WAZIRI MKUU AWATANGAZIA VITA MAFATAKI

NA TIGANYA VINCENT
RS TABORA
17 August 2018
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amewataka wanajamii wote katika maeneo wanayoishi kuwa walinzi wa wanafunzi wa kike ili kuwakinga na watu wazima na vijana wenye tabia ya kuwarubuni na kuwapa ujauzito.
Alisema watu wenye tabia mbaya wamekuwa wakiwarubuni na kuwakatisha ndoto zao na kuwata elimu kwa ajili ya maendeleo yao na Taifa kwa ujumla jambo ambalo sio la kulifumbia macho.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Igunga na Nzega wakati akizungumza na wananchi kwenye mikutano ya hadhara.
Alisema Serikali ya sasa haina huruma na mtu yoyote atakayekutwa  na mwanafunzi katika nyumba za kulala wageni au kwake na yule atakaye kutwa ameoa au kumpa mimba mwanafunzi.
“Ole wenu vijana wa kiume ambao mtakutwa mkiwa mmesimama na wanafunzi wa kike katika mazingira yasiyoeleweka na ole wake mtu atakayepatikana amempa ujauzito mwanafunzi au kuoa mwanafunzi atajuta” alisema.
Alisema ni lazima watoto hao wa kike walindwe kwa kuwa ndio watakaokuja kuwa miongoni mwao wabunge, wakuu wa wilaya, mawaziri na viongozi wa kada mbalimbali za baadae..
Waziri Mkuu aliwataka wanajamii kuhakikisha wanawafichua watu wenye tabia ya kuwavizia wanafunzi kwa ajili kuwaharibia maisha ili hatua kali dhidi yao ziweze kuchukuliwa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni