara zina mashimo kuanzia Nyakanazi wilayani Biharamulo mpaka eneo la Rusumo.
Nyongeza na Shaaban Ndyamukama
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni