Mbunge wa Jimbo la Siha mkoani Kilimanjaro, Dk. Godwin Mollel (CCM), ameahidi kuongoza maandamano ya wananchi wa jimbo hilo kwenda katika mashamba yanayomilikiwa na serikali na kuyagawa ili wananchi wapate viwanja.
Vilevile, amemtaka Spika wa Bunge Job Ndugai, kumwandalia jeneza lake mapema endapo serikali itashindwa kutatua changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya makazi na matumizi ya wananchi wa Wilaya ya Siha.
Mbunge huyo alitoa kauli hiyo jana katika hafla ya kumpokea aliyekuwa Diwani wa Kata ya Ndumet, Jackson Rabo (Chadema), aliyejiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hafla hiyo ilifanyika katika Kijiji cha Matadi, ikihudhuriwa na Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Jonathan Mabihya, aliyekabidhi kadi kwa mwanachama mpya huyo wa chama tawala.
Dk. Mollel alisema wananchi wa Jimbo la Siha wanakabiliwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya makazi, ilhali serikali inamiliki mashamba makubwa yaliyopo jimboni huko na kwamba suala hilo tayari limeshafikishwa kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
"Lipo tatizo kubwa la ardhi katika jimbo langu," Dk. Mollel alisema," sasa nimeshaiandikia serikali barua ya kuomba kutupatia viwanja vichache katika mashamba wanayoyamiliki.
"Wakishindwa kufanya hivyo, mimi kama mbunge, najua vyombo vya usalama mpo hapa na mnasikia, nitaongoza maandamano ya wananchi kwenda katika mashamba ya serikali na kujikatia viwanja na Spika niandalie jeneza maana sitakubali."
Dk. Mollel alidai kuwa Kata za Ngarenairobi na Ndumet zina wakazi 38,000 wanaotumia ardhi ekari 500 na ndani ya jimbo hilo serikali inamiliki eneo la ekari zaidi ya 120,000, lakini wananchi wanashindwa kujenga nyumba za makazi kutokana na kukosa ardhi.
Alisema wananchi wa jimbo hilo wanataka kunufaika na ardhi yao kwa kujenga nyumba za makazi na kituo cha magari.
Katika hafla hiyo, Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro (Mabihya), alidai Rabo ameamua kujiunga na CCM kutokana na kutambua wananchi wanataka maendeleo na chama alichokuwa hakiwezi kuwaletea wananchi maendeleo.
Mabihya alisema hakuna sababu za kuendelea kung'ang'ania katika vyama visivyojali wananchi bali vipo kwa ajili ya maslahi ya watu wachache na badala yake amewataka kufanya uamuzi wa kuhamia katika chama kinachowaletea wananchi maendeleo.
Kuhusu changamoto ya upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya matumizi ya wananchi wa Jimbo la Siha, Mabihya alisema CCM ipo pamoja na wananchi na tayari wametoa taarifa kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kuhusu suala hilo.
Aliwataka viongozi wa kata na vijiji vilivyopo Ndumet na Ngarenairobi kuanza kuitisha vikao na kupanga maeneo watakayojenga huduma muhimu kama stendi na shule pindi serikali itakapotoa maeneo hayo.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni