TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

      

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA RAIS
TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA

Mkurugenzi wa Jiji
Simu:
Nukushi:
+255 27 2508073/2503494 (Director)
+255 27 2544330 (General)
+255 27 2545768
S. L. P.  3013,
20 Barabara ya Boma,
23101 ARUSHA,
Barua Pepe:  cd@arushacc.go.tz
Tovuti:  www.arushacc.go.tz




UFAFANUZI JUU YA TAARIFA YA UZUSHI ILIYOTOLEWA KWENYE MITANDAO YA KIJAMII
Halmashauri ya Jiji la Arusha inakanusha taarifa ya uzushi na upotoshaji iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii jioni ya leo tarehe 17.10.2016 ikimuhusisha Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Ndg. Athumani Kihamia pamoja na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Arusha Mhe. Catherine Magige.
Taarifa hiyo ya kughushi iliyochapishwa kwa kutumia nembo ya Jiji la Arusha imetengenezwa na watu wenye nia ovu na dhamira mbaya kwa malengo ya kupunguza kasi ya utendaji wa Mkurugenzi wa Jiji la  Arusha Ndg. Athumani Kihamia pamoja na Serikali Mkoani Arusha kwa  ujumla.  
Aidha taarifa hiyo ya uzushi imebeba ujumbe wa kutunga wenye kusudio maalum la kumchonganisha Mkurugenzi wa Jiji la Arusha na mamlaka nyingine ikiwemo Mamlaka yake ya Uteuzi ili kumchafulia jina na kumgombanisha na Mamlaka hiyo.
Halmashauri ya Jiji la Arusha inaziomba Mamlaka zinazohusika na ufuatiliaji wa uhalifu wa mitandao zikiwemo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA) na Jeshi la Polisi Nchini kufuatilia watu wote walioshiriki upotoshaji na uhalifu huo wa kimtandao na kughushi ili kuwatia nguvuni na kuwachukulia hatua kali za Kisheria ili iwe fundisho kwao na watu wengine wenye tabia ya aina hiyo.
Hata hivyo Halmashauri ya Jiji la Arusha inapenda kuujulisha Umma kuwa, Mkurugenzi wa Jiji  ataendelea kwa mujibu wa Sheria, Taratibu  na kanuni zilizopo kusimamia maslahi ya Umma, kudhibiti mapato na matumizi ya Fedha za Umma ili kuhakikisha maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kutaka Fedha nyingi zitumike kwa ajili ya shughuli za maendeleo na hasa kuwahudumia wanyonge inatekelezwa ipasavyo. Pia Halmashauri ya Jiji inatoa wito kwa wadau wote ndani ya Jiji la Arusha kuunga mkono jitihada hizo za kuwahudumia wanyonge.
Halmashauri ya Jiji inapenda kuwaarifu watanzania wote kuipuuza mitandao inayotoa habari za uzushi na kupuuza habari hiyo na nyinginezo za uzushi zinazoenezwa dhidi ya viongozi kwani hazina ukweli wowote zaidi ya uchochezi na uchonganishi.
Aidha Halmashauri ya Jiji la Arusha inawashauri wahusika wote wa uzushi huu kuacha kupoteza muda badala yake waungane na Serikali katika utekelezaji wa Kauli Mbiu ya HAPA KAZI TU.
Nteghenjwa Hosseah
Afisa Habari, Halmashauri ya Jiji
Arusha.
17  Oktoba,2016

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni