. Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma (pili kulia), Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi (pili kushoto), Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Bilinith Mahenge (kulia) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Profesa Sifuni Mchome wakiimba wimbo wa taifa kabla ya kuanza mkutano wa pili wa wanasheria walio kwenye utumishi wa umma unaofanyika Chuo cha Mipango, jijini Dodoma.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, akiwahutubia washiriki wa mkutano wa pili wa wanasheria walio kwenye utumishi wa umma (hawako pichani). Kwenye hotuba yake Profesa Juma amewaasa wanasheria walio kwenye utumishi wa umma kuzingatia misingi wa maadili kwenye utekelezaji wa majukumu yao.
Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, akitoa neno la utangulizi mbele ya wanasheria waliohudhuria mkutano wa pili wa wanasheria wa walio kwenye utumishi wa umma.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma (katikati waliokaa) kwenye picha ya pamoja na viongozi mbalimbali waliohudhuria ufunguzi wa mkutano wa pili wa wanasheria walio kwenye utumishi wa umma. Mkutano huo wa siku mbili unafanyika jiji Dodoma, ukumbi wa mikutano Chuo cha Mipango.
Wanasheria kutoka Wizara, Serikali za Mitaa, Mashirika, Wakala na Idara za Serikali wakifuatilia kwa makini hotuba ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibarhim Juma, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa pili wa wanasheria walio kwenye utumishi wa umma.
……………………….
Na. Idara ya Habari-MAELEZO
Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, amewaasa wanasheria walio kwenye utumishi wa umma kuzingatia misingi ya taaluma wakati wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku.
Kauli hiyo ameitoa wakati akifungua mkutano wa pili wa wanasheria walio kwenye utumishi wa umma unaofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Mipango, jijini Dodoma.
“Mkiwa maafisa wa Mahakama tunawatazamia kufanya kazi zenu kwa kuzingatia misingi ya taaluma iliyowekwa kwa kuzingatia maadili, weledi, uwazi na usiri” alisisitiza he Profesa Juma.
Profesa Juma pia amewakumbusha wanasheria hao walio kwenye utumishi wa umma kuhakikisha kuwa sheria wanazosimamia zinalenga kuleta ustawi wa wananchi wanyonge na kuiwezesha serikali kutimiza azma yake ya kifanya Tanzania iweze kufikia hadhi ya nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.
Vilevile, wanasheria hao wa serikali wameaswa kuzingatia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kutekeleza majukumu yao ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya karne ya 21.
Aliongeza kuwa, wanasheria wanalo jukumu kubwa la kukidhi matarajio ya wananchi ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025, amani, usalama, umoja, utawala bora, na kujenga uchumi imara.
Kabla ya Jaji Mkuu Profesa Juma, kuhutubia mkutano huo Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palagamba Kabudi alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kufanya mabadiliko katika muundo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambao unategemewa kuleta ufanisi. Kwenye mabadiliko hayo yaliyoidhinishwa na Rais Magufuli, yamesababisha kuanzishwa kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Wakili Mkuu wa Serikali.
Mkutano huo wa siku mbili unawakutanisha wanasheria zaidi ya mia tisa kutoka Wizara, Serikali za mitaa, Mashirika, Wakala na Idara mbalimbali za Serikali.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni