MHE. GODBLESS LEMA AFUNGUA WARSHA YA AFYA YA UZAZI NA UKIMWI KWA VIJANA JIJINI ARUSHA

Kukosekana kwa maadili katika ngazi ya familia na taifa kwa ujumla ni miongoni mwa vitu vinavyochangia ongezeko la maambukizi ya magonjwa ya ngono ikiwemo UKIMWI hasa kwa vijana.
Kauli hiyo imetolewa na Mbunge wa jimbo la Arusha mjini Mh Godbless Lema wakati akifungua warsha ya afya ya uzazi na elimu ya virusi vya ukimwi kwa vijana wadogo ambapo yeye alikuwa mgeni rasmi katika warsha hiyo iliyofanyika jijini Arusha hii leo.
Mh. Lema amesema imekuwa kawaida sasa jamii hasa vijana kutokuwa na hofu ya kufanya vitendo vya ngono ambapo kutokana na sababu mbalimbali wengi wao wamekuwa wakifanya bila kutumia kinga jambo ambalo linachangia maambukizi hayo kupanda kwa rika hilo.
Ametaja sababu hizo kuwa ni umasikini, utandawazi, ulevi kuwa ni miongoni mwa vitu vinavyochangia maambukizi kwa vijana huku akiishauri serikali kuangalia na kuchukua hatua mapema ya kupunguza urahisi wa kupatikana kwa vilevi (pombe) kwani kutokana na wingi wa maeneo na urahisi wa kupata vilevi kunachangia vijana kulewa na kufanya maamuzi yasiyosahihi katika ngono.
"Serikali yetu ipunguze ama iweke ugumu wa watu kupata pombe. Siku hizi kila mahali pana grocery, pub au baa...Na hapa Arusha unakuta watu wanatembeza pombe kwenye mabox wanaziuza kama pipi. Hii inapelekea hata mtu aliyekuwa hana mpango wa kwenda baa kuinunua pombe kwa kuwa ipo hapo alipo, sasa tunategemea nini baada ya huyo mtu kulewa" amesema Lema.
Pamoja na mambo mengine ameishauri jamii kufuata imani za dini zao zinavyoelekeza kuhusu vitendo vya ngono, huku akiitaka serikali kupitia mamlaka zake kuhakikisha wanasimamia ipasavyo sera za nchi zinazohusu UKIMWI na kuwataka wenye mamlaka kutokuwa sehemu ya tatizo kwa kuwa hawataweza kuwakemea watu kwa vitendo.
Kwa upande wake Bi Grace Kessy Afisa vijana kutoka tume ya taifa ya Kudhibiti UKIMWI nchini TACAIDS amesema maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwa vijana bado yapo juu karibia asilimia 2 kwa vijana huku akisema kila mmoja kwa nafasi yake bado ana kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha vijana wanakuwa na afya bora na wanapata huduma zile wanazostahili kupata.
Amesema tume imepanga mipango mikakati kwa kila mkoa nchini yenye kulenga kuwafikia vijana kwa kuwa kila mkoa maambukizi ya VVU kwa vijana kinatofautiana tofautiana baina ya mkoa mmoja na mwingine, hivyo mipango hiyo itasaidia kutambua tatizo linalochangia maambukizi hayo na namna ya kufanya kwa kila mkoa huku akiwataka wadau wanaofanya kazi na tume ya taifa ya kudhibiti UKIMWI( TACAIDS) waweze kuzingatia mipango mikakati hiyo iliyopo kwenye mikoa
 Washiriki wakimsikiliza mgeni rasmi
 Afisa Vijana TACAIDS Bi Grace Kessy akizungumza kwenye warsha hiyo
 Mbunge wa Arusha mjini Godbless Lema akitoa hotuba ya ufunguzi wa warsha hiyo jijini Arusha
 Picha ya pamoja ya washiriki pamoja na mgeni rasmi Mh. Godbless Lema
Mbunge Godbless Lema akiagana na mmoja kati ya wawezeshaji wa warsha hiyo mara baada ya ufunguzi 
Na Edwin Moshi wa Eddy Blog

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni