FRED LOWASSA KUGOMBEA UBUNGE MONDULI KWA TIKETI YA CHADEMA


FED
Baada ya kuwepo kwa mashinikizo mbalimbali yakimtaka mtoto wa aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa awamu ya nne, Edward Lowassa kugombea Ubunge jimbo la Monduli Fred Lowassa, hatimaye ameweza kutimiza maagizo hayo kwa kuchukua fomu rasmi leo Agosti 09, 2018.
Fred Lowassa amechukua maamuzi hayo baada ya jimbo hilo kuwepo wazi kutokana na aliyekuwa Mbunge wa eneo hilo Julius Kalanga kujiuzulu mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu.
Mbali na Fred kuchukua fomu hiyo kutoka CHADEMA pia wamejitokeza wanachama wengine ndani ya chama hicho kuonesha nia ya kuomba ridhaa ya Jimbo hilo ambapo ni pamoja na Mwenyekiti Baraza la Wanawake wa CHADEMA mkoa Cecilia Ndosi, diwani viti maalum, Yona Laizer, Lobulu Kivuyo aliwahi kuwa mgombea katika uchaguzi mdogo uliopita Kata ya Muhita na Eric Ngwijo.
Akizungumza na EATV Katibu wa CHADEMA kanda ya Kaskazini ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Arusha, Aman Golugwa amesema wagombea hao wanatarajiwa kupigiwa kura za maoni katika kikao kitakachofanyika Agosti 12, 2018 siku ya Jumamosi.
“Kwa jimbo la Monduli hadi kufikia majira ya saa 10 jioni ambapo ndio ilikuwa mwisho wa kurudisha fomu, tulipata watia nia wanne. Kuhusu Fred Lowassa kesho tutatoa taarifa rasmi maana kuna vitu, tumekubaliana tuvifanye kidogo lakini naye ni miongoni mwa waliochukua na kurudisha fomu”, amesema Golugwa.
Jimbo la Monduli limekuwa wazi kuanzia usiku wa Julai 30, 2018 baada ya Mbunge aliyechaguliwa 2015 (CHADEMA), Julius Kalanga kujiunga na CCM kwa kile alichoeleza kuwa ni kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli na kudai kuwa ameondoka CHADEMA kwasababu ya siasa za chuki na uhasama.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni