SERIKALI KUWEKA MBINU ZA KISASA ULINZI MIRERANI

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Tumain Magesa akieleza jambo wakati wa mkutano wa hadhara kati ya Waziri
Mkurugenzi wa  kampuni ya TanzaniteOne Faisal Juma (kushoto) akiongozana na mmoja wa wafanyakazi ambaye aliwasilisha malalamiko yake kuhusu kampuni hiyo kwa Waziri wa Madini Angellah Kairuki wakati wa mkutano wa hadhara. Anayefuatilia ni mmoja wa viongozi katika kampuni hiyo  Hussein Gonga.


Mkurugenzi wa kampuni ya TanzaniteOne Faisal Juma (kulia) na mmoja wa viongozi katika kampuni hiyo Hussen Gonga (katikati) wakimsikiliza mmoja wa watumishi katika kampuni hiyo wakati akiwasilisha malalamiko yake kwa Waziri wa Madini Angellah Kairuki (hayupo pichani) wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika nje ya geti la kuingilia katika ukuta unaozunguka migodi ya tanzanite, mirerani.
Sehemu ya wananchi waliofika katika mkutano wa hadhara ambao ulijumuisha wamiliki wa migodi, wachimbaji, wauzaji, wanunuzi na wanaofanya shughuli mmbalimbali ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya tanzanite, Mireran wakimsikiliza Waziri wa Madini Angellah Kairuki, hayupo pichani.
Waziri wa Madini Angellah Kairuki akisisitiza jambo wakati akizungumza na  katika mkutano wa hadhara na wananchi wanaofanya shughuli zao ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya tanzanite, mirerani.  Wanaofuatilia mbele ni Mbunge wa Simanjiro James Ole Milya (kulia) na kushoto ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Tumain Magesa.



Waziri wa Madini Angellah kairuki (kushoto) akiteta jambo na Mbunge wa Simanjiro James Ole Milya wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika nje ya geti la kuingilia nda ni ya ukuta unaozunguka migodi ya tanzanite, mirerani. Mkutano huo uliwashirikisha wamiliki wa migodi, wachimbaji, wafanyabiashara na wanaofanya shughuli mbalimbali ndani ya ukuta huo.



Serikali imesema inajiandaa kuja na mbinu za kisasa zaidi za ukaguzi na ulinzi katika ukuta unaozunguka migodi ya Tanzanite, Mirerani  ili kudhibiti utoroshaji wa madini hayo yanayopatikana Wilayani Simanjiro Mkoa wa   Manyara.
Hayo  yalisemwa na Waziri wa Madini Angellah Kairuki  tarehe 2 Agosti, 2018 wakati wa mkutano wa hadhara ulishirikisha wamiliki wa migodi, wachimbaji, wauzaji na wote wanaofanya shughuli zao za ndani ya ukuta huo.
Alisema, mabadiliko ya ujenzi wa ukuta huo ni chanya ambayo yamelenga kukuza uchumi wa nchi kupitia sekta ya madini ili kuongeza mchango wa sekta husika katika pato la taifa.
Waziri Kairuki alieleza  ili shughuli za uuzaji na ununuzi ziweze kufanyika ndani ya eneo hilo, tayari Serikali imejenga sehemu maalum kwa ajili ya shughuli  hizo na kuongeza, “ baada ya kukamilika jengo hilo kutakuwa na sehemu kwa ajili ya Broker kufanyia shughuli zao hapo hapo ndani ya ukuta.”
Aliongeza, tayari Mkataba wa ujenzi wa Kituo cha kufanyia shughuli zote zinazohusu biashara ya madini ya tanzanite kwa ujumla (One Stop Center) umekwishakabidhiwa na ndani ya muda mfupi ujao, ujenzi wa jengo husika utaanza.
Akitoa ufafanuzi kuhusu taratibu za kuingia na kufanya shughuli za uchimbaji ndani ya ukuta, Waziri Kairuki alisema taratibu za ukaguzi zinalenga katika kudhibiti utoroshaji madini na hivyo kuwataka wadau wote kutoa ushirikiano wakati wa zoezi la ukaguzi katika ukuta huo na kuongeza kuwa, aina ya ukaguzi unaofanywa kwa sasa ni wa muda mpaka hapo taratibu maalum za ukaguzi zitakapokuwa tayari.
Akitoa ufafanuzi kuhusu wazawa wenye leseni za uuzaji kulipa ada kwa  kutumia Dola za Marekani, Waziri Kairuki alieleza kuwa, kwa kuwa Kanuni za eneo la Mirerani zimeandaliwa na Waziri mwenye dhamana na sekta, suala hilo litafanyiwa kazi ili kipengele husika kiweze kufanyiwa marekebisho na hivyo kuwawezesha kulipia kwa fedha za Tanzania. Pia, aliongeza kuwa, katika kipindi hiki ambacho mabadiliko hayo hayajafanyika, wahusika watalazimika kuendelea na utaratibu uliopo.
Ili kuongeza kasi ya shughuli ya uthamini wa madini hayo, waziri Kairuki alisema wizara yake itaongeza idadi ya wataalam kutoka mmoja hadi wanne ili kuongeza kasi ya kufanya shughuli husika.
Pia, Waziri Kairuki aliwataka wamiliki wa migodi kuhakikisha wanakuwa na mikataba ya wafanyakazi katika migodi yao na kuongeza kuwa, suala la maslahi ya watumishi ni jambo ambalo linapaswa kupewa kipaumbele na wadau wote katika sekta husika.
“Maslahi ya wafanyakazi yanatakiwa kuwa namba moja. Mimi ni Mbunge niliyechaguliwa kupitia umoja wa vyama vya wafanyakazi hivyo suala la maslahi ya wafanyakazi lazima nilisimamie kikamilifu,” alisisitiza Kairuki.
Akizungumzia suala la usafiri ndani ya ukuta, alisema zoezi husika litaendelea kama ilivyo sasa na kutumia fursa hiyo kukaribisha wawekezaji zaidi katika huduma ya kutoa  huduma ya usafiri ndani ya ukuta huo.
Pia, alitumia fursa hiyo kuwataka wadau wote katika eneo hilo kuwa waaminifu na kushirikiana na serikali na hususan ofisi ya Madini katika kutoa taarifa za utoroshaji madini hayo.
Mwisho aliwataka Maafisa Madini  kuendelea kutoa elimu ya Sheria ya Madini pamoja na taratibu zake pia, Mbunge wa eneo husika aendelee kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuwepo kwa ukuta huo ili kuwawezesha wadau wote kuwa na uelewa wa pamoja.
Kwa upande wake, Mbunge wa Simanjiro James Ole Milya, alisema alimweleza Waziri Kairuki kuwa kero kubwa katika eneo husika ni baina ya wamiliki wa migodi na wafanyakazi na hivyo kumtaka Waziri kuona namna ya kushughulikia suala hilo.
Pia, alipendekeza kuundwa kwa kamati mbili moja ikiwa ya wamiliki na wafanyakazi kwa lengo la kuondoa mvutano uliopo sasa kati ya pande mbili.





 




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni