Mradi
mkubwa wa kijiji cha digitali cha Ololosokwan, Loliondo umezinduliwa
rasmi mwishoni mwa wiki, miaka miwili tangu kutiwa saini kwa uanzishwaji
wake kati ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni
(Unesco) na kampuni ya Samsung.
Hiki
kitakuwa ni kijiji cha nne cha digitali barani Afrika cha kwanza kikiwa
nchini Afrika Kusini huku kingine kikiwa Gabon na Ethiopia.
Kijiji
hicho cha digitali ni nadharia ya Samsung katika kurejesha faida kwa
umma na kina huduma mbalimbali ambazo zikiunganishwa na haja ya wananchi
zitasaidia kubadili maisha ya wamasai na kuondokana na utegemezi wa
mifugo pekee.
Uzinduzi
rasmi wa kijiji hicho umefanywa na Mkuu wa mkoa Arusha Mrisho Gambo kwa
niaba yaWaziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na watoto
Ummy Mwalimu.
Kijiji
hicho cha digitali kina shule yenye tehama ikiwa na maunganisho ya
intaneti, kiliniki ya kisasa ikiwa na kituo cha teknolojia ya
mawasiliano yenye kuwezesha utabibu (telemedicine) na jenereta
linalotumia nguvu za jua.
Mradi
huo ambao ulishuhudiwa utiaji saini na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya
Taifa ya UNESCO, Bi. Leah Kihimbi kutoka Wizara ya Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo na Dkt. N. Iriya kutoka Shirika la Afya Duniani
(WHO) Dar es Salaam na wafanyakazi wa UNESCO mwaka 2014, kukamilika
kwake kunawezesha UNESCO na serikali ya Tanzania kuwapatia wakazi wa
eneo hilo huduma bora za afya na vijana wa Kimasai nafasi ya kupata
elimu kutokana na ukweli kuwa kwa utamaduni na kazi zao za ufugaji
wamekuwa wakipata shida ya kupata elimu.
Utiaji
saini wake katika mwaka huo ulifanywa na Mkuu wa ofisi na Mwakilishi
Shirika la UNESCO nchini Bi. Zulmira Rodrigues na Mkurugenzi wa Samsung
Electronics nchini Tanzania, Bw. Mike Seo .Kupitia kijiji hicho vijana
wataendelea na masomo hata kama wanachunga mifugo yao kutokana na
kupatiwa tablet ambazo zitawawezesha kujifunza hata wakiwa nje
wakichunga mifugo yao.
Aidha
miongoni mwa manufaa makubwa yatakayopatikana katika mradi huo wa
kijiji cha digitali ni kuweza kupata nishati rahisi na iliyo rafiki kwa
mazingira kwa kuwepo na jenereta linalotumia nishati ya jua.Kuwepo kwa
kijiji hicho kunataka kudhihirisha ni kwa namna gani teknolojia inaweza
kutumika kuleta mabadiliko chanya yanayotakiwa kwa ajili ya maendeleo ya
wananchi waliopo vijijini.
Kijiji
hicho cha Loliondo ambacho kitakuwa cha nne katika vijiji vya
kidigitali barani Afrika kimeelezwa naMkuu wa mkoa wa Arusha Mheshimiwa
Mrisho Gambo kama utekelezaji wa Sera ya Tiba Mtandao kutokana na
kuzinduliwa kwa Kliniki Mtandao iliyopo katika Kijiji hicho.Katika
uzinduzi wa mradi huo kwa ujumla wake, kliniki ndicho kitu ambacho
kinaonekana kwenda karibu zaidi na wananchi wa Ololosokwan kwani itakuwa
inatoa huduma za afya, bora za kisiasa na za haraka kwa wakazi wa kata
za Soitsambu naa Oloipiri, Wilayani Ngorongoro.
Katika
hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa mkoa wa Arusha ,Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na watoto Mhe Ummi Mwalimu
wakati wa uzinduzi wa kliniki hiyo,alisema kuwa Tiba Mtandao imekua ni
miongoni mwa Vipaumbele vya Wizara yake ili wananchi wote Tanzania
waweze kupata huduma stahiki za matibabu pasipo kujali changamoto za
Kijiografia zinazotukabili,
Pamoja
na kufanya uzinduzi huo katika hotuba yake Mkuu wa mkoa wa Arusha,
Mrisho Gambo aliwashukuru wote walioshiriki kuleta Mradi huo wa maana
kwa mkoa wa Arusha kwani wangeweza kupeleka sehemu nyingine yeyote na
kuongeza kuwa ni deni kubwa sana lazima tuhakikishe huduma hiyo
imefanikiwa.
Akizungumzia
masuala ya afya kama kipaumbele katika mradi huo wenye lengo la
kuhifadhi utamaduni wa kimasai huku wakitumia teknolojia ya kisasa
kuleta maendeleo katika elimu na kuhifadhi mazingira, Mkuu huyo wa mkoa
akizungumza kwa niaba ya Waziri alisema kuwa kutokana na umuhimu wa
sekta ya afya kwa kila Mtanzania ,serikali itaelekeza nguvu katika
Kliniki hiyo ili kuiwezesha kutoa huduma stahiki na Kwa muda mrefu kwa
wananchi wa maeneo haya.
"Kliniki
hii ni ya kwanza Tanzania na itaweza kutoa huduma bora na za kisasa kwa
njia ya mtandao kwa wananchi zaidi ya elfu kumi kutoka katika maeneo
ambayo hapo awali wananchi walikuwa wanatembea umbali mrefu zaidi ya
Kilomita 50 kufuata huduma za afya".
"
Hii inadhihirisha kwamba mwananchi wa Ololosokwan na maeneo ya jirani
anaweza kuhudumiwa na daktari bingwa aliyeko Muhimbili au kokote Duniani
kupitia Klinik hii;na mfumo wa Mtandao uliopo unaruhusu upatikanaji wa
huduma hizi kwa kipindi chote cha mwaka mzima".
Aidha
aliitaka Halmashauri kutenga Bajeti kwa ajili ya kuongeza hadhi ya
zahanati hiyo kuwa Kituo cha Afya ambapo itaenda sambamba na kuongeza
majengo Pamoja na wataalam watakaoweza kutoa huduma stahiki Kwa
wananchi.
Upatikanaji
wa kituo cha Afya katika eneo hilo huku kukiwepo na kliniki mtandao
kutasaidia kuokoa maisha ya wananchi ambao wengi wao waliamini kupona
magonjwa makubwa ni mpaka uende KCMC au Muhimbili tu.
Awali
akizungumza katika uzinduzi huo Mkuu Shirika la Umoja wa mataifa
linaloshigulikia Elimu na Sayansi (UNESCO) nchini Tanzania Bi. Zulmira
Rodrigues alisema kijiji hicho ni ushuhuda tosha wa ukuaji wa teknolojia
unaenda sambamba na maono ya shirika la Unesco la kutoa kipaumbele
katika miradi ya sayansi inayosaidia wananchi wenye mahitaji moja kwa
moja.
Alisema
kwa kutambua adha waliyokuwa wanaipata wananchi wa Ololosokwan
walitengeneza mradi ambao sehemu mojawapo ni kliniki Mtandao ili kuleta
mabadiliko ya afya za watu kwa njia ya kisayansi.
Naye
mkurugenzi wa Tiba Kutoka Wizara ya Afya Dr. Margareth Evelyne Mhando
alishukuru Unesco kusaidia kutekeleza malengo ya Wizara kupitia Mradi
huu wa kijiji cha digitali na kuongeza kuwa ni hatua nzuri katika sekta
ya afya Kwa sababu hivi sasa wananchi waliombali na vituo vya Afya
kupitia Mradi huu watapata huduma bora kutoka Kwa matabibu wabobezi.
Uzinduzi
wa Mradi huu ulihudhuriwa pia na Balozi wa Switzerland Nchini Tanzania
Bi. Florence Mattli, Wawakilishi wa Samsung ambao ndio waliotoa fedha na
Teknolojia pamoja na wawakilishi kutoka Umoja wa Ulaya (EU).
Bi.
Mattli alisema kwamba wataendelea kusaka wadau wengine kuhakikisha
kwamba mradi huo unaendelea kutanuka na kufanikiwa kwa kujazia maeneo
ambapo panahitaji nguvu nyingine.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni