Afisa Madini Mkazi, Mkoa wa
Kilimanjaro, Fatuma Kyando akielezea sheria na kanuni za uchimbaji wa
madini nchini katika mafunzo yaliyoshirikisha wachimbaji wa madini
Mirerani kuanzia tarehe 25 hadi 26 Julai, 2015. Lengo la mafunzo hayo
lilikuwa ni kuwapa uelewa juu ya huduma za leseni kwa njia ya mtandao.
Mtaalam kutoka Wizara ya Nishati
na Madini, Kitengo cha Leseni Charles Gombe (kulia) akihakiki leseni ya
mmoja wa wachimbaji (katikati) Kushoto ni Afisa Madini katika Ofisi ya
Madini, Mirerani, Denis Mrengo
Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kaskazini Alex Magayane (kulia) akifungua mafunzo hayo.
Baadhi ya washiriki wa semina hiyo wakifuatilia kwa makini mada zilizokuwa zinawasilishwa kwa nyakati tofauti.
Mjiolojia katika Ofisi ya
Afisa Madini Mkazi -Mirerani, Amir Chande Ramadhani (kushoto) na Mtaalam
kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Kitengo cha Leseni Charles Gombe
(kulia) wakifuatilia tovuti ya huduma za leseni kwa njia ya mtandao
(online mining cadastre transactional portal) kwenye mafunzo hayo.
……………………………………………………………………
Na Greyson Mwase, Arusha
Imeelezwa kuwa ili kuondokana na
migongano kwenye usimamizi wa sekta ya madini Kanda ya Kaskazini,
Wizara ya Nishati na Madini imeandaa mafunzo kuhusu sekta ya madini
yatakayoshirikisha viongozi mbalimbali katika mikoa ya Manyara, Arusha
na Kilimanjaro yanayotarajiwa kufanyika Agosti 12, mwaka huu.
Akizungumza katika mahojiano
maalum jijini Arusha jana, Afisa Madini Mkazi, Mkoa wa Kilimanjaro,
Fatuma Kyando alisema kuwa mafunzo hayo yatashirikisha wakuu wa wilaya,
wakurugenzi wa halmashauri, maafisa tawala wa wilaya, watendaji na
wenyeviti wa vijiji na kata na wawakilishi kutoka Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA)
Alieleza kuwa katika usimamizi wa
sekta ya madini katika kanda hiyo, kumekuwepo na mgongano wa mamlaka
ambapo kila upande umekuwa ukiona una nguvu kuliko mwingine kwenye
utoaji na usimamizi wa leseni za madini.
Alisema ni vyema kila mamlaka
ikafahamu majukumu na mipaka yake katika usimamizi wa shughuli za
madini ili kuzuia migogoro inayoweza kujitokeza.
Alisisitiza kuwa kati ya mambo
watakayojifunza ni pamoja na sheria na kanuni za madini, utunzaji wa
mazingira katika shughuli za madini na fursa za madini yaliyopo.
Akielezea changamoto nyingine
katika usimamizi wa shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini katika
kanda hiyo, Kyando alisema kumekuwepo na migongano kwenye tozo la kodi
kwenye mapato yatokanayo na madini.
Alisema mapato wanayokusanya
wamekuwa wakiwasilisha serikali huu ambapo fedha hizo hurudishwa
tena kwenye halmashauri kwa ajili ya kuimarisha huduma za jamii
lakini bado watu wamekuwa wakihoji kwanini fedha hizo zisilipwe moja
kwa moja tu kwenye halmashauri na kutumika kwa maendeleo moja kwa moja.
Aliongeza kuwa hali hii inatokana
na wananchi na viongozi kutokuwa na uelewa wa sheria na kanuni za
madini na ndio maana ofisi yake imeandaa mafunzo hayo.
Alisema kuwa mafunzo hayo
yatawawezesha mamlaka zote kuwa na lugha moja na kufanya kazi kwa
pamoja na kuzuia migogoro inayoweza kujitokeza.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni