Mkurugenzi wa mawasiliano wa taasisi ya Mfuko wa Wanawake Afrika, Anna Salado (kulia), akipakua mboga zilizopikwa kiasili na kuungwa kwa nazi wakati yeye na ujumbe wake walipotembelea mradi wa ukaushaji wa mboga na matunda wa wanawake wa Kata ya Mzinga mkoani Morogoro hivi karibuni. Kushoto ni Naibu Meya wa Manispaa ya Morogoro, Milikieli Mansweat Mahiku.
Mratibu wa mradi wa Green Voices kutoka taasisi ya Mfuko wa Wanawake Afrika ya Hispania, Alicia Cebada, akiwa ameshikilia pakiti ya kisamvu kilichokaushwa na kufungashwa huku akiwapongeza wanawake wa kikundi cha Mzinga katika Kata ya Mzinga, Manispaa ya Morogoro kwamba wamefanya kazi nzuri sana. Mwenye fulana nyeupe ni Bi. Esther Muffui, mshiriki kiongozi wa mradi huo.
SIYO tu mapishi ya asili ya kisamvu kikavu kilichoungwa kwa nazi, lakini mafanikio makubwa katika ukaushaji na usindikaji wa mboga na matunda katika mradi wa wanawake wa Kata ya Mzinga, Manispaa ya Morogoro yamewavutia wahisani wa taasisi ya Women for Africa Foundation kutoka Hispania.
Hali hiyo imewafanya wanawake hao wawe katika nafasi kubwa zaidi ya kusonga mbele ikiwa wafadhili hao watatoa tena fedha katika awamu ya pili ya mradi wa Green Voices unaotekelezwa nchini Tanzania.
Akizungumza katika Kijiji cha Konga kwenye Kata hiyo, mratibu wa mradi huo kutoka Hispania, Bi. Alicia Cebada, alisema kwamba licha ya kuwa na muda mfupi tangu kuanza kwa mradi huo, lakini wanawake hao wamefanya mambo makubwa ambayo yanastahili kuungwa mkono.
“Hii teknolojia ya ukaushaji wa mboga na matunda ni rahisi na inafaa sana kwa uhifadhi wa chakula, kinachotakiwa ni kwa wanawake hawa kuwezeshwa zaidi,” alisema Alicia ambaye aliongozana na Mkurugenzi wa habari wa taasisi hiyo, Anna Salado, na ofisa mwandamizi wa taasisi hiyo anayeshughulikia masuaa ya ubunifu, Bi Noellia pamoja na mratibu wa Green Voices Tanzania, Bi. Secelela Balisidya.
Alicia alisema kwamba, changamoto ndogo wanazokabiliana nazo wamezisikia, lakini akasema katu zisiwakatishe tamaa kwa sababu inaonyesha dhahiri wanaweza kufanya mambo makubwa mbele ya safari.
Maofisa wa taasisi ya Mfuko wa Wanawake Afrika kutoka Hispania wakiwa katika picha ya pamoja na wanakikundi wa Mzinga (wenye sare). Kulia ni mratibu wa mradi wa Green Voices nchini Tanzania, Bi. Secelela Balisidya.
Naibu Meya wa Manispaa ya Morogoro, Milikieli Mansweat Mahiku (wa nne kutoka kulia), akiwa katika picha ya pamoja na maofisa wa Mfuko wa Wanawake Afrika na washiriki wa mradi wa Green Voices Tanzania.
Taasisi ya Women for Africa Foundation mbayo ni Mfuko unaoshughulikia maendeleo ya Wanawake wa Afrika, ikiongozwa na makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandez de la Vega Sanz, ndiyo inayofadhili mradi wa Green Voices ambao unatekelezwa Tanzania pekee.
Hata hivyo, taasisi hiyo inafadhili miradi 15 ya wanawake katika nchi 12 barani Afrika ambayo imeonyesha mafanikio, huku mradi wa Green Voices ukitajwa kuwa na mafanikio makubwa katika kipindi kifupi.
Miongoni mwa changamoto ambazo wanawake hawa wasindikaji wanakabiliana nazo ni pamoja na makaushio ya umeme-jua (solar power) pamoja na masoko ya uhakika na vifaa vya kufungashia.
Mshiriki kiongozi wa mradi huo wa Mzinga Green Voices, Esther Muffui, alisema kwamba kaushio walilonalo kwa sasa ni dogo kuliko mali ghafi zilizopo na akaongeza kwamba itakuwa vyema kama walau kutakuwa na kaushio moja kwa kila wanawake watatu.
“Hapa Mzinga wanawake na jamii nzima wanalima mboga mboga na matunda kwa wingi, lakini kaushio tulilonalo ni moja tu ambapo haliwezi kutosheleza mahitaji, kama tutawezeshwa zaidi na walau kukawepo kaushio moja kwa kila wanawake watatu itasaidia sana hata jamii nzima ya hapa,” alisema.
Ujumbe huo ulifurahishwa zaidi baada ya kupata mlo wa mboga kavu zilizoungwa kwa nazi na karanga pamoja na wali wa nazi, ambapo siyo tu walishangazwa na mapishi hayo ya asili, bali pia walistaajabu namna ukaushaji huo usivyoathiri ubora wa mboga hizo.
Mratibu wa mradi wa Green Voices kutoka Hispania, Alicia Cebada, akiuliza jambo kuhusu namna ya ukaushaji wa matunda.
Mshiriki kiongozi wa kikundi cha Mzinga Women Group, Esther Muffui (wa pili kushoto), akitoa maelezo ya namna ya kukausha matunda katika mradi wa Green Voices kwenye Kata ya Mzinga mjini Morogoro.
Naibu Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Milikieli Mansweat Mahiku, alisema kwamba, atahakikisha anasimamia kwa bidii ili teknolojia hiyo iweze kusambaa kwa wanawake wote wa manispaa hiyo, ambayo inafahamika kwa uzalishaji wa mboga na matunda kwa wingi.
Mhe. Mahiku, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mzinga, alisema kwamba, kuanzishwa kwa mradi huo kutawachochea wanawake wengi kuingia kwenye ujasiriamali wa kilimo cha mboga mboga na matunda, kwa kuwa sasa hayawezi kupotea kama zamani.
Aidha, aliahidi kwamba, yeye na madiwani wenzake watahakikisha asilimia 10 ya fedha za maendeleo katika halmashauri wanapatiwa wanawake na vijana wanaofanya miradi endelevu yenye tija na inayolenga kutunza mazingira kama wanavyofanya wanawake hao wa Mzinga.
“Sasa hivi bajeti ya maendeleo ya halmashauri imeongezwa hadi asilimia 60, sasa kati ya fedha hizo, asilimia 10 ni miradi ya wanawake na vijana, ambayo kama tutaisimamia vyema na kuielekeza kwenye miradi endelevu kama hii italeta tija.
“Kama wahisani hawa wamejitokeza na wamekuja kutoka Hispania, sisi kama serikali nasi tunapaswa kuunga mkono jitihada hizi ambazo zina tija kubwa,” alisema Mstahiki Meya.
Hata hivyo, aliitaka jamii kubuni miradi mbalimbali endelevu na kuacha kuisubiri serikali ifanye kila kitu.
Mradi huo wa ukaushaji wa mboga na matunda umeanzishwa mwezi Machi mwaka huu baada ya Bi. Esther na wanawake wengine 14 kupatiwa mafunzo nchini Hispania ya ujasiriamali unaoendana na utunzaji wa mazingira na uelewa kuhusu mabadiliko ya tabianchi.
Miradi mingine inayotekelezwa kupitia Green Voices Tanzania ni kilimo cha viazi lishe Ukerewe, usindikaji wa mihogo Kisarawe, ufugaji nyuki Kisarawe, utengenezaji wa majiko banifu Mkuranga, kilimo cha matunda Uvinza – Kigoma, kilimo cha uyoga Boko na Bunju, Dar es Salaam, kilimo hai cha mboga mboga Kinyerezi, Dar es Salaam, ufugaji nyuki Dakawa, Morogoro, na utengenezaji wa majiko ya umeme-jua Kilimanjaro.
Bi. Esther Muffui, mshiriki kiongozi wa kikundi cha Mzinga Women Group mjini Morogoro kinachotekeleza mradi wa Green Voices kwa ukaushaji wa mboga na matunda, akieleza jambo wakati ujumbe kutoka taasisi ya Mfuko wa Wanawake Afrika ulipotembelea mradi huo hivi karibuni.
Matayarisho ya mboga mbichi kabla ya kuikausha.
Hapa sasa mboga inasambazwa tayari kwa kuwekwa kwenye kaushio.
Na walipatiwa zawadi maalum kwa ukumbusho. Hapa Alicia Cebada akivishwa skafu yenye rangi za bendera ya Tanzania.
Maofisa wa Mfuko wa Wanawake Afrika, Alicia na Anna Salado wakiserebuka katika ngoma ya Kirugulu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni