Mwanademokrasia wa kweli hahitaji vurugu

http://www.nationsonline.org/maps/political_world_map3000.jpg

KATIKA jamii yeyote iliyostaarabika, kutofautiana kimawazo ni jambo lililo la afya katika maendeleo yake ;na ndio msingi wa kupata wazo bora na linaloweza kuboreshwa katika ushindani wa hoja.

Ni tofauti hizo za mawazo kwa wastaarabu, hujenga maslahi na vikundi maslahi katika jamii na hata katika mifumo ya siasa na vyama vya siasa duniani kote.

Ndio maana katika nchi yenye demokrasia, ikiwemo Tanzania, uongozi hauna budi kusikiliza sauti na mawazo mbadala, ili kupata wazo bora linalokubalika la lenye maslahi kwa wote.

Kwa hili, hatuna budi kuipongeza Serikali na hasa Rais Jakaya Kikwete binafsi kwa kuwa kiongozi mwanademokrasia, aliye tayari kusikiliza mawazo ya pande zote, hata kwa wanaomzushia.

Mwishoni mwa wiki iliyopita katika hotuba ya kila mwisho wa mwezi, Rais Kikwete aliendelea kuonesha alivyo mwanademokrasia wa kweli, pale alipowaambia Kambi ya Upinzani, kuwa maoni yao kuhusu Muswada wa Sheria ya Katiba, yanazungumzika.

Aliwaambia kwamba hata baadhi ya maoni hayo, yangeweza kukubalika kama wabunge wake wangekuwepo bungeni, ambako ndio chombo cha kuwasilisha mawazo mbadala na kujenga wazo bora.

Alisema bahati mbaya hawakuwepo, hivyo hapakuwepo mtu wa kusema mawazo yao na baada ya kupoteza fursa yao halali, kutaka kupata ufumbuzi nje ya Bunge ni jambo lisilowezekana. Alisisitiza kuwa masuala yanayohusu Bunge, hujadiliwa na kuamuliwa bungeni na si vinginevyo.

Pamoja na kambi hiyo iliyoundwa na NCCR-Mageuzi, CUF na Chadema, kupoteza fursa halali ya kutoa maoni yao bungeni, ambayo hutumiwa na nchi zote zilizokomaa kidemokrasia, Rais Kikwete amewapa fursa nyingine ya kukutana nao kati ya Jumapili ya Oktoba 13 mwaka huu, ama Jumanne ya Oktoba 15.

Uungwana huu wa Rais Kikwete kwa kweli ni wa kuungwa mkono, lakini pia unapaswa kuigwa na wanasiasa na vyama vyote vya siasa, kama kweli vinataka kushika dola na kuongoza taifa ambalo msingi na uimara wake ni umoja, mshikamano na undugu unaostawi katika jamii yenye utii wa sheria.

Tunasema hivyo kwa kuwa kila mmoja ni shahidi kuwa vyama hivyo havijakomaa kisiasa, kiasi cha kupewa dola, ambayo kuiongoza lazima watu wake wawe na umoja, mshikamano na udugu utakaostawishwa na uongozi unaoamini katika utii wa sheria.

Hakuna ambaye hakusikia viongozi hao, ambao baadhi yao wamewahi kuomba kura ili waongoze taifa hili, wakitamka hadharani kuwa watahamasisha Watanzania wasitii sheria na kubatiza Oktoba 10 mwaka huu kuwa siku ya kutotii sheria.

Tumejiuliza hivi kweli kiongozi anayetaka kuongoza taifa hili, kama ameiva na kukomaa kisiasa, anaweza kutangaza siku ya kutotii sheria?

Siku ambayo haina tofauti na kuhamisha watu kuvunja na kuiba mali za walipa kodi wanaowapa viongozi hao ruzuku kila mwezi kupitia vyama vyao?

Tumesikitika kuona viongozi hao wa vyama vinavyoungwa mkono na wananchi, wakihamasisha wananchi hao hao wasitii sheria, lakini tumefarijika, kusikia wamekubali busara za Rais Kikwete za kukaa meza moja na kumaliza tofauti zao.

Tunashauri kukitokea tofauti tena, ambazo tuna hakika zitatokea katika mambo mbalimbali tu kwa kuwa ndivyo jamii iliyostaarabika ilivyo, basi tuepuke kutoa kauli za namna hiyo, za kushawishi wananchi wasitii sheria, kwa kuwa ni kauli za jabu ambazo hakuna mwanademokrasia makini anayeweza kuziunga mkono.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni