MAWAKILI WATUMIA MASAA MAWILI KUISHAWISHI MAHAKAMA KESI YA UBUNGE LONGIDO

Na Mahmoud Ahmad Arusha.
Mawakili  Method Kimomogoro na John Materu,jana walitumia masaa mawili  kuishawishi  Mahakama ya   Rufaa iliyochini ya majaji watatu Sauda Mjasiri, Mussa Kipenka, na Profesa Juma Musaa
  kutengua hukumu ya Mahakama Kuu ya jaji Sivangirwa Mwangesi kwa kumtangaza Nangole kama   mshindi halali wa kiti cha ubunge wa Jimbo la Longido.

  Aidha katika hoja zao sita walizowasilisha waliiomba Mahakama ya Rufaa kufuta hati iliyotolewa na Jaji   Mwangesi ikimjulisha Mkurugenzi wa Uchaguzi kwamba matokeo ya Jimbo la   Longido yalifutwa na Mahakama Kuu.

  Mawakili hao waliiomba Mahakama ya Rufaa kuamuru kwamba Dk Kiruswa ambae ni mjibu maombi   alipe gharama za kesi katika Mahakama Kuu na gharama za Rufaa hii.

  Walidai kuwa Jaji Mwangesi alikosea kisheria kwa kushindwa kuamua   iwapo kilichotokea kwenye chumba cha majumuisho ya kura ilikuwa vurugu   au mzozo tu wa maneno.

  Pia walidai  Jaji alikosea kwa kutotamka kwamba Dk Kiruswa aliamua   kuondoka kwenye chumba cha majumuisho ya kura kwa makusudi na utashi   wake mwenyewe.

  Hoja nyingine ni kwamba Jaji alikosea pale alipotamka kwamba mazingira   ya chumba cha majumuisho ya kura yasingeruhusu majumuisho ya kura   ambayo yanaendana na utashi wa wapiga kura katika jimbo la Longido.

  Wamedai Jaji alipotoka kwa kusema kulikuwa na kasoro nyingine tano   zilizosababisha Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo kutangaza matokeo bila   ya kuwapo kwa Dk Kiruswa.

  Na hoja ya sita ni walidai kwamba Jaji alikosea kisheria kwa
  kutotambua ujanja wa Dk Kiruswa alipodai eti kwamba yeye na timu yake   hawakuwahi kufanya majumuisho yao wenyewe ya kura alizopata kwa mujibu   wa fomu 21B za vituo vyote 175 va Jimbo la Longido.

 Awali , Dk Kiruswa kupitia kwa  mawakili watatu  Dk   Masumbuko Lamwai aliyekuwa akisaidiwa na David Haraka na Edmund  Ngemera, waliwasilisha rufaa kinzani (cross appeal) yenye sababu mbili ambazo hazikuzuia mahakama kuendelea kusikiliza shauri hilo.
Katika maamuzi yake mahakama hiyo chini ya jaji kiongozi wa jopo la majaji watatuSauda Mjasiri alisema maamuzi yote kuhusiana na shauri hilo watayatoa katika maamuzi yao ya mwisho ndani ya muda mfupi ambao umepangwa kusikilizwa kwa mashauri yote ya rufaa.
Katika kujibu hoja za upande wa watuma maombi wakili Lamwai aliomba mahakama kuukubali uamuzi uliotolewa na jaji mwangesi kwani ulizingatia misingi yote ya kisheria.
Alisema kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani hakukua na shaka kuwa uchaguzi ulikiuka misingi yake na njia pekee ilikua ni kuufuta na kurudia upya.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni