POLISI ARUSHA YATOA ONYO JUU YA WAHUSIKA WA BIASHARA YA BANGI




Mkuu wa Kikosi cha kutuliza Ghasia mkoa wa Arusha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Ramadhani Giro akiwa anaonyesha burungutu la madawa ya kulevya aina ya bhangi ambalo lilikuwa limehifadhiwa kwenye moja ya magunia yaliyopatikana katika kijiji cha Kismiri Juu wilayani Arumeru. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)


Mkuu wa Operesheni mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) James Manyama akiwa ameshikilia ndoo lenye mbegu za mmea wa bhangi mara baada ya operesheni iliyofanywa na jeshi la Polisi kijiji cha Kismiri wilayani Arumeru kumalizika. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)


Mmoja wa askari wa Jeshi la Polisi akiwa anaendelea na zoezi uchomaji wa bhangi katika kijiji cha Kismiri Juu, wilayani Arumeru wakati wa operesheni iliyofanyika katika eneo hilo. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)

Askari wa Jeshi la Polisi wakivusha moja ya gunia la bhangi lililofichwa katika korongo wakati wa operesheni ya bhangi iliyofanyika kijiji cha Kismiri wilayani Arumeru. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
……………………………………………………………………………
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Jeshi la Polisi mkoani hapa lipo kwenye mkakati wa kuwachukulia hatua viongozi wote wanaoishi au kufanyia kazi katika maeneo ambayo yatabainika wananchi wa maeneo yao wanalima bhangi bila wao kuwachukulia hatua zozote au kutoa taarifa kwa vyombo husika.
Hayo yameelezwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Naibu kamishna (DCP) Charles Mkumbo alipokuwa anaongea na waandishi wa habari ofisini kwake baada ya operesheni iliyofanyika katikati ya wiki iliyopita katika kijiji cha Kismiri Juu, kata ya Uwiro tarafa ya King’ori wilayani Arumeru,
“Mara kadhaa tunapofanya operesheni hizo wananchi wa eneo hilo huwa wanakimbia na kuacha nyumba zao huku viongozi wao kutoonekana kabisa au kutoa taarifa zozote juu ya uhalifu huo, sasa tutawachukulia hatua kwani wao ni sehemu ya uwajibikaji katika kuzuia vitendo vya uhalifu”. Alisema Kamanda Mkumbo.
Katika operesheni hiyo, jeshi la Polisi lilifanikiwa kupata jumla ya magunia 22 ya bhangi yaliyokuwa yamehifadhiwa katika nyumba za wakazi hao na kwenye makorongo yanayozunguka kijiji hicho pamoja na kilogramu 80 za mbegu za mmea huo ambazo zote ziliharibiwa kwa kuchomwa moto.
Kamanda Mkumbo aliendelea kueleza kwamba, katika operesheni hiyo pia walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja aitwaye Raphael Laizer (33) mkazi wa Kismiri Juu akiwa na magunia matatu ya bhangi huku taratibu za kumfikisha mahakamani zikiwa zinaendelea.
Kamanda Mkumbo aliongeza kwa  kusema kwamba, imekuwa vigumu kuwakamata watuhumiwa kutokana  na  jiografia ya eneo hilo ambapo kila kunapokuwa na operesheni askari wanapokwenda,  wananchi hao wanawaona kirahisi au kusikia miungurumo ya gari na kisha hukimbilia milimani na kuwaacha wazee na watoto.
“Japokuwa operesheni hizo ambazo tunazifanya mara kwa mara zimekuwa za mafanikio lakini changamoto zilizopo ni pamoja na miundo mbinu ya eneo hilo si rafiki kwa magari hasa uwepo wa milima mirefu na ubovu wa barabara”. Alifafanua Kamanda Mkumbo.
Operesheni hiyo iliyofanyika kuanzia saa 12:00 asubuhi mpaka saa 7:30 mchana ilijumuisha askari wa vikosi na vitengo mbalimbali huku ikisimamiwa na Mkuu wa Operesheni mkoani hapa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) James Manyama.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni