USHIRIKA SI SEHEMU YA ‘KUPIGA DILI’-MAJALIWA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa vyama ushirika wawatumikie wanachama wao ipasavyo na wasidhani hiyo ni sehemu ya ‘kupiga dili’. 
Amesema Serikali itawachukulia hatua kali viongozi wote wa vyama vya ushirika watakaobainika kuhujumu wanaushirika, hivyo amewataka wafanye kazi kwa uaminifu.
Aliyasema hayo jana jioni (Alhamisi, Agosti 16, 2018) wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Chomachankola. 
Hata hivyo, Waziri Mkuu aliwataka viongozi wa chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Tabora cha Igembensabo cha kuhakikisha wanasaidia wakulima katika kujiunga na huduma ya bima ya afya.
Alisema tayari Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NIHF) umeanzisha huduma kwa ajili ya wanachama wa vyama vya ushirika ambao wanatakiwa kuchangia sh. 75,000 kwa mwaka.
Waziri Mkuu alisema wanachama hao wakijiunga na NIHF watapata fursa ya kutibiwa bure wao, wenza wao na watoto wanne kwenye hospitali mbalimbali nchini ikiwemo ya Muhimbili.
Pia aliwahamasisha wananchi wa wilaya hiyo wajiunge na Mfuko wa Afya wa Jamii (CHF) ili waweze kuwa na uhakika wa kupata matibabu wao pamoja na familia zao kwenye hospitali zilizoko ndani ya mkoa Tabora bure. 
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wakulima wa zao la pamba wajiandae kwa kupanua mashamba yao katika msimu ujao wa kilimo kutokana na uwepo ya masoko ya uhakika. 
Waziri Mkuu alisema kwa sasa kuna viwanda vingi vya kuchambua pamba ambavyo vimeanza uzalishaji na baadhi ya wamiliki wake wamelalamikia upungufu wa malighafi. 
Pia Waziri Mkuu aliwataka vijana waache tabia ya kukaa vijiweni na kucheza ‘pool’ badala yake wajishughulishe na kilimo cha zao la pamba ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuondokana na utegemezi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, AGOSTI 17, 2018.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni