Serikali imesema kuanzia septemba 5, mwaka huu visimbuzi vitaanza kuonesha channeli zote za ndani bila kutoza gharama yoyote kwa mtazamaji.
Akiwaeleza waandishi wa habari jana jijini Dar es salaam,
kuhusu yaliyozungumzwa katika kikao kati ya Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe na wadau na wamiliki
wa televisheni nchini, Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji
Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi amesema kuwa serikali imefikia
uamuzi huo baada ya visimbuzi vya AZAM, ZUKU na DSTV kutoonesha channeli
za ndani, kulingana na aina ya leseni zao.
“Ningependa watanzania wafahamu kwamba kuanzia septemba 5
mwaka huu, visimbuzi vya Ting, Starmedia, Continental na Digtek
vitaonesha takribani channeli 34 za ndani bure, ili kutoa fursa ya kila
mwananchi kuwa na haki ya kupata taarifa” alisema Dkt. Abbasi
Aidha, alielezea kuwa wadau hao na wamiliki wa televisheni
wameonesha kuridhishwa na hatua hiyo kwa vile Serikali imetengeneza
miundombinu itayoruhusu channeli zao kuonekana nchi nzima.
Dkt. Abbasi, alisisitiza kuwa “nchi imeandaa mfumo, ambao
unaweza kufanyakazi bila kutegemea kampuni kutoka nje ya nchi kwa ajili
ya kuonesha channeli za ndani au matangazo, kwa hivyo wadau au wamiliki
wa vyombo vya habari wasihofu kuhusu hilo”
Kikao kati ya Waziri Mwakyembe na wadau na wamiliki wa
televisheni nchini, kimefanyika kwa lengo la kuwa na majadiliano ya
pamoja baina serikali na wadau hao ili kupata muafaka kuhusu kutooneshwa
kwa chaneli za ndani katika visimbuzi vilivyokiuka masharti ya leseni
zao.
Aidha, kikao hicho pia kilihudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Injinia James Kilaba, pamoja na
wataalamu wake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni