Mawakili wa Serikali kuwa na Chama chao-AG


IMG_4075[1]
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dk. Adelardus Kilangi akitoa mada kuhusu Nafasi na Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wakati  wa mkutano unaoendelea wa Mawakili wa Serikali waliokatika  utumishi wa umma. Pamoja na mambo mengine Dk. Kilangi amesema Mawakili wa Seriakali walio katika utumishi wa umma watakuwa na chama chao.
WIN_20180830_142142 (2) - Copy
Sehemu ya mawakili wa  serikali kutoka wizara mbalimbali, Idara na Taasisi zinazojitegema,  Wakala na Serikali za Mitaa ambao wapo Jijini Dodoma kwa mkutano wao wa siku mbili.
Na Mwandishi Maalum, Dodoma
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dk. Adelardus Kilangi amesema,  anakusudia  kuanzisha Chama cha Wanasheria walio  katika utumishi wa Umma.
Dk. Kilangi ameyaeleza hayo   wakati akiwasilisha mada kuhusu  Nafasi na Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa  Mawakili wa Serikali walio  katika utumishi wa umma wanaokutana  katika mkutano wao wa siku mbili  unaofanyika katika  ukumbi wa mikutano wa  Chuo cha Mipango Jijini   Dodoma.
Mawakili hao wa Serikali  wapatao mia tisa ( 900) wanatoka  Wizara mbalimbali,  Idara za Serikali, Taasisi na  Mashirika yanayojitegemea, Wakala na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Mkutano huo  ambao  ni wa pili kufanyikia ulifunguliwa na  Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali amebainisha kwamba, kuanzishwa kwa  Chama hicho ni kwa mujibu wa  Ibara ya 74 ya  Muswaada wa  Sheria ya  Marekebisho  Mbalimbali ( Na.2) 2018  inayoeleza kuwa , “ Mwanasheria Mkuu wa Serikali  anaweza  kuanzisha Chama cha Wanasheri katika Utumishi wa Umma”.
Amewaeleza  Mawakili  wa Serikali kwamba Chama hicho kitakuwa  kinakutana  mara moja kwa mwaka kwaajili ya  kujadili masuala mbalimbali ya kisheria ikiwamo  maendeleo ya taaluma hiyo.
Dk. Kilangi amesema, pamoja  na wanachama wa chama hicho kukutana mara moja kwa mwaka,  Waziri mwenye dhamana na  mambo ya sheria anaweza kuitisha mikutano ya wanasheria waliokatika utumishi wa umma kila anapoona kuna umuhimu wa kufanya hivyo.
Amefafanua zaidi kwa kusema, ripoti ya mikutano ya chama   hicho itawasilishwa kwa Waziri wa Katiba na Sheria na kwamba, Waziri atatunga  Kanuni kuhusu  usimamizi, uongozi, muundo na uendeshaji wa shughuli za chama.
Aidha Mwanasheria Mkuu wa Serikali  amesema kuanzishwa kwa  chama cha Mawakili  wa Serikali walio katika utumishi wa Umma hakutawanyima fursa  mawakili hao ya  kujiunga au kuwa wanachama wa  vyama  vingine vya kitaaluma kikiwamo  Tanganyika law Society ( TLS).
Akizungumzia  kuhusu kuanzishwa kwa   daftari la mawakili wa serikali,  Mwanasheria Mkuu amesema, daftari  hili litaanzishwa kwa mujibu  wa Ibara ya 74 ya  Muswaada wa Sheria ya Marekebisho mbalimbali ( Na. 2) 2018 unaotamka kwamba, “ Mwanasheria Mkuu wa Serikali ataanzisha Daftari la Mawakili wa Serikali ( Roll of State Attorneys)”.
Amesema daftari hilo likuwa na majina ya mawakili wa serikali kwa kuzingatia ukuu ( seniority ) miongoni mwao na kusisitiza kwamba, hatua hiyo haitaathiri sifa au hadhi  ambayo mtu alikuwa nayo kabla ya kuazishwa kwa  daftari  hilo.
Kuhusu mawakili hao  sasa kutambulika kama  wanasheria wa Serikali ( State Attonerys ) Mwanasheria Mkuu wa Serikali amelitolea ufafanuzi kwa kusema
Kila Afisa Sheria aliyeteuliwa au  kuajiriwa katika Wizara, Idara inayojitegemea, wakala au serikali za mitaa sasa anakuwa wakili wa serikali na kwa sababu hiyo yuko chini ya usimamizi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali isipokuwa  kwa Wanasheria wa Serikali ambao wapo chini ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na  Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.
“Hivyo Afisa huyo anachukuliwa kuwa anafanya kazi na kutekeleza majukumu na  mamlaka ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika Wizara zao , Idara zinazojitegemea, wakala wa serikali na Serikali za mitaa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ataweweza kutoa maelekezo ya jumla au maelekezo  mahsusi kwa  mawakili wa  serikali  walio katika utumishi wa umma kuhusu utekelezaji wa majukumu yao ya kisheria.
Akawahimiza wanasheria hao kila mmoja wao kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa bidii, maarifa na ujuzi wake huku akitanguliza maslahi ya taifa lake katika  kila jambo analokishughulikia.
Akahadharisha kwamba,  hatasita kuchukua hatua dhidi ya mtumishi yeyote atakaye kiuka maadili ya  Mawakili katika utumishi wake.
Awali akifungua  Mkutano huo Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa  Ibrahim Juma, amewataka  Mawakili wa Serikali  kutumia njia mbadala ya usuluhi katika baadhi  kesi za madai pale inapobidi   na kufikia usuluhishi nje ya Mahakama.
Jaji Mkuu amesema , ikiwa njia ya usuluhishi nje ya  mahakama  utafanyika, basi  utapunguza  muda wa undeshaji kwa kesi hizo ambazo nyingine huchukua hadi miaka kumi bila kufikia muafaka.
“Niwaombe wanasheria wa Serikali  katika kesi  nyingine za madai pale inapobidi wajaribu sana kulenga kufikia usuluhishi wa nje ya mahakama badala ya kuendesha kesi kwa miaka  hata kumi, kuanzia kesi inapoanza ngazi ya chini hadi kufikia Mahakama ya Rufani” amesema Jaji Mkuu na
Akasisitiza  kwamba, “ Kuna wakati wanasheria wa Serikali wanakiri kwa pembeni, kuwa kesi  wanayoendesha haina nafasi ya kushinda au hata wakishinda gharama hadi  kupata ushindi huyo  ni kubwa. Wanapambana tu kwa sababu Mkuu wa Idara au Kitengo amesema hivyo”.
Akasisitiza kwa kusema. “Hapa ndipo ipo haja ya kujenga Imani ya Mawakili hawa ( wa Serikali) na kuwaruhusu wapate usuluhisho wa mashauri nje ya  mahakama”
Akitoa takwimu za Kituo cha Usuluhishi ( Mediation Centre) cha Mahakama Kuu Dar es Salaam kwa mwaka  jana ( 2017) kinaonyesha kuwa jumla ya mashauri 41 yalisuluhishwa na kituo bila ya kufikishwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kusikilizwa na kati ya hizo, ni 10 tu zilikuwa za taasisi ya Umma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni