Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo leo ametekeleza
agizo la Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dr. John
Joseph Pombe Magufuli la kusitisha safari ya kwenda Mkoani Simiyu kwenye
sherehe za kwenda kuhitimisha kilele cha mbio za mwenge wa Uhuru kwa
kurejesha kiasi cha Jumla ya Shilingi 1,389,300 ambayo yalikuwa ni
malipo kwa ajili ya Mkuu wa Mkoa, Msaidizi wa Mkuu wa Mkoa , Dereva wa
Mkuu wa Mkoa na gharama za mafuta.
Kwa mujibu wa mchakato wa malipo ya posho kwa safari hiyo
ya kwenda mkoani Simiyu kwa siku tatu, posho ya RC ilikuwa ni Sh
360,000, Msaidizi wa RC Sh 240,000, posho ya dereva 240,000 na Sh
549,300 kwa ajili ya Mafuta ya gari.
Akiongea na mwandishi huyu ofisini kwake leo, Mkuu huyo wa
Mkoa wa Arusha amesema wakati agizo hilo linatolewa yeye alikuwa bado
hajaanza safari ya kuelekea Mkoani Simiyu, na kwamba amelipokea bila
kinyongo na mara moja akaamua kurejesha posho hiyo, akionesha stakabadhi
ya kuthibitisha hilo (pichani).
Pia Rc Gambo ameahidi kusimamia zoezi hilo kwa wahusika
wote mkoani Arusha na kuhakikisha wanatekeleza agizo hilo kwa wakati na
fedha hizo zielekezwe kwenye ujenzi wa madarasa kama sehemu ya
maandalizi ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza, darasa la kwanza
na darasa la awali kwa mwaka 2017.
Rais Dkt. Magufuli jana aliagiza viongozi wote wa Serikali
walioalikwa kuhudhuria sherehe za Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru
kitaifa zitakazofanyika tarehe 14 Oktoba, 2016 katika Wilaya ya Bariadi
Mkoani Simiyu kutohudhuria sherehe hizo na wale ambao walishalipwa fedha
ya posho na safari kwa ajili hiyo wazirejeshe.
Rais Magufuli alitoa maagizo hayo ikiwa ni utekelezaji wa
azma ya Serikali ya awamu ya tano ya kubana matumizi yasiyo ya lazima na
kuelekeza rasilimali nyingi katika shughuli za maendeleo ya nchi.
Viongozi waliotajwa kutakiwa kufuta safari zao za kwenda
Bariadi ni pamoja na Wakuu wote wa Mikoa, Wakuu wote wa Wilaya,
Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mameya na Wenyeviti
wote wa Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya pamoja na
watumishi ambao huambatana nao wakiwemo madereva na wasaidizi wao ambao
kwa idadi hufikia takribani 1,500.
Kwa kuwa sherehe za Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru
huambatana na Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Muasisi wa Taifa na
Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyefariki dunia
miaka 17 iliyopita, agizo hilo limewataka Viongozi wote wa Mikoa na
Wilaya kubaki katika maeneo yao ya kazi na kujiwekea utaratibu wa jinsi
ya kuienzi siku hiyo.
Aidha, Rais Magufuli aliagiza kuwa Wilaya zote ambazo
zimefanya vizuri katika shughuli za maendeleo wakati Mwenge ulipokuwa
katika maeneo yao, zitambuliwe kwa kutangazwa rasmi katika siku ya
kilele cha Mbio za Mwenge na kwamba zawadi zilizoandaliwa zitapelekwa
kwa wahusika kwa utaratibu utakaoelekezwa na Mamlaka inayohusika kutoa
zawadi hizo.
Hata hivyo Dkt. Magufuli ameelekeza kuwa kutokana na
umuhimu wa Mwenge wa Uhuru kwa Taifa, Viongozi wote wa Serikali ya Mkoa
wa Simiyu na Wilaya zake pamoja na wananchi wote wa mkoa huo wajitokeze
kwa wingi na kushiriki katika sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru siku
hiyo ya tarehe 14 Oktoba, 2016.
Mgeni Rasmi katika sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru
atakuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt.
Ali Mohamed Shein.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni