NA. LUSUNGU HELELA-DODOMA
RAIS wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye Tamasha la Mwezi wa Urithi linalotambulika kama Urithi Festival, Celebrating Our Heritage litakalozinduliwa rasmi kitaifa katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma Septemba 15, 2018.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga amesema lengo la Tamasha hilo ni kuenzi, kudumisha, kuburudisha na kujifunza masuala muhimu yanayohusu Urithi wa Mtanzania hususani tamaduni zetu, historia, malikale na maliasili.
Aidha, Amesema kwa kutambua hazina kubwa ya malikale na utamaduni wa makabila zaidi ya 128 yaliyopo nchini, tamasha hilo litaongeza wigo wa mazao ya utalii kwa kukuza utalii wa utamaduni wa malikale hatua ambayo itaongeza ushindani wa Tanzania kama kituo bora cha utalii kwenye masoko mbalimbali duniani.
Ameongeza kuwa Urithi Festival itasadia kukuza utalii wa ndani kwa kuongeza muda wa watalii wa kimataifa kukaa nchini kwa vile Tamasha hilo lifanyika katika kipindi ambacho watalii wengi wanatembelea Tanzania.
Naibu Waziri huyo amesema kutokana na watalii kuongeza muda wa kukaa nchini kutaleta faida kwa wananchi na uchumi wa nchi kwa ujumla
Aidha, Naibu Waziri huyo ametaja mikoa sita pamoja na tarehe zake ambayo Tamasha hilo linafanyika kitaifa wa upande wa jiji la Dodoma tamasha hilo litafanyika Septemba 15 hadi tarehe 22 na kwa Zanziba litafanyika Septemba 23 hadi 29.
Pia, kwa upande wa Dar es Salaa na Mwanza tamasha hilo litafanyika Septemba 29 hadi Oktoba 6.
Aidha, kwa upande wa Wilayani Karatu tamasha hilo litafanyika Oktoba 8 hadi 12, huku Jijini Arusha tamasha hilo linatarajiwa kutafanyika Oktoba 8 hadi 13 mwaka huu.
Amesema tamasha hilo kutakuwa na shughuli mbalimbali kama vile sherehe za uzinduzi na kilele, kuenzi lugha adhimu ya Kiswahili na kutoa tuzo kwa wasanii na wadau wa Urithi.
Ameongeza kuwa Tamasha hilo litapambwa na shamrashamra za carnival ya mirindimo ya urithi, burudani za ngoma za asilil, muziki na kwaya pamoja n asana na maonesho ya bidhaa ya wadau.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo amesema kuwa Tamasha hilo litahusisha makongamano ya wataalamu, usiku wa urithi, ziara ya kutembelea vivutio vya utalii pamoja na kunadi urithi katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kupitia themes za Mvalishe, Misosi ya Kwetu na Michongo ya Urithi.
Tamasha la Urithi Festival litakuwa linafanyika kila mwezi Septemba ya kila mwaka kuanzia mwaka huu.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Urithi Festival walioshiriki kwenye mkutano wa Waandishi wa Habari uliofanyika leo jijini Dodoma. Tamasha hilo linalotarajiwa kuzinduliwa Septemba 15, 2018 na kuenzi, kudumisha, kuburudisha na kujifunza masuala muhimu yanayohusu Urithi wa Mtanzania hususani tamaduni zetu, historia, malikale na maliasili.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga akizungumza na Waandishi wa Habari leo jijini Dodoma kuwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli, anatarajia kuwa mgeni rasmi kwenye Tamasha la Mwezi wa Urithi linalotambulika kama ‘’Urithi Festival, Celebrating Our Heritage’’ litakalozinduliwa rasmi kitaifa katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma Septemba 15, 2018.
Baadhi ya Wajumbe wakiangalia nembo ya Urithi Festival inakayotumika kwenye Tamasha hilo.
(Picha zote na Lusungu Helela-WMU)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni