Mwakilishi kutoka Tanzania Health Promotion Support (THPS) ,Sisty Moshi akimkabidhi mbunge wa Chalinze ,Ridhiwani Kikwete msaada wa vifaa mbalimbali vilivyogharimu milioni 48.412 katika hospital ya wilaya ya Msoga.(picha na Mwamvua Mwinyi)
NA MWAMVUA MWINYI, CHALINZE
WADAU wa afya Tanzania Health Promotion Support (THPS) ,wametoa msaada wa vifaa mbalimbali vilivyogharimu milioni 48.412 katika hospital ya wilaya ya Msoga,Chalinze Mkoani Pwani .
Kati ya vifaa vilivyotolewa ni pamoja na mabenchi za wagonjwa 30, meza za ofisi kumi ,viti vya ofisini 12 ,makabati ya kuhifadhia nyaraka matatu na stool kwa ajili ya maabara 13.#
Akikabidhi vifaa hivyo kwa mbunge wa jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete ,mganga mkuu wa halmashauri ya Chalinze na uongozi wa hospital hiyo, mwakilishi kutoka THPS ,Sisty Moshi alisema ,wamewezesha vifaa hivyo ikiwa ni kuunga mkono juhudi za serikali katika sekta hiyo.
Alieleza ,kuanzia 2016/2018 wameshatoa vifaa tiba na samani zenye thamani zaidi ya milioni 761.508 mkoani Pwani, kati ya hivyo vifaa vilivyogharimu milioni 236.647.568 vilipelekwa Chalinze.
“Katika mradi huu wa kusaidia kuzuia maambukizi mapya ya VVU ,kutoa huduma,tiba na msaada wa kisaikolojia kwa ufadhili wa serikali ya Marekani , sisi tunafanya kazi katika mikoa ya Kigoma,Pwani na visiwa vya Zanzibar”
“Ufadhili huu unatokana na makubaliano kati ya serikali ya Tanzania na Marekani kufuatana na malengo ya kitaifa ” alifafanua Moshi.
Awali akitoa taarifa ya hospital ya wilaya ya Msoga ,mganga mkuu wa halmashauri ya Chalinze ,Rahim Hangai ,alisema hospital hiyo ilianza kutoa huduma za tiba kama zahanati tangu mwaka 1943 kikiwa na watumishi watatu .
“Ilipandishwa hadhi kuwa kituo cha afya mwaka 2016 baada ya rais mstaafu Jakaya Kikwete kujenga majengo mapya ndani ya eneo la zahanati ya Msoga.”
“Mnamo tarehe 12/10/2017 waziri wa afya ,maendeleo ya jamii ,jinsia ,wazee na watoto aliridhia na kutoa kibali cha kituo cha afya Msoga kuwa hospital ya wilaya ” alifafanua Hangai .
Hangai alisema ,hospital hiyo bado inakabiliwa na ukosefu wa jengo la utawala,ukosefu wa gari kwa ajili ya shughuli za kiutawala,upungufu wa watumishi na chumba cha kuhifadhia maiti.
Changamoto nyingine ni ukosefu wa jengo la maabara ,jengo la tiba na mafunzo kwa watu wanaoishi na VVU (CTC),jengo la mionzi ,ukosefu wa mashine ya X-ray ya ziada na chumba cha daktari na wodi ya wagonjwa wa akili.
Alisema vituo vya afya na hospital hiyo ,vimekuwa vikipokea majeruhi wengi wa ajali za barabarani kwa takwimu za julai 2016-juni 2017 vimepokea majeruhi 799 na wagonjwa waliokuwa na dharula 5,477 na wajawazito 4,678 .
Akikabidhiwa vifaa hivyo ,Ridhiwani aliwashukuru wadau hao na kuomba wadau wengine wasiwachoke kuendelea kuisaidia changamoto ambazo zinazoikabili hospital ya Msoga .
Ridhiwani alielezea kuwa ,halmashauri ya Chalinze inapitiwa na barabara kuu tatu ikiwemo Dar-es-salaam -Chalinze-Arusha,Chalinze -Msata-Arusha na Bagamoyo-Msata-Arusha.
Alibainisha ,vituo vya afya vilivyopo katika halmashauri hiyo vimekuwa vikipokea majeruhi wengi wa ajali za barabarani na magonjwa mengine hasa yatokanayo na kujaamiana ikiwemo (Ukimwi).
Halmashauri ya Chalinze ina jumla ya wakazi 240,326 ,kata 15,vijiji 71 na vituo vya kutolea huduma za afya 62 ikiwemo vya serikali vitano ,zahanati za serikali 39 na vilivyobaki ni vya watu binafsi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni